Na Mwandishi Maalum
New York
Imeelezwa kwamba, Vyama vya Ushirika, kama vikisimamiwa vizuri, vikaandaliwa sera na sheria stahili , na vikaachwa vifanye kazi zake bila ya kuingiza siasa, ni eneo muhimu sana linaloweza kutoa ajira kwa mamilioni ya vijana ambao wamepoteza matumaini ya kupata ajira.
Aidha imebainishwa kwamba, kwa kupitia Vyama hivyo vya Ushirika ni rahisi kwa wananchi kujiletea maendeleo yao haraka na kuondokana na umaskini.
Kwa kutambua hayo Umoja wa Mataifa, umeutangaza mwaka 2012 kuwa mwaka wa Kimataifa wa Vyama vya Ushirika. Na kuzitaka Serikali za nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa, kuvijengea vyama vya Ushirika mazingira mazuri yatakayoviwezesha kukua, kustawi na kutekeleza majukumu yake kikamilifu .
Hayo yamesemwa na wazungumzaji tofauti akiwamo Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk. Asha-Rose Migiro wakati wa uzinduzi wa mwaka huo, uliofanyika siku ya jumatatu katika Ukumbi Mkuu wa Mikutano wa Umoja wa Mataifa, na kuhudhuriwa pia na watu mashuhuri akiwamo aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Bw. Gordon Brown.
Ujumbe wa mwaka wa Kimataifa wa vyama vya ushirika unasema.“Makampuni ya kibiashara ya Vyama vya Ushirika hujenga ulimwengu bora zaidi”.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliotanguliwa na kongamano lililoyojumisha nchi wanachama wa UM, Shirika la Kazi Duniani ( ILO) na wataalamu mbalimbali. Naibu Katibu MKuu, Dkt.Asha- Rose Migiro amesema “Mwaka wa Kimataifa wa Vyama vya Ushirika ni fursa ya kuongeza uelewa kwa umma kuhusu vyama hivyo, kuhimiza ukuaji wake na kuzihimiza Serikali kuanzisha sera nzuri zitakazo weka mazingira mazuri ya ustawi wa vyama vya ushirika”.
Akasema uzinduzi huo unafanyika katika kipindi ambacho dunia iko katika mtafaruku wa kutengana na kutoridhika kunakotokana na mwendelezo wa mdodoro wa uchumi.
Akaongeza kuwa kupitia Vyama vya Ushirika, dunia inaweza kujifunza namna ya kukabiliana na mdodoro huo kwa kuwa vyama hivyo vimeweza kuhimili matatizo ya uchumi kwa kuwa na mitaji na akiba kubwa.
Aidha akasema Vyama hivyo vimetoa mchango mkubwa si tu kwa wanachama wake lakini pia katika jumuia zao na jamii inayowazunguka.
“ Vyama vya Ushirika vinauwezo mkubwa wa kupunguza umaskini, kukuza na kutoa ajira kwa vijana, wanawake, wazee, watu wenye ulemavu na watu asilia. Ni vyama vinavyotoa mafunzo na kukuza ujuzi wa wanachama wake, Na ni chanzo muhimu cha usalama wa chakula na amani na usalama” akasema Migiro
Akasisitiza kwamba, umuhimu mwingine wa Vyama vya Ushirika unatokana na Mshikamano wake . Kwa maana ya kwamba vyama hivyo ni imara, vinajenga uhusiano miongoni mwa wanachama wake, kuna uwajibikaji kwa wanachama na wateja wake na vinazingatia ustawi wa wanachama wake na ustawi wa jamii nzima.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Bw. Gordon Brown yeye amesema vyama vya Ushirika vinaajiri zaidi ya watu 100 milioni duniani kote,
Aidha Bw. Brown amesema kuwa taarifa mbalimbali zinaonyesha kuwa vyama vikubwa 300 vya Ushirika vilivyoko duniani vilifaya mauzo ya dola za kimarekani 1.1 trilioni katika mwaka 2008. Hali inayoonyesha kwamba vyama hivyo vina nguvu kubwa sana kiuchumi ni kimitaji.
Akasema kama hiyo haitoshi Vyama hivyo vya Ushirika ambavyo vimeenea katika nchi mbalimbali vinahudumia wanachama zaidi ya bilioni Moja. Akasema ni muhimu kwa jumuia ya kimataifa kuutumia mwaka huu wa kimataifa wa vyama vya Ushirika kujifunza zaidi utendaji wake pamoja na kuvisaidia kwani vina nafasi kubwa ya kukabiliana na changamoto mbalimbalili zinazoendelea hivi sasa dunia zikiwamo za ajira kwa vijana.
Kilele cha Mwaka wa Kimataifa wa Vyama vya Ushirika kitakuwa Desemba 31,2012.
Washiriki wa Kongamano lililotangulia uzinduzi wa Mwaka wa 2012 kuwa Mwaka wa Kimataifa wa Vyama vya Ushirika. Baadhi ya wazungumzaji katika kongamamo hilo walizitaka serikali kutoingiza siasa katika utendaji kazi wa vyama vya Ushirika. wakainisha pia mafanikio mbalimbali yaliyotokana na vyama hivyo pamoja na changamoto zinazovikabili vyama hivyo. Umoja wa Mataifa umeutaganza mwaka 2012 kuwa mwaka wa Vyama vya Ushirika kwa kutambua mchango wake katika utoaji wa ajira, kukuza uchumi na kuleta maendeleo endelevu, kupiga vita umaskini, kuchangia utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya millenia pamoja na hifadhi salama ya chakula.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269