Balozi Sefue kaimpongeza Kihongosi |
Na Mwandishi Maalum
New York
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon amewataka vijana wa kiume kushiriki kikamilifu katika kupinga na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake.
Ban Ki Moon ametoa wito huo wakati wa maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya kukomesha ukatili dhidi ya wanawake, maadhimisho ambayo hufanyika kila Novemba 23.
Katika maadhimisho hayo yaliyofanyika siku ya jumatano, hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu, licha ya kusisitiza haja na umuhimu wa vijana wa kiume kuwa mstari wa mbele kupinga ukatili dhidi ya wanawake.Lakini pia alitoa tuzo kwa vijana sita kutoka mabara sita walioshinda ubunifu wa fulana( T- Shirts) zenye nembo maalum ya kampeni dhidi ya unyanyasaji wa wanawake.
Miongoni mwa washindi hao, yuko kijana wa Kitanzania, Mwasapi Kihongosi ambaye pia ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliyekuwa mshindi wa kwanza Barani Afrika . maadhimisho hayo yalihudhuliwa na Mkurugenzi Mkuu wa chombo maalum cha Umoja wa Mataifa kinachoshughulikia masuala ya wanawake- UN WOMEN Michelle Bachelet na viongozi mbalimbali wakiwamo mabalozi.
“ Ninapenda kuwapongeza sana vijana hawa sita ,ambao wameshinda tuzo ya ubunifu wa fulana zenye nembo na ujumbe maalum. Wito wangu kwenu na kwa vijana wote wa kiume ni huu, unganeni kukomesha unyanyasaji dhidi ya wanawake. Na nimefurahi kuona wengi wenu ( wageni waalikwa) mmevaa fulana walizobuni vijana hawa ” akasema Ban Ki Moon.
Akasema kuwa kauli mbiu ya mwaka huu ya siku ya kimataifa ya kukomesha ukatili dhidi ya wanawake ni “ Uongozi wa vijana”.
Akaongeza kuwa yeye binafsi kila anaposafiri hujaribu kukutana na kuwasilikiza vijana, kwa sababu vijana kwa kupitia hisia na nguvu zao wanaouwezo mkubwa wa kuifanya dunia yetu kuwa mahali pazuri.
Ban ki Moon amesisitiza kwamba kwa kupitia vijana hao sita waliobuni na kushinda mpango wa kimataifa wa kutengeneza nembo na fulana kwaajili ya kampeni ya ukatili dhidi ya wanawake , kila mtu na hasa vijana anatakiwa kusema “ Hapana” kwa unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana.
Akizungumzia zaidi kuhusu ukatili dhidi ya wanawake, Katibu Mkuu wa UM amesema . “ wote tunaelewa kwamba unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana uko wa aina nyingi, unyanyasaji huu ambao uko katika nchi zilizoendelea na zinazoendelea ni pamoja na ubakaji, tohara, ukatili wa majumbani, ubaguzi katika mashule, unyanyasaji wa wanawake katika maeneo ya kazi na ukatili wa kijinsia katika maeneo yenye vita”.
Akaongeza kwamba kundelea kuwapo kwa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake siyo tu kwamba ni jambo lisilokubalika lakini pia ni kikwazo kikubwa katika kufikia usawa kamili wa kijinsia.
Akazitaka serikali na washirika wote duniani, na uongozi wa vijana kuunganisha nvugu zao na mawazo yao kukomesha gonjwa hilo la ukatili dhidi ya wanawake. Na kwa kufanya hivyo ulimwengu utakuwa mahali pa haki, amani na usawa.
Kwa Upande wake Mkurugenzi Mkuu wa UN-Women Michelle Bachelet amesema ingawa nchi nyingi zimetunga sheria dhidi ya vitendo vya ukatili kwa wanawake, bado kunahitaji uwajibikaji na utashi wa kisiasa kutoka kwa viongozi na wananchi kwa ujumula katika kulikabili tatioz hilo
Akaainisha masuala kumi na sita ambayo anadhani kama yakitekelezwa yanaweza kusaidi kama si kupunguza basi kumaliza kabisa ukatili huo. Akayataja mambo hayo kuwa ni pamoja na kuwa na sera madhubuti za kumaliza ukatili dhidi ya wanawake, utoaji wa huduma za dharura kwa waathirika, kuwashirikisha wanaume na vijana wa kiume na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria watuhumiwa wa ukatili dhidi ya wanawake.
Vijana hao sita kila mmoja wao sasa anakuwa Balozi maalum katika kampeni zitakazozinduliwa mwakani kuhusu ukatili dhidi ya wanawake. Kwa upande wa Afrika kampeni hizo zinatarajiwa kuzinduliwa mapema mwakani kwa washiriki kupanda mlima Kilimanjaro kupinga ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.
mwisho
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269