Breaking News

Your Ad Spot

Nov 14, 2011

KCB WAIPA SHULE MSAADA WA VIFAA YA MAMILIONI YA FEDHA MWANZA

Wanafunzi wa shule ya Msingi Mkundi Mwanza wakikalia
madawati ya msaada wa KCB baada ya makabidhiano.
Na Mwandishi Wetu, Mwanza.
Benki ya KCB Tanzania imetoa msaaada wa madawati 120, meza na viti vya walimu 20 vyenye thamani ya Shilingi Milioni 10 katika shule ya msingi Mkudi iliyopo jijini Mwanza.

Msaada huo umefuatia upungufu mkubwa wa vifaa mbalimbali unaoikabili shule hiyo yenye wanafunzi 1,729 na vyumba kumi vya madarasa hivyo kuchangia  mrundikano wa wanafunzi wanaofundishiwa kwenye darasa moja kuanzia 150 hadi 200.

Akikabidhi vifaa hivyo Mkuu wa Masoko na Mahusiano wa KCB Tanzania Bi Christine Manyenye amesema, kwa kutambua umuhimu wa elimu nchini Benki yake imetoa msaada huo wa Shilingi Milioni 10/- ili kuwawezesha wanafunzi wa shule ya Mkudi kupata elimu bora.

“Katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba mwaka huu tumepanga kutumia kiasi cha shilingi Milioni 190/- katika  kuadhimisha wiki ya jamii kwenye maeneo ambapo benki yetu inatoa huduma. Kwa jijini Mwanza ingawa kiasi hiki si kikubwa sana ila ni matarajio yangu kimepunguza uhitaji  wa madawati kutoka 458 hadi 160.

Awali Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Celina Bachubila alisema licha ya kupokea msaada huo wenye thamani ya Milioni 10/- kutoka KCB Tanzania, bado shule yake inakabiliwa na upungufu wa vifaa mbalimbali ikiwemo madawati 160, Viti  21, Makabati 10, vyumba vya madarasa 22 na vitabu 7,018.

Vilevile Mwalimu Bachubila amebainisha kwamba kutokana na upungufu huo, wanafunzi wanakumbana na changamoto hiyo kitaaluma inayofanya  mazingira ya kujifunzia kuwa magumu.

“Upungufu wa vyumba vya madarasa 21 madhara yake ni kuwepo kwa mrundikano wa wanafunzi darasani kuanzia 150 hadi 200 kwenye darasa moja lenye uwezo wa kubeba wanafunzi 45 tu,” alisema Mwalimu Bachubila.

Kwa upande wake Bw Allanus Lwena ambaye ni mjumbe wa Kamati ya shule ya Mkudi  ameishukuru KCB Tanzania na kusema ni matarajio yake msaada huo wa vifaa utaboresha kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa darasa la saba kutoka idadi ya watoto 122 mwaka jana hadi kufikia 196 mwaka 2011.

“Tunaomba washirika wengine wa maendeleo zikiwemo taasisi zingine kuunga mkono jitihata za KCB Tanzania katika kuhakikisha wanarudisha kiasi cha faida katika kusaidia jamii zinazoizunguka.

Hivi karibuni benki hiyo ilitoa vifaa mbalimbali kwa nyumba ya kulelea watoto yatima ya Don Bosco iliyopo Kimara Suka jijini Dar es Saalam wenye thamani ya shilingi milioni 4.5/-

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages