Breaking News

Your Ad Spot

Nov 3, 2011

TANZANIA YASISITIZA KUKATAA USHOGA

TANZANIA imesisitiza msimamo wake wa kukataa sharti la kuridhia wananchi wake kushiriki ushoga kutekeleza sharti la lililotajwa na  Uingeereza kuwa nchi zinazotaka misaada yake ziruhusuvitendo  hivyo vya ushoga na  ndoa za jinsia moja.                                                                 Akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe , alitoa msimamo huo akisema huko ni kwenda kinyume na sheria na utamaduni wa Tanzania inayotambua ndoa ya mume na mke kama kiini cha familia.                                                                                    Membe katika mkutano wa Jumuia ya Madola uliofanyika wiki iliyopita Perth, Australia, Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron alitamka kuwa nchi hiyo ina mpango wa kusitisha misaada kwa nchi ambazo katiba na sheria zake hazitambui mashoga na ndoa zao.

"Nchi yetu inaheshimu sheria na utamaduni wake, hivyo hatupo tayari kuabudu na kuendekeza nchi nyingine kutuwekea masharti kama hayo ya kuwa na uhusiano wa jinsi moja, eti kwa kutegemea msaada, hili ni tamko hatarishi linaloweza kuvunja uhusiano na nje", alisema Membe.


Aidha Waziri Membe aliwaambia waandishi wa habari kuwa tamko hilo ni msimamo wa chama cha Conservative na kibaya zaidi linatoka Uingereza ambako ndio wenye Jumuia ya Madola hivyo linaweza kusababisha kuvunjika kwake na Cameroun na nchi hiyo ndio watawajibika jumuia hiyo ikivunjika.

Alisema miongoni mwa nchi 54 za Jumuia ya Madola kati yake nchi 13 ushoga ni sehemu ya katiba yao wakati 41 hazina utamaduni huo hivyo msimamo wa Tanzania ni kuwa na ndoa za jinsi mbili tofauti, kinyume na hapo unafungwa kifungo miaka 30. Alisema kuendelea kukumbatia ushoga si jambo zuri na si la kulishabikia hata kidogo vinginevyo wanaweza kujuta nchi ikijihusisha na ushoga na kuukubali kupata misaada ya maendeleo.


"Tanzania hatuwezi kuyumbishwa kwa masharti ya kipuuzi bora tuitunze nchi yetu. Tanzania ni nchi maskini lakini kamwe haturuhusu kuingiliwa na nchi nyingine. Kama ndio hivyo basi wakae na hela zao," alisema Waziri Membe wizarani kwake.


Alisema katika mkutano wa Madola, walijadili mabadiliko ya hali ya hewa ambapo walibainisha nchi zinazotegemea mvua zichukue hatua gani kuishi bila kuathiri hali hali ya hewa. 

Pia alisema walijadili kuhusu hatua za kuchukua ili kuvisaidia visiwa vidogo kama Maldives vinavyoliwa na maji ya bahari yanayojaa kufuatia mabadiliko ya hali ya hewa. Alisema watakuwa na mkutano London Aprili mwakani kujadili mikakati hiyo.
Rais Jakaya Kikwete akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa  Julius Nyerere, Dar es Salaam, alipowasili nchini jana, akitokea Perth Australia kwenye mkutano wa Jumuia ya Madola. Kulia ni Makamu wa Rais Dk. Muhammed Gharib Bilal, Waziri Mkuu Mizengo Pinda (Wapili Kushoto) na Kushoto ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe. (Picha:  Ikulu)

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages