.

MUKAMA ANG'AKA KUHUSISHWA NA KASHFA MRADI WA MACHINJIO DAR

Apr 4, 2012


Katibu Mkuu wa CCM Wilson Mukama akizungumza leo

Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama amekana na kung'aka vikali kuhusika  kwa aina yoyote katika kashfa ya ubadhiribu kwenye mradi wa ujenzi machinjio ya kisasa jijini Dar es Salaam, anaripoti Mwandishi Wetu.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mukama amesema hajawahi kuandika barua zozote kuhusiana na mradi huo ambao inadaiwa kampuni ya East Agfrican Meat ambayo ilipewa kazi ya kuuendesha ilisababisha  hasara ya sh. bilioni 2.7.


Mukama amesema licha ya kwamba alikuwepo katika Halmashauri ya Jjiji la Dar es Salaam, wakati mradi unabuniwa  lakini hakuhusika kamwe katika kuzichangisha  fedha Halmashauri za Ilala, Kinondoni na Temeke,  mwaka 2006 kama ilivyoandikwa na gazeti la Tanzania Daima.


Alisema, aliteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa  Wizara ya Tawala za Mikoa na  Serikali za Mitaa , Januari 20, 2006 na hivyo kutoweza kuhusika kwa vyovyote vile  na uchangishaji huo ambao kwa mujibu wa taarifa ulifanyika baadaye.


Mukama amesema, licha ya kuwepo maneno mengi kuhusu mradi huo, mradi wenyewe haukuwa na matatizo kitaalam zaidi ya ukweli kwamba uendeshaji wake ndio ulikuwa na kasoro.


Alisema haikuwa jambo rahisi kitaalamu kwa mradi mkubwa kama huo wenye thamani ya sh. bilioni kumi uliokuwa ukilenga kuchinja  ng'ombea 800 kwa siku, uendeshwe kwa kutegemea michango ya halmashauri tatu za jiji hilo.


Mukama amezikana pia taarifa za kudaiwa kuhuska na utiaji saini mkataba kati ya Halmashauri ya Jiji na Kampuni ya Nicol Oktoba 13, 2006 na pia kukana kuhusishwa na utiaji saini kusitishwa kwa mradi huo  mwaka 2009, akisema wakati huo alikuwa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na hakuwa akifanya kazi katika Halmashauri ya Jiji.


"Huu ni uzushi wa ajabu sana na wa makusudi, inawezekanaje kuandika barua  mwaka 2006,  kisha nikatia saini makubaliano mwaka 2009 wakati sikuwa tena Mkurugenzi wa Jjiji?" alihoji Mukama.


Mukama amesema atalichukulia hatua za kisheria gazeti la Mtanzania lililoandika habari za kumhusisha na taarifa hizo katika toleo lake la jana.


Wakati Mukama akizungumza na waandishi wa habari leo kuhusu gazeti la Tanzania Daima kumhusisha katika kashfa hiyo, gazeti hilo, limemuomba radhi mwishoni mwa habari kuhusiana kanusho hilo ambayo limeiweka ukurasa wa tatu leo.


"Gazeti la Tanzania Daima linapenda kutumia fursa hii kumuomba radhi, Wilson Mukama kutokana na usumbufu wowote alioupata kutokana na habari iliyoandikwa katika gazeti letu la jana. Mhariri", limeandika Tanzania Daima mwishoni mwa habari yenye kichwa, "Mukama: Msinihusishe na kasha mradi wa machinjio", katika ukurasa wake wa tatu.

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ª