Breaking News

Your Ad Spot

Nov 13, 2011

NAPE AWAHUSISHA CHADEMA NA VURUGU ZA MACHINGA MBEYA

 Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Nape Nnauye amesema tafsiri rahisi ya fujo na vurugu zinazofanywa na Chadema nchini kwa sasa ni hasira walizonazo baada ya kunyimwa kura katika chaguzi mbalimbali nchini na hivyo kuamua kuwaadhibu Watanzania kwa kuwanyima fursa za kufanya kazi na kuishi kwa amani na utulivu.

Bwana Nnauye aliyasema hayo alipokuwa akiongea na wana CCM na wananchi kwenye uzinduzi wa shina la CCM lililopo katka barabara ya pamba eneo la posta mpya katikati ya jiji la Dar es salaam.
Nape alisema haelewi kwanini Chadema hawataki kukubali kuwa wananchi waliwakataa kwenye uchaguzi mkuu uliopita na hata majimbo machache waliyochukua ni kwa sababu ya makosa ya ndani ya CCM yenyewe. Alisema hata uchaguzi mdogo wa Igunga umethibitisha hili na kwamba matokeo ya chaguzi ndogo za madiwani pia ni ushahidi tosha.

" Nashangazwa sana na kinachofanywa na watani zetu Chadema. Watanzania waliwakataa kwenye chaguzi nyingi tu nchini kwa kuwanyima kura, sasa hii hasira ya kukataliwa ndo wanaanzisha vurugu kila kona ya nchi ili kuwanyima watanzania muda wa kufanya shughuli zao za maendeleo, hili halikubaliki hata kidogo" alisema Nape.
 
Alitoa mifano ya vurugu za Arusha, Mbeya, Igunga na maeneo mengine na kusisitiza kua licha ya kuvuruga amani na utulivu, inavuruga pia ratiba za watu kuzalisha hivyo kupunguza kipato chao.

" hatuungi mkono matumizi ya nguvu kwenye kushughulikia swala la machinga nchini kwani linarudisha nyuma juhudi zao za kujikwamua, ila pale Chadema wanapojificha nyuma ya pazia na kufanya fujo kwa kisingizio cha machinga hili halikubaliki" alisema Nape

Alisema kwa tukio kama la Mbeya si kweli kwamba waliokuwa wakichoma bendera za CCM na ofisi za CCM ni machinga bali anaamini ni Chadema waliojificha kwenye joho la Machinga, hivyo akatoa wito kwa vijana nchini kutokubali kutumiwa kama ngao.
" pale Mbeya jana kumetokea vurugu kubwa, kuna madai kuwa ni machinga na polisi, lakini hivi jamani machinga ndo wachome bendera na ofisi za CCM? Tunayetaka kumdanganya nani? Tunajuwa liko tatizo la machinga nchini, nasi kama chama tawala hatuungi mkono matumizi ya nguvu kwenye kushughulikia swala lao, lakini Chadema wasijifiche nyuma ya hili na kuhujumu mali za chama chetu" alisema Nape

Akamgeukia Mkurugenzi wa kitengo cha usalama cha Chadema Ndg. Rwakatare na kudai kuwa anaamini yeye ndiye anayeandaa machafuko haya kwani amekuwa mzoefu alikuwa akiyaandaa toka akiwa CUF.
" kuna huyu kakaangu Rwakatare alipokuwa CUF kulikuwa na fujofujo karibu kama hizi tuzionazo leo, amehamia Chadema tunaanza kuona fujo hizohizo, kwanini tusiamini yeye ndiye mpangaji? na hasa ukizingatia ndiye Mkurugenzi wa kitengo cha Usalama wa chama chao" alihoji Nape.

Alienda mbali kwa kudai kuwa kwa matendo hayo kwanini chadema kisiitwe chama chenye malengo ya kuvuruga amani kwani kina tenda matendo yasiyofanana na chama cha siasa.
" kwa matendo haya ndugu zangu, hivi bado tunasababu za kuamini kuwa Chadema ni chama cha siasa? Hivi kwanini tusiamini kuwa Chadema ni chama cha kigaidi? Haya matendo hayafanani na chama cha kigaidi? Maana magaidi ndo hufanya matendo haya kwa faida zao binafsi, sasa hawa wanafanya kwa faida ya nini?" aliuliza Nape.

Alidai anazo taarifa kuwa zilikuwepo na bado zipo juhudi kubwa za kulipua ofisi za CCM mahali kwingi na kuwa wanazifanyia kazi taarifa hizo lakini wanaamini watazidhibiti.

Akasema yapo matukio mawili matatu ya majaribio ya kutaka kuhujumu ofisi na mali za CCM hicho ambayo wameyadhibiti lakini akawatahadharisha wanaCCM nchini kote kuwa makini na njama hizo na kuchukua tahadhari ya kulinda mali zao.
" tunazo taarifa kadhaa za majaribio na mipango ya kuhujumu mali zetu zinazofanywa na wenzetu, baada ya kuwashitukia kwenye matukio kadhaa sasa wanajipanga kuhujumu hata ofisi na mali za umma. Hili hatutakubali na vyombo vya dola visifumbie macho swala hili" alisisitiza Nape.

Alipongeza uamuzi wa kufungua shina hili la CCM lakini akawataka kuhakikisha wanafuata sheria na utaratibu wa jiji kufanya biashara kwenye maeneo halali kwa mujibu wa sheria na taratibu.

Pia alitoa wito kupitia kwao  kwa mashina ya namna hiyo kote nchini, kwamba pamoja na shughuli za kisiasa wafanye pia shughuli za uzalishaji mali, ili maeneo hayo ya mashina yawe ni maeneo ya uzalishaji mali badala ya kugeuka kuwa vijiwe vya majungu.
" lazima sasa tuangalie upya mashina yetu ya wakereketwa wa CCM yaache kuwa vijiwe vya majungu badala yake pamoja na kufanya siasa viwe pia ni vituo vya uzalishaji ili kujikwamua kiuchumi kwa chama na mtu mmoja mmoja." aliasa Nape

Aliwataka waungane na kuanzisha umoja utakaowasaidia kupata mitaji kutoka kwenye taasisi za kifedha nchini ili wajikwamue na umasikini.

Akatoa wito kwa vijana wote nchini kuungana katika vita dhidi ya rushwa na kwamba ni vita ya vijana zaidi kwani wao ndio waathirika wakubwa kwani wanaishi leo na kesho.
" iko vita kubwa ya rushwa ambayo vijana lazima tuungane na kuacha tofauti zetu na kuahakikisha tunashinda ili kuhakikisha rasilimaliza nchi zinanufaisha wote"


No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages