Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Asha-Rose Migiro amewahimiza wabunge kuweka mbele maslahi ya wananchi wanaowawakilisha.
Ameyasema hayo jana Jumatatu, wakati alipokuwa akifungua mkutano wa siku mbili unaowakutanisha wabunge kutoka mabunge mbalimbali duniani, ufunguzi uliomshirikisha pia Rais wa Baraza Kuu la 66 la Umoja wa Mataifa, Nassir Abdulaziz Al-Nasser.
Katika mkutano huo ambao umeandaliwa na Umoja wa Mataifa na Muungano wa Mabunge ( IPU),Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linawakilishwa na wabunge wawili, Mhe. John M. Cheyo na Mhe. Betty Machangu.
“ Mkiwa ni wabunge kazi yenu si kupitisha sheria tu na kusimamia utendaji wa serikali. Bali mnatakiwa kuwajibika kisiasa kwa kuwasikiliza wananchi na kuelezea matakwa yao”, Akasisitiza Migiro.
Naibu Katibu Mkuu amewaambia wabunge hao, wakiwamo pia baadhi ya maspika , kwamba, uwajibikaji wa kisiasa na utawala wa kidemokrasia haviwezi kutengenishwa kwa kuwa vyote ni muhimu katika kuchagiza maendeleo ya binadamu, haki na amani.
“ uwajibikaji wa kisiasa ni muhimu sana katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili dunia hivi sasa. Baadhi ya Changamato hizo ni pamoja na umaskini, vurugu, na uhalifu wa kupangwa mambo ambayo yanashamiri katika nchi ambazo hakuna uwajibikaji” akabainisha Migiro.
Akasema kuwa taarifa ya Bank ya Dunia imeonesha kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe, makosa ya jinai, vurugu na hata ugaidi na uhalifu wa kupangwa ni mambo yanayoota mizizi na kukua katika nchi ambazo ama utawala wa sheria ni dhaifu au taasisi zake zimeghubikwa na ufisadi.
Hata hivyo Migiro amewaeleza wabunge hao kwamba hakuhitajiki utafiti kama huo ulioofanywa na Bank ya Dunia,kufahamu kwamba kuongezeka kwa vitendo vya halifu kunasababishwa na serikali kandamizi.
Akatoa mfano kwa kutaja vunguvungu la kisiasa linaloendelea hivi sasa Mashariki ya Kati maarufu kama Arab Spring, ambako anasema vuguvugu hilo limeamsha hamasa hususani kwa vijana, hamasa ya kutaka kuwepo na serikali za kidemokrasia, zinazowajibika na zenye kuheshimu misingi ya haki za binadamu.
Akasema anafahamu vema changamoto wanazokabiliana nazo wabunge kwa sababu hata yeye aliwahi kuwa mbunge.
Hata hivyo akasema yapo mambo kadhaa ambayo wabunge kwa kushirikiana na serikali zao yanaweza saidia kuzuia au kupunguza mitafaruku ya kisiasa na vitendo vya uhalifu.
Ameyataja mambo hayo kuwa ni pamoja na kujenga mazoea ya uwajibikaji, kufanya uchanguzi wa mara kwa mara na unaozingatia utawala wa sheria, uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kukusanyika na kutoa mawazo na kuongeza idadi ya wanawake mabungeni.
“ Lakini uwajibikaji unakwenda mbali zaidi ya hapo” anasema Migiro. “ Ni kwa kuhakikisha ushiriki wa wananchi na hasa vijana katika mambo ya siku hadi siku, kwa kutimiza hayo na mambo mengine wabunge mnaweza kujenga daraja imara kati ya wananchi na serikali zao” akasisitiza Migiro.
Aidha Migiro ameyataka mabunge yote duniani yawajibike katika kuzuia vitendo vya rushwa.
Ajenda muhimu zinazojadiliwa na wabunge hao katika mkutano huo wa siku mbili ni pamoja na, uhusiano kati ya Umoja wa Mataifa na Mabunge , nafasi ya Umoja wa Mataifa katika kusimamia na kuimarisha dhana ya uwajibikaji, na fursa na changamoto zinazowakabili vijana katika ushiriki wao katika demokrasia.
Nyingine ni uwajibikaji katika usimamizi wa fedha za umma na uimarishaji wa uhusiano kati ya taasisi za kitaifa na asasi zisizo za kuserikali ili kujenga jamii yenye uwazi.
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Asha-Rose Migiro akifungua siku ya jumatatu mkutano wa siku mbili wa wabunge kutoka mabunge mbalimbali duniani mkutano huo unafanyika makao makuu ya Umoja wa Mataifa New York, kushoto kwake ni Rais wa Baraza Kuu la 66 la Umoja wa Mataifa, Bw. Nassir Abdulazizi Al-Nasser na kulia ni Katibu Mkuu wa IPU Bw. Anders B. Johson.
Naibu Katibu Mkuu Asha-Rose Migiro akibadilishana mawazo na Waheshimiwa Wabunge John M. Cheyo na Betty Machunge wakati alipowakaribisha Ofisini kwake Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.Wabunge hao wapo hapa wakihudhuria mkutano wa wabunge ambao Naibu Katibu Mkuu aliufungua. Wabunge hao wanaliwakilisha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mkutano huo .
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269