Breaking News

Your Ad Spot

Jan 28, 2012

MGOMO WA MADAKTARI: PINDA KUKUTANA NA MADAKTARI KESHO JUMAPILI

Waziri Mkuu Mizengo Pinda
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda kesho  (Jumapili, Januari 29, 2012) atakutana na madaktari waliofanya mgomo.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu leo jijini Dar es Salaam, imesema Pinda atakutana na madaktari hao saa 4:00 asubuhi katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam, na kuwataka madaktari wote wanaohusika kuhudhuria bila kukosa.
 
"Madaktari hao kwa nyakati tofauti wamekuwa wanaomba kuonana na Waziri Mkuu na mara zote Waziri Mkuu amekubali kuonana nao lakini hawakutokea", ilisema taarifa hiyo na kuongeza.
 
"Pamoja na kukubali huko kwa Waziri Mkuu, tarehe 25 Januari 2012 katika Mkutano wake na Wahariri wa Vyombo vya Habari aliwaomba Madaktari kuwa alikuwa tayari kuonana nao lakini hawakutokea".
 
Taarifa ilisema, ili kuendeleza jitihada za kutaka kuonana na madaktari hao, Waziri Mkuu alituma Uongozi wa Serikali ukiongozwa na Mawaziri wa Afya na Ustawi wa Jamii; na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kuonana na Madaktari kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Starlight tarehe 27 Januari 2012. Kwenye Mkutano huo madaktari waliwasilisha malalamiko yao na kuomba kuonana na Waziri Mkuu. Kufuatia maombi hayo, Waziri Mkuu amewaandikia madaktari hao barua ya kuwataka kuonana nao Kesho, tarehe 29 Januari 2012 kwenye Ukumbi wa Karimjee, saa 4:00 asubuhi.
 
Kabla ya kufikia uamuzi huo, kulikuwa na mawasiliano kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Uongozi wa Medical Association of Tanzania (MAT) na baadaye Mwenyekiti wa Muda wa Kamati ya Madaktari kuhusu mgomo wa Madaktari unaoendelea.
 
Aidha, Viongozi mbalimbali wa Serikali wamefanya mazungumzo na Wawakilishi wa Madaktari na Madaktari wenyewe kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Starlight ili kuweza kupata ufumbuzi wa matatizo yaliyowasilishwa Ofisi ya Waziri Mkuu.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages