Na Mwandishi Maalum
New York
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Philippines zitaanda mkutano wa kilele wa wakuu wa nchi na serikali utakaojadili haki na fursa za watu wenye ulemavu .
Hayo yameelezwa na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa mataifa, Ombeni Sefue, wakati alipokuwa akizungumza katika mkutano wa Kamati ya Tatu ya Baraza Kuu la 66 la Umoja wa Mataifa.
Kamati ya Tatu ni kati ya Kamati Sita za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Na ni kamati inayohusika pamoja na mambo mengine masuala yote yanayohusu maendeleo na ustawi wa jamii, misaada ya kibinadamu, wakimbizi, haki za binadamu, haki za makundi mbalimbali wakiwamo wanawake, watoto, na wazee.
Balozi Ombeni Sefue, Tanzania inaamini kwamba kuna uhusiano mkubwa kati ya umaskini na ulemavu na ndiyo maana imekubali kuandaa mkutano kwa kushirikiana na Philippines. Mkutano huo unatarajiwa kufanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, mwezi Septemba 2012.
Amefafanua kwa kueleza kwamba, ili watu wenye ulemavu waweze kuondokana na umaskini kama ilivyo kwa makundi mengine ya jamii. Jumuia ya kimataifa inatakiwa kuweka mikakati ya makusudi ya kulisaidia kundi hilo.
“Nchi yangu kwa kushirikiana na Philippines tutaanda mkutano wakilele wa wakuu wa nchi na serikali kuhusu watu wenye ulemavu, naomba kutumia fursa hii kuwaomba mtuunge mkono kwa kuridhia azimio tunalolianda kuhusu walemavu na mkutano tutakouandaa. akasema Balozi.
Tayari nchi hizo mbili zimeanza maandalizi ya rasimu ya azimio la watu wenye ulemavu.
Mwaka jana (2010) Tanzania na Philippines zilishirikiana kuanda azimio kuhusu watu wenye ulemavu. Ni kutokana na azimio hilo, masuala ya watu wenye ulemavu yameeingizwa katika taarifa ya mkutano wa kilele uliofanyika mwaka huo kuhusu utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia ( MDGs).
Akizungumzia juhudi na mikakati ya Tanzania katika kuwasaidia watu wenye ulemavu pamoja na wale wanaoishi katika mazingira magumu. Balozi amesema serikali imeandaa na inatekeleza sera mbalimbali zinazolenga kupunguza makali ya maisha kwa makundi hayo.
Amezitaja sera hizo kuwa ni pamoja na sera ya hifadhi ya jamii, sera ya wazee na mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza umaskini wa mwaka 2010.
Wakati huo huo, Tanzania imesisitiza kwamba kilimo kinabaki kama chanzo muhumu cha ajira na hasa kwa nchi kama Tanzania ambayo watu wengi wanaishi vijijini na kutegemea kilimo.
Na kutokana ukweli huo, Balozi Sefue amesema maendeleo ya vijijini na uzalishaji wa kilimo ni muhimu sana katika kuleta maendeleo ya jamii na kupunguza umaskini pamoja na kuchagiza utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya millennia.
“Maendeleo ya sekta ya kilimo ni muhimu mno kwa Tanzania katika kutoa ajira na kukabiliana na umaskini”. Amesisitiza.
Akasema katika kutilia mkazo kilimo, serikali imeandaa mpango unaojulikana kama kilimo kwanza, ukiwa na lengo la, pamoja na mambo mengine, kukifanya kilimo kiwe cha kisasa , kuboresha uzalishaji, utafutaji wa masoko na kushughulikia kwa kina matatizo yanayokwamisha kilimo.
Aidha akasema kuwa mpango huo unawashirikisha wadau mbalimbali katika ngizi zote za serikali,mashirika ya kiraia,mashirika ya kilimo na sekta binafsi.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269