Baadhi ya walinzi wa amani wa UN walioko Syria wakizungukwa na wananchi |
New York
Mkuu Idara ya Operesheni za Ulinzi wa Amani za Umoja wa
Mataifa (DPKO) , Balozi Herve Ladsous, ameziomba nchi ambazo zimepelekewa
maombi ya kutoa waangalizi wa amani kwenda
kuhudumu nchini Syria, kutoa waangalizi hao haraka na mapema iwezekanavyo.
Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, ni kati ya mataifa ambayo yameombwa kutoa wanajeshi wake.
Balozi Ladsous ametoa wito huo siku ya ijumaa wiki hii, wakati alipokutana
na kufanya mazungumzo na wawakilishi wa
nchi ambazo zinashiriki katika Operesheni za ulinzi wa kulinda amani za UN maarufu kama TCC.
Ombi la Balozi Ladsous kwa nchi hizo linakuja ikiwa ni takribani wiki moja tangu
Baraza Kuu la Usalama kupitisha Azimio namba 2043 ( 2012) linalotakamka pamoja na mambo mengine, kuanzishwa kwa Misheni ya Umoja wa Mataifa ya kusimamia amani Syria (
UNSMIS) itakayokuwa na waangalizi 300 wanaotakiwa kupelekwa nchi humo ndani ya
kipindi cha siku 90 tangu kupitishwa kwa Azimio hilo.
“ Ninawaomba sana sana, tafadhali fanyeni hima, kutupatia
waangalizi wa amani, wasilianeni na
Makao Makuu ya Nchi zenu. Hatuna muda na dunia inatuangalia”. Akasisitiza na
kusihi ombai alilokuwa akirudia mara
kwa mara ,Mkuu huyo wa DPKO aliyekuwa
ameandama na maafisa waandamizi kutoka
Idara hiyo.
Kwa
mujibu wa Bw. Herve Ladsous ili Azimio hilo liweze kutekelezwa
kikamilifu, waangalizi wa amani 100 wanatakiwa wawe wamewasili nchini Syria ndani ya siku 30
na idadi itakayobakia ya waangalizi
200 iwe imekamilika ndani ya siku 60.
Akasema
kwamba ili malengo hayo yaweze kufikiwa
kama ilivyopangwa, ni vema na muhimu nchi zilizoombwa zikawasilisha majina ya wanajeshi
wanaowapendekeza haraka na mapema
iwezekanavyo ili taratibu za maandalizi ya kuwapeleka Syria yaweze kutekelezwa.
Akifafanua
zaidi kuhusu majukumu ya waangalizi hao,
ambao hawatakuwa na silaha za aina
yoyote ile , kuwa jukumu lao kuu la
msingi litakuwa ni kufuatilia na kusimamia
kwa ukamilifu utekelezaji wa ajenda
Sita za mpango wa amani kama zilivyoainishwa na Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa na Muungano
wa Nchi za Kiarabu, Bw. Kofi Annan.
Mapendekezo
hayo yanataka pande zote husika nchini
humo kusitisha mapigano na vitendo vyovyote
vya uvunjifu wa amani, kuondoa
wanajeshi na silaha katika makazi ya
watu, kuruhusu mashirika ya misaada ya kibinadamu na hatimaye kuruhusu kuanza mchakato wa mazungumzo ya amani
yatakayozingatia matakwa ya watu wa
Syria.
Akabainisha
kwamba waangalizi hao wa amani 300
watasambazwa katika maeneo 25 ambayo yameainishwa kama maeneo tete
yanayohitaji uwepo wa maafisa hao.
Hadi
kufikia siku ya ijumaa wiki hii kulikuwa na waangalizi wa amani
wapatao 14 ambao wapo tayari nchini Syria kwa lengo la kusimamia mchakato huo wa usitishswaji wa mapigano na uondoaji wa silaha katika makazi ya watu na pia kutoa taarifa ya kile
kinachoendelea.
Hata
hivyo idadi hiyo ya waangalizi hao imekuwa ikilalamikiwa na wananchi wa Syria
kwamba haitoshi ikilinganishwa na ukubwa wat atizo.
Wakati huo huo katibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, ametangaza uteuzi wa Meja Jenerali Robert Mood raia wa
Norway kuwa Mkuu wa Misheni ya Usimamizi
ya Umoja wa Mataifa nchini Syria (UNSMIS)
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269