Na Mwandishi Maalum, New York
Maandamano yasiyokuwa na ukomo na yasiyozingatia utawala wa sheria, vurugu na fujo zinazofanywa na vijana kwa kisingizo cha kutaka fursa sawa na uwajibikaji, hayawezi kujenga mazingira ya uzalishaji wa ajira.
Kauli hiyo imetolewa na Mhe. John M. Cheyo mbunge wa Bariadi Mashariki na mwenyekiti wa UDP, wakati alipokuwa akichangia majadiliano kuhusu fursa na changamoto za ushiriki wa vijana katika demokrasia.
Mhe. Cheyo ni kati ya wabunge wawili wanaouhudhuria mkutano wa siku mbili unaoshirikisha wabunge kutoka mabunge mbalimbali duniani, mkutano huo unafanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, ukiwa umeandaliwa na UN kwa kushirikiana na Chama cha Mabunge ( IPU). Mbunge mwingine kutoka Tanzania anayeshiriki mkutano huo ni Mhe. Betty Machunge
Akafafanua zaidi kwa kusema ingawa vijana wanadai uwajibikaji zaidi kutoka serikali zao pamoja na fursa za ajira, lakini ajira na fursa hizo haziwezi kupatikana katika mazingira ambayo yametawaliwa na vurugu na maandamano yasiyokuwa na kikomo.
“ Ni kweli wanayo haki ya kudai fursa sawa za kushiriki katika demokrasia na kupata ajira, lakini pia wanatakiwa kukumbuka kwamba wanaowajibu pia wa kufuata utawala wa sheria na taratibu zilizopo katika kuwasilisha madai yao, kinyume na hapo wanachokifanya si demokrasia” akasititiza Cheyo.
Akizungumzia ushiriki wa vijana katika siasa, Bw. Cheyo amesema bila ya kubadili mifumo ya uchaguzi ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati ya makusudi itakayoongeza idadi ya vijana mabungeni. Vijana wengi hususani Barani Afrika watabaki kuwa wasindikizaji badala ya kuwa washiriki .
Akasema kuwa vurugu nyingi na maandamano yasiyokwisha na yanayoendelea sehemu mbalimbali duniani na yakiwahusisha zaidi vijana, yanatokana na sababu nyingi lakini kubwa ni kunyimwa kwao fursa za kushiriki siasa.
“ Vijana wengi hivi sasa wamekata tamaa na wamechoka kuendelea kuwa vipandio vya watu wengine kujipatia nafasi za uongozi wa kisiasa. Kama kweli tunataka na wao washiriki kikamilifu katika siasa basi tunatakiwa kubadili mifumo yetu ya uchanguzi na hasa zile chaguzi ambazo zinatanguliza mbele fedha” akasisitiza Bw. Cheyo.
Akaongeza kuwa kila nchi inatakiwa kuweka mikakati ya makusudi itakayohakikisha kunakuwapo na ongezeko la wabunge vijana katika mabunge yao.
“ sisi katika Tanzania tumeweza kuongeza idadi ya wanawake bungeni maradufu kwa sababu tulijiweka malengo na mikakati ya kuhakikisha kwamba idadi ya wanawake inaongezeka. Kwa utaratibu huu ambao Tanzania imeutumia tunaweza pia kuutumia kwa vijana”. Akasema Cheyo.
Akizungumzia suala zima la vijana na changamoto zinazowakabili. Mhe. Cheyo ametahadharisha kwamba, vijana wasipopatiwa matumaini ni sawa na silaha ya maangamizi inayosubiri kulipuka.
Akasema wanachokifanya vijana hivi sasa katika maeneo mbalimbali duniani kama hakitaangaliwa katika umakini wake. Kuna hatari kubwa ya kujirudia kwa tabia ya kuwaondoa viongozi walioko madarakani kwa njia zisizo halali. Pamoja kurejea kwa matukio kama vile mapinduzi ya kijeshi yaliyotawala sana katika miaka ya 70 na 80.
Wachangiaji wengine waliochangia ajenda hiyo, walisema kwamba pengine vijana si wakulaumiwa sana bali wakulaumiwa ni wale wanaowatumia vijana kwa manufaa na malengo yao.
Aidha baadhi ya wachangiaji, walitaka kuwepo na tafsiri sahihi ya nani ni kijana. Kutokana na kile kilichoelezwa kwamba kumekuwa na tafrisi zinazochanganya ni umri gani unaoweza kutajwa kwamba ni umri halali wa kijana kushiriki siasa na hata uchaguzi.
“ tumezungumza sana kuhusu haki na fursa za vijana, wote tunakubaliana kwamba vijana wanahasira na wanataka mgawanyo sawa wa raslimali. Lakini hebu tuanzie humu humu katika ukumbi tuliomo, je kati yetu ni nani mbunge kijana? Hakuna. Nadhani tuna mengi ya kufanya”. Akasema mbunge mmoja kutoka Bunge la Uingereza na kuwafanya washiriki wengine kuangua kicheko.
Ajenda hiyo ambayo ilikuwa kivutio kwa wachangiaji wengi lakini pia kila mmoja akitoa maoni tofauti, na hisia tofauti katika matumizi ya vyombo vya habari vya kijamii kama vile face book na tweeter kama eneo mbadala la mawasiliano kwa vijana.
Lakini kauli za wazungumzaji wengi ilijidhirisha wazi kwamba kila aliyeichangia hakusita kusema vijana wengi si katika nchi zinazoendelea bali hata zile zilizoendelea wamechoka, wamekata tamaa na hawana matumaini ya maisha yao ya baadaye.
Naye Mhe. Betty Machunge akichangia majadiliano kuhusu dhana ya uwajibikaji, uhusiano kati ya UM na Mabunge na ushiriki wa wanawake katika siasa na demokrasia kwa ujumla. Yeye alitaka kuimarishwa na kuwepo kwa ushirikiano wa karibu kati ya Umoja wa Mataifa na Mabunge.
Akasema kuwa maamuzi mengi yanayofanywa na Umoja wa Mataifa hayawafiki wabunge na kama yanawafikia basi yanachelewa mno.
Akapendekeza kuwapo na mfumo au utaratibu utakao wawezesha wabunge kupitia mabunge yao kutoa taarifa za utekelezaji wa maazimio mbalimbali ya Umoja wa Mataifa hasa yale ambayo yanatakiwa kufanyiwa kazi na wabunge.
Aisha akasema kuwa kama ushirikiano kati ya UM na wabunge utaratibiwa vizuri, utasaidia pia katika kubadilishana mawazo na mbinu mbadala za kuongeza idadi ya wanawake wabunge.
Aisha akasema kuwa kama ushirikiano kati ya UM na wabunge utaratibiwa vizuri, utasaidia pia katika kubadilishana mawazo na mbinu mbadala za kuongeza idadi ya wanawake wabunge.
John Cheyo akibadilishana mawazo na Bw. Oscar Fernandez-Taranco aliyewahi kuwa Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP) nchini Tanzania. muda mfupi kabla ya ufunguzi wa mkutano wa siku mbili wa wabunge kutoka mabunge mbalimbali. Bw. Taranco ambaye kwa sasa ni Msadizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, akisimamia Idara ya masuala ya Siasa alikuwa miongoni mwa watoa mada.Mhe. Cheyo anahudhuria mkutano huo akiliwakilisha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269