Breaking News

Your Ad Spot

Nov 2, 2011

AFRIKA YALIA NA MZIGO WA WAKIMBIZI, YATAKA ISAIDIWE

Moja ya kambi za wakimbizi Afrika
Na Mwandishi Maalum
New York
Afrika  imesema  mgogoro wa kifedha na mtikisiko wa uchumi , visiwe visingizio vya kuliachia Bara hilo jukumu la kuwahifadhi, kuwahudumia na kuwalinda wakimbizi wanaokimbia machafuko na njaa katika nchi zao.
Kauli hiyo imetolewa na  Mwakilishi wa  Ubalozi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa , Balozi Ombeni Sefue, wakati alipozungumza kwa niaba ya kundi  la nchi za Afrika katika Umoja wa Mataifa.
Ilikuwa ni katika mkutano uliokuwa ukijadili   Ripoti  kuhusu masuala ya wakimbizi iliyowasilishwa na Kamishna wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala hayo.  Mkutano huo umefanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.
Balozi Sefue amesema,  jukumu la kuwahudumia na kuwahifadhi wakimbizi ni  jukumu ambalo  halipashwi kuachiwa waafrika wenyewe kwa kisingizio cha  hali mbaya ya uchumi, kwa sababu, hata nchi za Afrika zinazobeba  jukumu hilo nazo zimeathirika kwa tatizo hilo  ambalo hawakulisababisha.
Akasema, Afrika ina wasi wasi mkubwa kutokana na  ongezeko kubwa la watu wanaokimbia makazi yao. Ambapo mwaka 2010 likuwa na nyongeza    kubwa ndani ya kipindi cha miaka 15 iliyopita na idadi hiyo imeongezeka katika mwaka 2011.
Balozi Ombeni Sefue akaeleza kwamba, wakati takwimu zilikuwa zikoonyesha kupungua kwa idadiya wakimbizi kati  ya mwaka 2000 hadi 2009.Lakini  hali imebadilika kati ya mwaka 2010 na 2011 ambapo idadi ya wakimbizi imeongezeka  ama  kutoka na  mapigano mapya au yale yanayoendelea.
Aidha akasema ongezeko  hilo, limechangiwa  pia na hali ya  ukame na njaa katika maeneo  mbalimbali ya bara la Afrika.  Na  inakadiriwa  kwamba hivi sasa kuna zaidi ya watu milioni 11.1 ambao wameyakimbia makazi yao Barani Afrika, sawa   asilimia 40 ya watu wote  ambayo wameyakimbia makazi yao duniani.
 “ Huu ni mzigo mkubwa  kiuchumi, kijamii na kiutamaduni ndani ya jamii jumuia  na   kwa nchi zinazowahifahi wakimbizi hao.  Na hasa ikizingaiwa  baadhi ya nchi hizi zinamiundombinu duni ya kiuchumi ya kuweza kuhili kikamili jukumu hilo.” akasisitiza Balozi Sefue.
 Akasema   Viongozi wa Afrika   kupitia mikataba mbalimbali  ya kimataifa pamoja na ile ya Umoja wa Afrika,wameonyesha utashi mkubwa wa kisiasa,  hali na mali  katika kuwahifadhi na kuwasaidia waafrika wenzao ambao   ni wakimbizi  wa aina zote wakiwamo wakimbizi wanaokimbia makazi yao.
Akatoa mfano kwa kuzitaja nchi za  Kenya, Ethiopia na Djibout kama nchi ambazo zimefungua Milango yao kwaajili ya kuwahifadhi wakimbizi  wanaokimbia mateso na njaa nchini Somalia. Na nchi za Misri  na Tusinia ambazo  nazo zimefungua milango yao kwa mamia  ya maelefu ya wananchi wa Libya.
Akasema kwamba kutokana na uwajibikaji huo. “   Nchi za Afrika zinaunga  mkono tamko lililotolewa na Kamishna  anayeshughulika masuala ya  wakimbizi kwamba, nchi za Afrika  zinatapashwa kuungwa  mkono  ili ziwezei  kukidhi  mahitaji  ya wakimbizi ya  haraka na ya muda mrefu”.
Na kuongeza kwamba, pamoja na mafaniko hayo  na kuwajibika huko, nchi za  Afrika zinakabiliwa na changamoto nyingi zikiwamo za kutoa ulinzi wa uhakika kwa wafanyakazi wa  kimataifa wanaotoa misaada ya kibinadamu kwa wakimbizi.
Akatoa mfano wa matukio  ya hivi karibuni  utekaji nyara wa wafanyakazi   waliokuwa wakitoa huduma kwa wakimbizi wa Somali na katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
 
Akasema  ili kuikabili hali hiyo   kuna haja  kwa  Jumuiya ya Kimataifa,   chini ya usimamizi na uongozi wa  Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama la Umoja wa Afrika kushirikiana na   kuongeza juhudi za kuleta hali ya utulivu na usalama  nchini Somalia.
Aidha  mwakilishi huyo wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, akabainisha  kuwa, kutokana  na  kwamba bado kuna migogoro mingi  duniani  na ambayo bado haijapatiwa ufumbuzi wa kudumu ni wazi kwamba changamoto za kuwalinda na  kuwahudumia wakimbizi zitaendelea.
“Ingawa uhifadhi wa wakimbizi ni   moja ya misingi ya kimataifa ya ulinzi, lakini msingi huo hauwezi kuwa suluhisho la tatizo. Tunahitaji kuwa ni mikakati madhubuti yenye kutoa suluhisho la kudumu, ikiwa ni pamoja na urejeshwaji wa hiari wa wakimbizi katika nchi zao”  akasema Balozi.
 Aidha akasema     Afrika  inamsemo wake  unaosema   Nguzo ya Dunia ni Matumaini”. Hakuna mahali popote ambapo binadamu wenzetu wameonyesha matumaini ya nguzo hiyo zaidi ya kwenye makambi ya wakimbizi na  wale  waliokimbia makazi yao katika Afrika” akasema Balozi.
Na kuhitimisha kwa kusema. Kwa pamoja tunaweza  kuunganisha juhudi zetu katika kuyatafutia ufumbuzi  matatizo ya  wakimbizi duniani kote.  katika umoja wetu na  tuwape  basi nguzo  ya matumaini wakimbizi wote pamoja na wale waliokimbizi makazi yao”.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages