.

WANAWAKE WA CHADEMA KUKUTANA ARUSHA

Apr 23, 2012


Na Rose Jackson,Arusha
ZAIDI ya wajumbe  20 ambao ni viongozi wa baraza la wanawake wa Chadema(Bawacha) mkoani Arusha wanataraji kukutana kwa pamoja hivi karibuni jijini Arusha kwa lengo kuzungumzia mikakati ya kuimarisha uhai wa baraza hilo kuanzia ngazi za mashina,matawi hadi kata.

Viongozi wa baraza hilo wanataraji kukutana mnamo Aprili 28 mwaka huu ambapo wanatoka katika wilaya za Arusha,Arumeru Mashariki,Arumeru Magharibi ,Longido,Monduli,Ngorongoro na Karatu.

Aliwataja washiriki wengine katika mkutano huo ni pamoja na wabunge wa viti maalumu kupitia Chadema mkoani Arusha ambao ni Joyce Mukya,Rebeca Mngodo sanjari na Cecilia Pareso.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mwenyekiti wa baraza hilo mkoani Arusha,Cecy Ndossi alisema kwamba mkutano huo utawashirikisha pia wenyeviti na makatibu wa Bawacha kutoka wilaya mbalimbali mkoani Arusha.

Alisema kwamba  lengo kuu la kuwakutanisha wajumbe hao ni kujadili changamoto mbalimbali zinazojitokeza ndani ya baraza hilo sanjari na kuimarisha uhai wake kuanzia ngazi za chini hadi taifa.

Ndossi,alisema kwamba  katika mkutano huo watajikita kubadilishana ujuzi wa namna ya kumkomboa mwanamke wa kitanzania katika mikono ya unyanyasaji wa kijinsia ambao umekuwa ukijitokeza katika jamii mbalimbali nchini.

“Nimeamua kuitisha kikao hiki kwa lengo la kuimarisha uhai wa baraza letu pamoja na kuzungumzia changamoto mbalimbali za kumkomboa mwanamke wa kitanzania hapa nchini”alisema Ndossi

Hatahivyo,alisisitiza kwamba wajumbe mbalimbali katika mkutano huo pia watapata fursa ya kujadili mchakato wa uundwaji wa katiba mpya nchini ili waweze kuwa mabalozi wazuri ambao watasaidia kueneza umuhimu wa uundwaji wa katiba hiyo katika ngazi za wilaya hapa nchini.

“Ushiriki wa wanawake kuhusu uundwaji wa katiba mpya mkoani Arusha kwa mtizamo wangu bado elimu haijatolewa kwa kutosha hivyo mkutano wetu utatoa fursa ya kuzungumzia suala hilo kwa undani”alisisitiza mwenyekiti huyo

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ª