.

SYRIA INAPOENDELEA KUIUMIZA KICHWA JUMUIYA YA KIMATAIFA

Apr 7, 2012


Kofi Annan akisalimiana na  Meja Jenerali Robert Mood raia wa Norway 

Na Mwandishi Maalum, New York
 Licha ya kwamba serikali ya Syria  imekubali kutekeleza mapendekezo  ya kumaliza vurugu yaliyotolewa na  Mjumbe Maalum wa Pamoja wa  Umoja wa Mataifa na Muungano wa  Nchi za Kiarabu, Mhe. Kofi Annan. Damu bado inaendelea kumwagika nchini humo.
      Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon wakati Baraza  Kuu la 66 la Umoja wa Mataifa, lilipokutana siku ya Alhamisi katika mkutano wake usio rasmi ili kupokea taarifa ya maendeleo ya juhudi zinazofanywa na Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa nchi za Kiarabu, Mhe. Kofi Annan.
      Na kwa sababu hiyo Ban Ki Moon ametoa wito kwa  Jumuiya ya Kimataifa   kuunga mkono na kusaidia juhudi za mjumbe huyo maalum. Huku akilitaka Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuendelea kutoa shinikizo kwa pande zote zinahohusika na mgogoro huo kukomesha vita na  mateso.
      Mkutano huo uliitishwa na Rais wa Baraza Kuu la 66 la Umoja wa Mataifa, Bw Nassir Abdulaziz Al Nasser ambapo Mhe. Kofi Anna alizungumza kwa njia wa Video-Link kutokea Geneva
     “ Pamoja na serikali ya Syria kukubali mpango  na mapendekezo ya awali ya  Mjumbe Maalum ya kutatua mgogoro huo, ghasia na mashambulizi katika maeneo ya raia hayaja simamishwa. Hali katika nchi hiyo inaendelea kuzorota” akasema Ban Ki Moon.
      Akawaeleza wajumbe wa UM kwamba Mhe. Annan aliwasilisha mapendekezo Sita wakati alipokuwa Damascus (Syria )mwezi uliopita. Baadhi ya mapendekezo hayo ni kusitisha ghasia na mauaji, kutoa fursa kwa mashirika ya kimataifa  kutoa  misaada ya kibinadamu, kuachia wafungwa na kuanzisha majadiliano ya kisiasa.
     “ Serikali ya Syria ilimtaarifu Mjumbe Maalum kwamba itakuwa imekamilisha kuondoa askari na silaha nzito kutoka katika maeneo ya watu ifikapo April 10 mwezi huu.  Mamlaka ya Syria inawajibu sasa wa kutekeleza kwa vitendo ahadi hiyo kwa ukamilifu na bila ya masharti  yoyote” akasisitiza Katibu Mkuu.
      Akatoa wito kwa Rais wa Syria Bashar al- Assad, serikali yake na wote wanaohusika kuonyesha utashi wa kiuongozi na pia akatoa wito kwa  upande wa  upinzani  nao kuwa tayari kusitisha mapigano na unyanyasaji kama ilivyoanishwa kwenye mpango wa Mhe. Annan.
 “ wengi wenu mliopo hapa mmetaka kuwapo kwa juhudi za mwisho za kuutatua mgogoro huu kwa njia za amani. Na baadhi yenu mmeonyesha wasi wasi wenu  kwamba vita kamili inaweza kujitokeza ikiwa   juhudi za kidiplomasia zitashindwa.  Ni kweli hali  nchini Syria inaendelea kuzorota. Ninawaomba muunge mkono juhudi za Mhe. Annan katika kipindi hiki kigumu” akasihi Ban Ki Moon.
      Aidha Ban Ki Moon  amebainisha kwamba matumizi ya kijeshi nchini Syria hayatakuwa na  manufaa yoyote na badala yake amesisitiza kuanza kwa mchakato wa mazungumzo na  kwamba  muda wa maneno umekwisha na jumuia ya kimataifa inaonyeshe kwamba  iko pamoja na  wananchi wa Syria.
      Kwa upande wake Mjumbe Maalum  Kofi Annan amesema serikali ya Syria na  upande wa wapinzani lazima sasa waache mapigano na vitendo vyote vya unyanyasaji.
     Na kuongeza kwamba kama ilivyokubaliwa na mamlaka ya Syria  timu ya umoja wa mataifa, ikiwa ni pamoja  maofisa  kutoka Idara ya Operesheni za Kulinda Amani (DPKO), watakwenda  nchini humo ili kuanza maandalizi ya kiufundi kwa ajili ya kupeleka waangalizi wakufuatilia  usitishaji wa vita vya kutumia silaha na utekelezaji kamili wa  mapendekezo yake sita ya kuleta amani. 
     “ Naomba makamanda  wa serikali na upinzani kutoa maelekezo ya wazi  kwa walinzi wa amani wa umoja wa mataifa  wakishafika nchi humo kusimamia uondoaji wa majeshi” akasema Annan”
Akasisitiza kwamba serikali ya Syria  ilimhakikishia kwamba ifikapo Aprili  10 itakuwa imeondoka vikosi  vyake katika makazi ya   watu.
     “ Baada ya  serikali kukamilika kwa zoezi la kuondoka majeshi hapo Aprili 10. Pande zote zitatakiwa  kusitisha kabisa mapigano ifikapo saa 0600 kwa saa za Damascus alhamisi, Aprili 12. Akasema Mjumbe Maalumu.     
      Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa zaidi ya watu 8,000, wengi wao wakiwa raia wameuawa,pamoja na  wengine milioni wakihitaji misaada ya kibinadamu ndani ya Syria  huku maelefu wengine wakiwa wameyakimbia makazi yao tangu mapigano yalipoanza nchi humo.
Wajumbe wa Baraza Kuu la 66 la Umoja wa Mataifa katika mkutano wao ambao haukuwa rasmi, ambapo walipokea taarifa ya  Mjumbe  Maalum wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Nchi za Kiarabu, Mhe. Kofi Annan ambaye amepewa jukumu la  kushughulia mgogoro unaoendelea nchini Syria. katika mkutano huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki  Moon amesema serikali ya Syria licha ya kukubali kutekeleza mapendekeo sita yaliyotolewa na mjumbe  maalum, bado hali ni tete na damu inaendelea kumwagia. Kwa upande wake kofi Annan aliyezungumza kwa  njia ya Video-Link kutokea Geneva anasema wakati umefika kwa pande zote mbili kusitisha mapigano mara moja na kuondoa majeshi yao kwenye maeneo ya watu na kupisha mazungumzo ya kurejesha amani.

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ª