Breaking News

Your Ad Spot

Nov 3, 2011

NAPE AMALIZA MGOGORO CCM HOUSTON

Nape
* Ageuka kivutio mkutanoni
* Wampa jina Simba wa Vita Mtoto
* Wakubaliana kufungua tawi  kila Jimbo
* Wasema kwa mwendo huu CCM jabali
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Itikadi na Uenezi bwana Nape Nnauye amemaliza mgogoro wa CCM Houston uliodumu kwa muda mrefu sasa kwa kuwataka wanaCCM waaishio Marekani kufungua matawi kila jimbo wanapoweza ili kukisogeza Chama karibu na watu.
"Uamuzi wa kukisogeza Chama kwa wanachama zaidi ni maagizo ya Halmashauri kuu ya Taifa ya CCM. Hamuwezi kuwa na tawi moja Marekani nzima na mkadhani litafanya kazi vizuri kwa ufanisi, kila jimbo idadi ya wanachama ikitosheleza fungueni mashina kisha tawi" alieleza Nape.
Akihitimisha ziara yake kwa jimbo la Texas jijini Houston juzi, Nape alikutana na Jumuiya ya Watanzania waashio Houston na kutangaza uamuzi huo ambao ulipokelewa kwa furaha na Wana CCM na Watanzania waishio hapo.
" hakika CCM imepata katibu mwenezi, mgogoro huu ulidumu kwa muda na kukiathiri sana chama hapa Marekani lakini kuja kwa huyu bwana kumekata kabisa mzizi wa fitina, sasa CCM itaimarika zaidi Marekani" Alisema bwana Kittoga Mtanzania aishie Houston.
Nape akiwaeleza watanzania waliokusanyika  kumsikiliza, akisema kulikuwa na matatizo kidogo ya tafsiri ya katiba ya CCM na maamuzi ya Chama jambo ambalo sasa amelimaliza na anamatumaini kuwa CCM Marekani itakuwa imara na chachu nzuri ya mabadiliko ndani ya Chama na nchini Tanzania kwa ujumla.
"kimsingi tofauti zilizokuwepo zimekwisha, hazikuwa kubwa ila ilikuwa ni tofauti za tafisiri tu katika utekelezaji wa katiba na majukumu ya kila siku ya Chama hapa Houston. Tumeyamaliza na sasa kazi ni moja, tawi hili liwe chachu ya mabadiliko ndani ya chama na nchi na liwe chanzo cha Umoja na mshikamano kwa Watanzania waishio Jimbo la Texas." alisema Nape.
Alipofika jijini Houston, Nape ambaye ameambatana na Katibu Msaidizi mkuu Itikadi na Uenezi Ndg. Sixtus Mapunda alifanya kikao na viongozi wa CCM Houston na kujadili mgogoro uliotokea na jinsi ya kuutatua. Kikao hicho kifanyika mpaka usiku wa manane wa tarehe 28/10/2011.
Kesho yake jioni Ndg. Nape na ujumbe wake walikutana na jumuiya ya Watanzania waishio Houston ambapo alitumia muda mwingi kujibu maswali mbalimbali kutoka kwa Watanzania hao na kuelezea mambo mbalimbali yanayoendelea nyumbani Tanzania.
Katika hali isiyotarajiwa vijana wawili wa Kitanzania waliojitambulisha kama wanachama wa Chadema walifika eneo la mkutano na mabango yaliyokuwa na kauli mbalimbali za kuikejeli CCM, lakini Nape alikwenda na kupokea mabango hayo na kuwashukuru vijana hao kwa kutumia uhuru wao wa kujieleza kueleza wanachokiwaza juu ya CCM.
" siasa sio ugomvi, hawa rafiki zangu wametumia uhuru wao wa kujieleza na kuandika mabango haya, japo ni kijiko kimoja cha sukari baharini, si sawa na kutokuwepo kabisa, mmefanya mkutano uwe mzuri, sasa kaeni msikilize sera badala ya kuimba ngojera za kwenye mabango" aliwaambia Nape.

Kauli iliyopokelewa kwa makofi na vifijo na kelele za ccm, ccm,ccm. Kisha Nape akapiga nao picha wakiwa na mabango yao nakuwa hakikishia kuwa ujumbewao umefika.

Baada ya masaa mawili na nusu ya maswali na majibu, Nape aligeuka kuwa kivutio kikubwa pale alipoonyesha uwezo mkubwa wa kuelezea mambo yanavyoendelea nyumbani, mafanikio na changamoto zake, kiasi cha kupelekea mashabiki wa Chadema ukumbini kulipuka kwa furaha wakimwita Nape Simba wa Vita mtoto.

" hakika bwana mdogo kiboko! Kwanza umeonyesha uvumilivu mkubwa wa kisiasa kwa kipokea mabango yetu. Lakini jinsi ulivyojibu maswali hata yaliyokuwa yanakera sana, wewe ni simba wa vita mtoto baada ya Mzee Kawawa. Sasa CCM mmeamka! Ntachukua kadi ya CCM!" alisema kada mmoja wa Chadema.

Baada ya kikao hicho karibu Watanzania wote waliokuwepo ukumbini ambao hawakuwa wanachama wa CCM walikwenda kuomba kupewa kadi za CCM kwa madai kuwa kwa mwendo huo CCM sasa imepata mwelekeo mpya wenye matumaini.

" tulishapoteza matumaini sana na Chama hichi hasa sisi vijana, lakini kwa mwendo huu sasa matumaini yapo. Alikuja Zito hapa alipata watu kama kumi na moja hivi, kaja huyu Nape watu hapa ni zaidi ya sitini na wote wameondoka wameridhika hili si jambo la kawaida Houston" alisema Liliani Mtanzania aishie Dallas. 

Akijibu swala la Bwana Fue juu ya hoja kuwa kuna wanasiasa wanatafutwa kuuawa kwasababu ya misimamo yao juu vita dhidi ya ufisadi naye Nape akitajwa, Nape alisema.

"siamini kabisa kama naweza kufa kwa mapenzi ya binadamu. Mkisikia nimekufa mjue ni mapenzi ya Mungu kwani Mungu ninaye mwamini yuko juu ya yote, hata wanaowaza mabaya juu yangu"
" hata hivyo kuwaza mabaya juu ya vita hii ya matumizi mazuri ya rasilimali za nchi, hawamuwazii mabaya Nape ila watanzania wote na wapenda nchi yetu wote, hivyo kwa hakika hawatashinda, kwani sauti ya wengi ni sauti ya Mungu." alisisitiza Nape

Kwenye muafaka,  Nape kawaelekeza wana CCM wa Texas kuacha mifarakano na kuwataka kufanya mchakato wa kufungua mashina manne ya CCM Texas na kisha ameahidi kuja mwenyewe kwenye ufunguzi wa Tawi la CCM Texas na majimbo mengine kama watakavyojipanga.
Aidha alimalizia kwa kuwataka Wana CCM kutumia matawi yao ya Chama kuwaunganisha Watanzania badala a kugeuka vijiwe vya majungu na kubaguana kwa vigezo vyovyote vile, huku akiwataka kuweka Utanzania wao kwanza kuliko itikadi na tofauti zao malimbali.

Nape anaendelea na ziara yake nchini Marekani yenye lengo la kukagua uhai wa chama, ambapo atatembelea Columbus-Ohio, New York na atamalizia Washington Dc, kabla ya kurejea nchini Tanzania wiki ya kwanza ya mwezi Novemba.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages