Na Mwandishi Maalum
New York
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesisitiza kuwa silaha ndogo ndogo na nyepesi bado ni tishio kwa maisha ya watu na mali zao katika nchi nyingi za Afrika zikiwamo za Maziwa Makuu.
Na kwa sababu hiyo, Tanzania imetaka majadiliano kuhusu upokonyaji na ukomeshaji wa matumizi ya silaha za maangamizi zikiwamo za nyukilia yalenge pia katika ukomeshaji na upokonyaji silaha ndogo ndogo na nyepesi.
Msisitizo huo umetolewa na Mwakilishi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Ombeni Sefue , alipokuwa akichangia mjadala kuhusu ukomeshaji, upokonyaji , ulimbikizaji na matumizi ya silaha za maangamizi .
Mjadala huo ambao unazihusisha nchi 193 wanachama wa UM , unafanyika nchini ya usimamizi wa Kamati ya kwanza ya Baraza Kuu la 66 la Umoja wa Mataifa. Kamati hiyo pamoja na mambo mengine ndiyo yenye dhamana ya masuala yote yanayohusiana na udhibiti wa silaha.
Balozi Ombeni Sefue, ameeleza kuwa, Tanzania inasisitiza matumizi haramu ya silaha ndogo ndogo na nyepesi kupewa uzito unaostahili katika majadiliano hayo, kutokana na ukweli kwamba silaha hizo zimekuwa chanzo kikubwa cha machafuko,uvunjifu wa amani na ongezeko la matukio ya uhalifu yakiwamo ya uharamia na biashara ya dawa za kulevya.
“Silaha zote bila ya kujalisha ni za aina gani zinaathari kubwa kwa maisha ya watu na mali. Ni kwa sababu hiyo tunasisitiza kwamba majadiliano kuhusu upokonyaji wa silaha usibague aina ya silaha”.
Akasema kuwa Tanzania inasikitishwa na namna ambavyo silaha hizo zimendelea kuwa tishio na kusema .“Tunaishi katika dunia ya utandawazi, madhara ya kuenea kwa silaha hizi ndogo ndogo na nyepesi yanatugusa wote. Kwa hiyo ni wajibu wetu kushirikiana kwa pamoja siyo tu katika kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa kupunguza silaha za maangamizi zikiwamo za nyukila bali pia katika upunguzaji na upokonyaji wa silaha ndogo ndogo na nyepesi” akasisitiza Balozi Sefue
Na kuogeza. “ Ubaguzi wa aina yoyote kati ya makundi haya mawili ya silaha ni sawa na kuwabagua binadamu”.
Akizungumzia mchango wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika upunguzaji wa matumzi ya silaha za maangamzi zikiwamo silaha ndogo na nyepesi.
Balozi Sefue anasema, ingawa Tanzania haina silaha za nyukilia au za maangamizi, imekwisha ridhia mikataba mbalimali ya kimataifa na kikanda inayolenga katika kulitafutia ufumbuzi tatizo la matumizi ya silaha hizo pamoja na kulifanya bara la Afrika kuwa bara huru dhidi ya silaha za nyukilia.
Aidha akasema, Tanzania haiungi mkono nchi yoyote ile kujilimbikizia silaha za maangamizi zikiwamo za nyukilia.Na kwamba Tanzania inaamini kuwa dunia inaweza kuwa mahali pa amani na salama zaidi pasipo kuwa na silaha hizo.
Akatumia fursa hiyo kuzipongeza Marekani na Urusi kwa kuingia makubaliano ya upunguzaji na ulimbikizaji wa silaha za nyukilia na akazishauri nchi nyingine kuiga mfano wa nchi hizo mbili.
Katika hatua nyingine Tanzania imebainisha kuwa ugaidi unaendeleo kuwa changamoto kwa usalama na amani ya kimataifa,
Akizungumza wakati wa majadiliano kuhusu juhudi za kukabiliana na ugaidi, Balozi wa Tanzania katika UM.Ombeni Sefue amesema kuendelea kujirudia kwa matukio ya ugaidi kunaonyesha dhahiri kwamba hakuna nchi ambayo iko salama.
Akasema cha kutisha zaidi ni hali ya ugaidi huo kutobagua hata vyombo vinavyosimamia na kutetea haki za binadamu, usalama na ustawi wa jamii kama Umoja wa Mataifa.
Akatoa mfano wa hivi karibu ambapo tukio la kigaidi lilihusisha majengo ya Umoja wa Mataifa huko Abuja, nchini Nigeria tukio liliposababisha pia upotevu wa maisha ya watu wasio na hatia.
Aidha Balozi Sefue amesema Tanzania inasikitishwa na mkwamo wa maandalizi ya rasimu ya mkataba kuhusu ugaidi kutoka na tofauti za kimitizamo zikiwamo za tafsiri sahihi na inayokubalika kuhusu neno ugaidi.
Tanzania kupitia mwakilishi wake, imezitaka nchi zote kuonyesha utashi wa kisiasa ili kusukuma mbele mchakato wa maandalizi ya Mkataba huo.
“Kwa pamoja tunaweza kama tukitaka kuratibu na kushirikiana kwa karibu kuzitafutia ufumbuzi ajenda zinazotukwamisha kukamilisha rasmu ya Mkataba kuhusu Ugaidi”.akasema Balozi Sefue.
mwisho
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269