Breaking News

Your Ad Spot

Jan 30, 2012

RAIS KIKWETE NA WATANZANIA WAMETUNUKIWA TUZO MAALUM YA ALMA


UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

Telephone: 255-22-2114512, 2116539

Fax: 255-22-2113425




PRESIDENT’S OFFICE,
      THE STATE HOUSE,
       P.O. BOX 9120,  
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
 
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Tanzania na Rais wa Jamhuri ya Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete wametunukiwa Tuzo Maalum kutokana na juhudi zilizotukuka katika kupambana na ugonjwa wa malaria katika Tanzania na katika Bara la Afrika.
Tuzo hiyo inayojulikana kwa lugha ya Kiingereza kama Alma Award for Excellence imetolewa kwa Tanzania na Rais Kikwete na Umoja wa Marais wa Afrika katika Kupambana na Ugonjwa wa Malaria – African Leaders Malaria Alliance (ALMA) na kukabidhiwa kwake leo, Jumatatu, Januari 30, 2012, mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Tuzo hiyo imekabidhiwa kwa Rais Kikwete na Mwenyekiti Mpya wa ALMA, Rais Sirleaf Johnson wa Liberia wakati wa chakula maalum cha mchana kilichoandaliwa na ALMA kwenye makao makuu ya Umoja wa Afrika (AU), ikiwa ni sehemu ya Mkutano wa 18 wa Viongozi wa AU uliomalizika leo mjini Addis Ababa. Mkutano huo ilianza jana na Rais Kikwete yupo Addis Ababa kuhudhuria mkutano huo.
Akiwasilisha maelezo ya uteuzi wa Rais Kikwete kutunukiwa Tuzo hiyo, Katibu Mtendaji wa ALMA, Mama Johannah-Joy Phumaphi amemweleza Rais Kikwete: “Ni heshima isiyo kifani kwangu kukujulisha kuwa umeteuliwa kupokea Tuzo ya ALMA Award for Excellence, kwa kutambua juhudi nyingi na mchango mkubwa uliotolewa na Tanzania, chini ya uongozi wako, katika kupambana na balaa la malaria.”
Viongozi na nchi nyingine zilipokea Tuzo hiyo katika sherehe hiyo fupi ya leo ni Benin, Cameroun na Kenya.
Hii ni mara ya pili kwa Tuzo hiyo kutolewa katika historia ya ALMA. Na Tuzo hiyo linalenga kutambua mchango mkubwa wa nchi ambazo zimefikia malengo makuu katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria, ugonjwa ambao unaendelea kuua watu wengi zaidi katika Afrika kuliko ugonjwa mwingine wowote.
Washindi wa Tuzo hiyo huchaguliwa na jopo linalojitegemea la watalaamu na mabingwa wa kupambana na malaria ambao huchaguliwa na wadau wakubwa wa mapambano dhidi ya ugonjwa huo kutoka sekta ya umma na sekta binafsi, taasisi zisizokuwa za kiserikali (NGO’s), na wasomi na wanazuoni.
Mwaka huu Tuzo hiyo imetolewa kwa nchi ambazo zimeondoa kodi na vikwazo visivyokuwa vya kodi kwenye dawa na vifaa maalum vya kupambana na ugonjwa wa malaria, zilizopiga marufu baadhi ya dawa zisizokubalika kimataifa katika kupambana na ugonjwa wa malaria, ama nchi zilizoonyesha mafanikio yasiyokuwa ya kawaida katika kukabiliana na ugonjwa huo.
Mbali na jitihada zake kubwa za kupambana na ugonjwa wa malaria katika Tanzania katika kipindi chake chote cha uongozi wake, Rais Kikwete pia amekuwa Mwenyekiti Mwanzilishi wa ALMA na ameongoza Umoja huo tokea ulipoanzishwa Septemba mwaka 2009 hadi leo, Jumatatu, Januari 30, 2012, alipokabidhi uongozi huo kwa Rais Sirleaf Johnson ambaye amekuwa Makamu wake kwa miaka yote miwili na miezi minne iliyopita.
ALMA ni Umoja Maalum wa wakuu wa nchi za Afrika ambao wanafanya kazi pamoja na kushirikiana katika kukabiliana na ugonjwa wa malaria katika Bara hilo. Mpaka sasa Umoja huo unao wanachama 41 ambao ni Wakuu wa Nchi za Afrika pamoja na Umoja wa Afrika wenyewe.
Mbali ya Umoja wa Afrika na Tanzania, nchi nyingine wanachama wa ALMA ni Angola, Benin, Botswana, Burkina Faso, Cameroun, Cape Verde, Comoro, Jamhuri ya Congo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Djibout, Misri, Equatorial Guinea, Ethiopia, Gambia, Ghana, Guinea, Kenya, Lesotho, Liberia, Madagascar, Malawi na Mali.
Nyingine ni Mauritania, Mauritius, Mozambique, Namibia, Nigeria, Rwanda, Sao Tome and Principe, Senegal, Syechelles, Sierra Leone, Somalia, Afrika Kusini, Sudan Kusini, Sudan, Togo, Uganda, Zambia na Zimbabwe.
ALMA inalenga kutoka mchango wake kwenye jitihada na mafanikio ya AU, wadau wa taasisi ya Roll Back Malaria na malengo ya Umoja wa Mataifa kwa kuongeza kasi ya kuhakikisha kuwa kila binadamu analindwa dhidi ya malaria na kila mgonjwa anatibiwa kwa lengo la kuhakikisha kuwa hakuna binadamu atakayekuwa anakufa kwa ugonjwa huo ifikapo mwaka 2015.
Kwenye sherehe ya leo, pia nchi nyingine tatu zimepokea Tuzo maalum kwa juhudi na jtihada zao katika kuondoa vikwazo vya kodi na visivyokuwa vya kodi kwenye dawa na vifaa vya kupambana na malaria na pia kupiga marufuku dawa zisizokubalika duniani katika vita dhidi ya malaria.  Nchi hizo ni Burundi, Mozambique na Rwanda.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
30 Januari, 2012

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages