Breaking News

Your Ad Spot

Jan 19, 2012

TANZANIA YAWASILISHA UMOJA WA MATAIFA ANDIKO LA KUDAI NYONGEZA YA ENEO LA BAHARI

Waziri Anna Tibaijuka akidhi andiko hilo Tarassenko
NA MWANDISHI MAALUM, NEW YORK
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imewasilisha  katika  Umoja wa Mataifa, Andiko la kudai eneo la nyongeza  lenye ukubwa wa  maili 16,000 nje ya eneo la sasa la maili 200 za Ukanda wa Kiuchumi wa Bahari.

 Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Anna Tibaijuka (Mb) ndiye aliyewasilisha Andiko hilo, kwa niaba ya serikali,  katika hafla fupi na ya kihistoria   iliyofanyika  siku ya  jumatano katika ofisi za  Idara ya Umoja wa Mataifa  inayoshughulikia masuala ya  Bahari  na Sheria ya  Bahari.

Andiko hilo limepokelewa na  Mkurugenzi wa Idara hiyo, Bw. Sergei Tarassenko kwa niaba ya  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. ambaye aliipongeza Tanzania kwa hatua hiyo muhimu na kuahidi kwamba Idara yake kupitia, Kamisheni ya Umoja wa Mataifa inayohusika na mipaka ya  baharí italifanyika kazi Andiko hili.

Aidha Mkurugenzi huyo ameielezea Tanzania, kama moja kati ya nchi inayoheshima sana  na  yenye historia nzuri   katika Umoja wa Mataifa.

Akizungumza wakati wa kuwasilisha  Andiko hilo, Waziri Anna Tibaijuka,  amesema kwa kuwasilisha Andiko hilo, Tanzania  si tu kwamba imefanya kazi ya uhakika ya maandalizi na hatimaye uwasilishaji lakini ni hatua kubwa kwa maendeleo ya kiuchumi  na kijamii kwa Tanzania.

Akabanisha kwamba  mchakato wa  maandalizi ya Andiko hilo ambao umechukua miaka mitano, umewashirikisha wataalamu mbalimbali wakiwamo  wa ndani na nje , ikiwa ni pamoja na kuzihusisha nchi ambazo zinapakana kibahari na Tanzania.

Akizungumza manufaa ya kudai nyongeza ya eneo hilo, Waziri Tibaijuka anasema,
“ Tanzania itanufaika kwa kuongeza ukubwa wa eneo la mipaka ya nchi lakini  la msingi zaidi ni unufaikaji wa rasilimali zikiwamo za mafuta na gesi na madini ambazo zitakuwamo katika eneo hilo  jipya, rasilimali ambazo kwa sasa  zinaelekea kutoweka  katika eneo la maili 200”.

Eneo ambalo Tanzania inadai liongezwe  la maili 61, 000  ukubwa wake ni sawa na eneo la mikoa mitatu ikiunganishwa kwa pamoja. 

Aidha kuongezwa kwa eneo hilo kutaisaidia pia serikali katika  masuala ya ulinzi na usalama hasa katika  kipindi hiki ambacho vitendo vya  uharamia wa baharini vikiwa vimeongeza katika eneo la bahari ya Hindi.

“ Pamoja na kuwasilisha Andiko hilo, lakini nchi yangu inapenda pia kutoa ombi la pekee  kwa  idara yako, kuangalia uwezekano wa kuharakisha mchakato wa kupitia nyaraka na vielelezo tulivyowasilisha katika Andiko letu, kwani itatusaidia sana katika ulinzi wa eneo la mipaka yetu dhidi ya uharamia” akasisitiza  Waziri .

Na kuongeza kwamba Tanzania, kama ilivyo kwa nchi nyingine ambazo zinaendelea zinatajitaji msaada mkubwa kutoka kwa wadau mbalimbali ikiwamo Idara ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya bahari na sheria ya bahari katika kuukabili uharamia.

 Faida nyingine ukiacha za kiuchumi ni kwa  wataalamu  wa fani mbalimbali kuwa na fursa ya  kufanya  utafiti katika eneo hilo  hapo litakapokuwa limeridhiwa rasmi na kuwa sehemu ya Tanzania.

Baada ya kuwasilisha Andiko hilo,   hatua inayofuatia ni kwa Tanzania kupitia wataalamu wake,  itatakiwa kulitetea Andiko  hilo mbele ya Makamishna wa Kamisheni ya  Umoja wa Mataifa inayohusika na  Mipaka ya  Bahari utetezi huo utafanyika mwezi  Agosti mwaka huu.

Tanzania imewasilisha Andiko hilo kwa kuzingatia Sheria  ya kimataifa ya Bahari namba 76 kifungu kidogo cha 4, sheria hiyo inaziruhusu nchi ambazo  ziko kando kando ya bahari kudai eneo la nyongeza iwapo zitakidhi vigezo  vilivyotolewa na Umoja wa Mataifa.

Mchakato wa kuanda Andiko hilo   ulianza mwaka 2007 ukiwashirikisha wataalamu wa kada mbalimbali kutoka Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi,  Serikali ya Mapinduzi  Zanzibar, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Chuo Kikuu  cha Ardhi na Mazingira,  Wizara ya   Sayansi na Teknolojia na Shirika la Maendeleo ya Petroli ( TPDC). 

Sehemu kubwa ya Mradi  imefadhiliwa na   Serikali Kuu na kwa kusaidiwa na   Serikali ya Norway.

Hafla ya kuwasilisha Andiko hilo imehudhuriwa  na  Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Mhe. Ombeni Sefue,  na   waheshimiwa wabunge,   Zakhia Meghji na  Abulrahman Hassan Shah ambao ni wajumbe wa Kamati ya  Bunge ya  Ardhi, Maliasili na Mazingira.

 Wengine waliohudhuri  hafla hiyo ni  baadhi ya wataalamu waliohusika na maandalizi ya Andiko hilo ambao ni Dr. Sellasie Mayunga, Prof. Evelyne Mbende,  Bw. Ayoub Mohamed Mahmoud kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,   Bw. Kelvin Komba na  Bi. Verdiana Mashingia. 

 Tanzania inakuwa nchi ya 59 kuwasilisha Andiko la kudai nyongeza ya eneo la bahari na ikiwa ni nchi 10  kutoka  Afrika kufanya hivyo.
Kutoka  kulia ni Mhe. Zakhia Meghji ( Mb), Bw.  Sergei Tarassenko ambaye ameshika sehemu ya nyaraka za Andiko la kudai eneo la maili 61,000 za bahari, Mhe. Waziri Anna Tibaijuka ( Mb), Mhe. Ombeni Sefue, Balozi wa Tanzania Katika Umoja wa Mataifa,  Mhe. Abulrahman Hassan Shah (Mb) na Bw.  Ayoub Mohamed Mahmoud  Mkurugenzi  wa Sera   na  Mipango Wizara ya Ardhi, Makazi na Madini  Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ambaye pia alimwakilisha Waziri wake katika hafla hiyo. 
 Ujumbe wa Tanzania  ukiwa katika  furaha kubwa na Mkurugenzi wa Idara ya Umoja wa Mataifa  ya masuala ya Bahari na Sheria ya Bahari Bw. Sergei Tarassenko  na maofisa wake ,mara baada ya makabidhiano ya Andiko la kudai nyongeza ya eneo la maili ya 61,000 za bahari lililowasilishwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Umoja wa Mataifa. katikati ni  Boksi ambalo ndani yake mnamakabrasha na nyaraka nyeti zinazo husu  Andiko la madai hayo, Andiko ambalo mchakato wake umechukua miaka mitano kuuandaa. Tanzania imewasilisha Andiko hilo kwa mujibu wa Sheria  ya kimataifa  ya masuala ya bahari namba 76 kifungu kidogo cha 4 ambayo inatoa ruksa kwa nchi ambayo iko kando kando ya bahari kudai nyongeza ya eneo la bahari endapo itakidhi  vigezo vilivyotolewa na Umoja wa Mataifa. Tanzania inakuwa nchi ya 59 kuwasilisha dai  hilo.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages