Walinzi wa amani wa UN wakiwa Darfur ya Kaskazini. |
Na Mwandishi Maalum
New York
Tanzania imeitaka Idara ya Umoja wa Mataifa inayohusika na masuala ya ulinzi wa amani (UNDPKO), kutoendekeza dhana inayotaka kuota mizizi ya kuwa, kuna nchi ambazo jukumu lake ni kutoa walinzi wa amani kwa upande mmoja, na kuna nchi ambazo jukumu lake ni kutoa raslimali fedha na vifaa kwa upande mwingine.
Kauli hiyo imetolewa na Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Ombeni Sefue, wakati wa mkutano wa Kamati Maalum ya 34 ya Opereshani za Ulinzi wa Amani (C34). kamati hiyo ni sehemu ya Kamati ya Nne ya Baraza Kuu la 66 la Umoja wa Mataifa. Mkutano huo ulikuwa ukijadili ajenda namba 54 inayohusu dhana nzima ya ulinzi wa amani.
Kamati ya nne ni kati ya kamati sita za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kamati hiyo inahusika pamoja na mambo mengine, masuala ya siasa na umalizaji ukoloni na operesheni za ulinzi wa amani na vilevile masuala ya Habari.
Balozi Sefue amesema, kuna kila dalili ndani Umoja wa Mataifa, za kutaka kujengeka kwa mazingira ya kubaguana kati ya nchi zile zinazojiita wachangiaji wakubwa wa askari na zile zinazojiita wachangia wakubwa wa raslimali zikwamo fedha.
“Ningependa kusisitiza mambo kadhaa, ambayo ujumbe wangu unaamini ni ya msingi na yanatakiwa kuzingatiwa. Kwanza tunahitaji kupanua wigo wa kuchangia walinzi wa amani. Na tuachane na dhana inayotaka kujengekea ya kwamba kuna nchi ambazo jukumu lao ni kuchangia askari,kwa upande na wengine jukumu lao ni kuchangia raslimali. Hii ni dhana potofu na si sahihi. Jukumu hili adhimu ni wajibu wetu sote”. Akasisitiza Balozi Ombeni Sefue.
Takwimu zinaonyesha kuna walinzi wa amani 120.000 wanaume na wanawake, wanaotekeleza majukumu yao katika misheni mbalimbali. Idadi kubwa ya wanajeshi hao wakiwamo askari polisi wanatoka katika nchi za Afrika , Asia na baadhi ya nchi za Mashariki ya Kati.
Tanzania inashika nafasi ishirini miongoni mwa katika kundi la nchi zinazotambuliwa kama wachangiaji wakubwa. Aidha Naibu Kamanda wa vikosi vya kulinda amani huko Darfur ni Mtanzania, Meja Jenerali Wynejones Kisamba.
Aidha Balozi Ombeni Sefue ameitaka pia Idara hiyo , kutoa tafsiri sahihi kuhusu baadhi ya majukumu wanayopewa walinzi wa amani.
Akatoa mfano kwa kusema, jukumu lijulikanayo kama ya Robust Peacekeeping ni moja ya jukumu jipya ambalo licha ya kwamba utekelezaji wake ni tata lakini hata tafsri yake yaijaeleweka miongoni mwa walinzi wa amani.
Akasema kama hapatolewa tafsiri sahihi ya jukumu hilo na namna ya kulitekeza, inaweza kujenga mazingira ya mkanganyiko na hivyo kuhatarisha mfumo mzima wa utekelezaji wa amri na udhibiti katika eneo la husika. “ kwa kweli hili ni jambo la mwisho kutarajiwa na walinzi wa amani na makanda wao ” akasisitiza Balozi.
Suala lingine ambalo Tanzania imetaka lipewe umuhimu ni usalama wa walinzi wa amani.
Akasema usalama wa walinzi hao ambao wanatekeleza majukumu yako katika mazingira magumu na hatari, unatakiwa kuratibiwa ipasavyo.
“ Lazima tuhakikishe walinzi wetu wa amani kwanza, wanakuwa salama wao wenyewe ,wanapewa vifaa zikiwamo Helkopta. Na kwamba majukumu yako yanatambulika na yameratibiwa vizuri ” akasitiza Sefue.
Taarifa kutoka Idara hiyo ya Operesheni za Ulinzi wa Amani, zinaonyesha kwamba jumla ya walinzi wa amani 86 wamepoteza maisha kwa mwaka huu peke yake na kati hao 29 ni raia.
Kuhusu marejesho ya malipo kwa nchi zinazochangia walinzi wa amani pamoja na vifaa, Balozi Ombeni Sefue amesema, Tanzania inakaribisha wazo la kuundwa kwa Jopo la washauri ambao watalifanyia kazi suala la marejesho ya malipo.
Hata hivyo akasema ni matarajio ya Tanzania kwamba, ushauri wowote utakaotolewa na Jopo hilo utakuwa jumuishi.
Suala jingine ambalo pia lilichangiwa na wazungumzaji wengi. Lilihusu jukumu la kulinda raia wakati wa machafuko (Protection of Civilians).
Akiizungumzia jukumu hilo, Balozi wa Zimbabwe katika Umoja wa Mataifa,Chitsaka Chipaziwa. Amesema kama iliyokuwa kwa jukumu la Robust Peacekeeping. Jukumu ulinzi wa rais pia bado lina utata na utekelezaji wake pia .
“ Hivi tunapozungumzia jukumu la ulinzi wa raia, je ni kweli walinzi wetu wanaelewa vema namna ya utekelezaji wake?. Ni wiki iliyopita tu tulionyeshwa hapa namna gani jukumu hilo linatakiwa kuingizwa katika mitaala ya ufundishaji. Lakini tayari walinzi wetu walishaanza kulitekeleza jukumu hili. Kwa hiyo ni nini kinachoanza, mafunzo kwanza au utekelezaji kwanza mafunzo baadaye”. Akahoji Balozi wa Zimnbabwe.
Akafafanua zaidi kwa kusema pale ambapo jukumu hilo la kulinda raia lisipotekelezwa ipasavyo wanaolaumiwa ni nchi zinazochangia walinzi wake . Ili hali hapakuwa na muda wa kutosha kwa walinzi wetu kujifunza na kulielewa vema jukumu hilo.
mwisho
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269