Breaking News

Your Ad Spot

May 10, 2012

BAN Ki MOON ALAANI MLIPUKO SYRIA

Ki Moon na Asha-Rose Migiro kwenye mkutano huo
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon,  amelaani vikali shambulio la mlipuko uliotokea siku ya jumatano katika kizuizi karibu na  mji wa Dar’a kusini mwa Syria, muda mfupi baada ya   msafara wa waangalizi wa amani wa Umoja wa Mataifa kupita.

Akizungumza na Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa Umoja wa Mataifa,  Ban Ki Moon amesema tukio hilo linatakiwa kulaaniwa na jumuia yote ya kimataifa na ni kielelezo  cha dhahiri kwamba hali nchi Syria  inazidi kuwa mbaya.

 “ Ninalaani kwa nguvu zangu zote tukio hili, ni tukio ambalo halikubaliki, linatakiwa kulaaniwa vikali na jumuia yote ya kimataifa. Hiki ni kielelezo cha wazi cha namna gani waangalizi wetu wa amani wanavyokabiliwa na mtihani mkubwa, lakini pia ni kielelezo cha hali halisi ya kile kinachowasibu wananchi wa  Syria kila siku”. Akasema Katibu Mkuu.

“ Nimeongea na  Meja Jenerali Robert Mood,   mkuu wa Misheni ya Usimamizi wa Amani ya Umoja wa Mataifa nchini  humo ( UNSMIS) amenipa taarifa kamili ya nini kilichotokea. Hakuna  aliyejeruhiwa kufuatia mlipuko huo au uharibifu kwa magari ya  Umoja wa Mataifa ingawa kulikuwa na  majeruhi kwa upande wa askari kumi wa Syria waliokuwa wakisindikiza msafara huo” akafafanua Ban Ki Moon
 Katika mazungumzo hayo ambayo pia  yalihudhuriwa na  Naibu Katibu Mkuu, Asha-Rose Migiro.

Katibu Mkuu  ameelezea  kwamba kuendelea kutokea kwa milipuko hiyo  anapata wasiwasi mkubwa   wa uwezekano wa kutokea kwa vita kamili ya wenyewe kwa wenyewe nchi humo ikiwa pande mbili zinazohusika hazitaweka silaha zao chini, kusitisha mapigano na kuanza mazungumzo ya amani.

Akawasihi sana mabalozi hao kuunga mkono juhudi za   mjumbe maalum  Bw. Koff Annan  za kujaribu kurejesha amani nchi  Syria na vile vile kuunga mkono upelekekaji wa waangalizi wa amani 300.

Aidha akatumia  mazungumzo hayo kuzishukuru nchi 38 ambazo zimekubali kutoa wanajeshi wa kwenda kuangalia amani nchi humo.

“ Ninapenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa nchi 38 ambazo zimeonyesha nia ya kutoa watu wao kwenda kusaidia kuangalia amani nchini Syria, natambua uzito wa  jukumu hili na hatari inayowakabiri ni kazi kubwa lakini ni lazima tufanya hivyo kwaajili ya watu wa  Syria”  akaongeza Ban Ki Moon.

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kati ya nchi zilizoombwa kuchangia waangalizi hao wa amani na tayari imeshaonyesha nia  ya   kutekeleza ombi hilo.

 Akizungumzia hali ya kisiasa katika Bara la Afrika, Ban Ki Moon, ameelezea  kusikitishwa  kwake    na hali ya mambo ilivyo katika nchi za Guinnea Bisau,  Mali na kati ya Sudan na Sudan ya Kusini.

 Kuhusu mgogoro wa  nchi  za Sudan na Sudan ya Kusini, Ban Ki Moon amezitaka pande hizo  mbili kusitisha mapigano na vitendo vyote vinavyoashiria uvunjifu wa amani na kurejea katika  mkataba wa makubaliano ya amani. Na kwamba Umoja wa Mataifa  uko tayari kuzisaidia pande hizo mbili.

Kwa upande wa Guinea Bisau, Mkuu huyo wa UM ameeleza  masikitiko yake ya kuwapo kwa taarifa za ukiukwaji mkubwa wa haki za  binadamu na kuwaonya wale wote  wanaohusika na ukiukwaji wa haki za binadamu  kwamba watawajibishwa.

 Akahimiza kurejeshwa kwa utawala wa kikatiba na kwamba amemuagiza mwakilishi wake kushirikiana kwa karibu na Umoja wa Africa, ECOWAS na  Muungano wa nchi zinazozungumza Kireno katika kutatua mgogoro unaoendelea nchini humo.

 Na huko Mali, Katibu Mkuu  anasema  Umoja wa Mataifa  unashirikiana   kwa karibu na AU, ECOWAS na wadau wengine  ili nchi hiyo   ambayo nusu ya eneo lake  limetwaliwa na  wapiganaji wanaotaka kujitenga irejee katika hali ya amani na kuwa nchi moja.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu ametangaza kuundwa kwa jopo la watu mashuhuri ambalo litafanya marejeo ya masuala yote  yahusuyo maendeleo endelevu na hususani utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo  ya Millenia baada ya 2015  na kutoa mapendekezo ya nini kifanyike.

 Jopo hilo litakalokuwa na wajumbe kati ya 20 na 25 litaongozwa na  wenyeviti wenza watatu ambao ni   Marais Susilo Bambang Yudhoyono wa Indonesia,Ellen Johnson Sirleaf  wa Liberia  na  Bw. David Cameron,  Waziri Mkuu waUingereza

Akizungumzia kuhusu maandalizi ya Mkutano wa Kimataifa kuhusu maendeleo endelevu na mazingira maarufu kama RIO+20 unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao huko Rio de Jenairo nchini  Brazil. Katibu Mkuu amewahimiza wakuu wa nchi na serikali kuhudhuria mkutano huo muhimu na ameelezea kuridhishwa kwake na mwitiko wa wakuu  wa nchi na serikali.

Hata hivyo amewataka wadau wote wanaoshiriki katika kuandaa kabrasha  maalum la mkutano huo  kuonyesha utashi wa kisiasa  na kukamilisha majadiliano hayo ambayo yameongezewa muda wa wiki moja zaidi.

 Kumekuwa na mvutano mkubwa kati ya wadau wakuu, nchi za Ulaya kwa upande mmoja na kundi la nchi 77 na China kwa upande mmoja, kuhusu  masuala gani muhimu yanayotakiwa kuingizwa katika kabrasha hilo kwa kuzingatia vipaumbele vya  makundi hayo.

Vuta ni kuvute hiyo  imefanya majadiliano hayo kuwa magumu na kutokamilika kwa wakati na hivyo .  kupunguza  kasi ya  ukamilishaji wake ikiwa  ni  pamoja na kupunguza ukubwa wa kabrasha hilo ambalo lina kurasa zaidi ya 200. 

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages