Breaking News

Your Ad Spot

Nov 5, 2011

LUDOVICK UTOUH APITISHWA KUWA MJUMBE WA BODI YA WAKAGUZI YA HESABU ZA UMOJA WA MATAIFA

Na Mwandishi Maalum New York
Bw. Utouh
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali  kutoka  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bw. Ludovick   Utouh amependekezwa na kupitishwa kwa kauli Moja kuwa Mjumbe wa Bodi ya wakaguzi wa Hesabu za Umoja wa Mataifa.

Bw.  Utouh  amepitishwa na  wajumbe wa Kamati ya Tano  ya Utawala na Fedha ya Baraza Kuu la 66 la Umoja wa Mataifa, katika kikao chake kilichofanyika siku ya Ijumaa,  hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, Jijini New York, Marekani. Utouh  atakuwa mjumbe wa Bodi hiyo kwa kipindi cha miaka sita kuanzia Julai Mosi 2012 akichukua nafasi  itakayoachwa wazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu kutoka Afrika ya Kusini anayemaliza muda wake mwezi Juni mwakani.

Tanzania inakuwa nchi ya  tatu kutoka Afrika  kuingia katika Bodi hiyo tangu  ilipoanzishwa. Nchi nyingine kutoka Afrika  ambazo zimewahi kuwa wajumbe wa  bodi  ni  Ghana na Afrika ya Kusini.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Seriakali atafanya kazi na wajumbe wengine wawili  ambao pia ni wadhibiti na wakaguzi wa hesabu  kutoka Serikali za China na Uingereza,  baadhi ya majukumu ya Bodi ya  wakaguzi wa hesabu za Umoja wa Mataifa, ni pamoja na kukagua Vitabu vya hesabu za Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, Mashirika na asasi zote zilizochini   ya Umoja wa Mataifa , Misheni za ulinzi wa Amani za Umoja wa Mataifa, miradi mbalimbali inayosimamiwa na Umoja wa Mataifa,  hesabu za   Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai  zikiwamo za  mauaji ya kimbari ( Rwanda na Yugoslavia)

Bodi hiyo hukutana mara mbili kwa mwaka katika miezi ya Juni na  Novemba. Pamoja na kwamba wajumbe wa bodi hiyo hutakiwa kukutana  mara mbili kwa mwaka, lakini wanaweza kukutana wakati wowote  pale wanapohitajika.

Kwa mujibu wa taratibu za kazi, wajumbe hao watatu wa bodi ya wakaguzi wa hesabu za  Umoja wa Mataifa ( Tanzania, China na Uingereza) watasaidiwa na wakurugenzi watatu kutoka katika  nchi hizo.

Wakurugenzi hao ambao watatakiwa kuwapo   muda wote , Ofisi zao za kudumu kwa kipindi hicho cha miaka sita zitakuwa katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages