UHURU WA VYOMBO VYA HABARIHUIMARISHA JAMII
PAO Dana L Banks |
Na Dana L. Banks
Habari au taarifa ni nguvu. Ni watu wachache sana wanaoweza kuishi,
kuiwajibisha serikali yao na kuwaelimisha watoto wao bila kuwepo kwa mtiririko
huru na thabiti wa habari. Raia wanahitaji taarifa sahihi na zenye kuaminika,
katika wakati sahihi. Vivyo hivyo kwa wafanyabiashara, masoko na hata serikali.
Watumiaji wa leo wa taarifa duniani kote
wanataka kupata tarifa wanazozihitaji katika sekunde kadhaa na wala si saa au
siku kadhaa. Kupanuka kwa njia mbalimbali za kijamii za kusambaza habari hasa
kwa kupitia teknolojia ya kisasa miongoni mwa watu na hata vyombo vya habari
vyenyewe, kunaashiria hamu kubwa ya umma kupata taarifa wakati wote. Jambo hili
limekuwa kama sehemu muhimu ya maisha ya kila siku. Watu wengi hawawezi
kuendesha shughuli zao za kila siku za kujikimu, kuwajibisha serikali zao au
kuelimisha watoto wao bila kuwa mtiririko huru na thabiti wa habari. Raia
wanahitaji taarifa sahihi na zenye kuaminika kwa wakati sahihi. Uhuru wa vyombo
vya habari huzifanya jamii pamoja na uchumi wake kuchangamka, kuimarika na
kustawi. Pale ambapo mtiririko huru wa habari umekatwa basi watu mmoja mmoja,
jamii na hata uchumi huathirika vibaya.
Karne
ya 21 imeleta mapinduzi makubwa ya mawasiliano na upashanaji habari. Mataifa na
watu ambao hapo awali walikuwa wametenganishwa na mipaka ya nchi zao,
wanaunganishwa moja kwa moja kwa kupitia mtandao wa mawasiliano wa Internet.
Aidha, ni wao ndio wanaoandika na kuueleza ulimwengu mzima kuhusu hali zao.
Kama tulivyoona katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, jamii ambazo
zinakandamiza waandishi na vyombo vya habari, haziwezi tena kufanya hivyo kwa
muda mrefu kabla ya raia hawajaweza kusambaza taarifa zao na kujenga mitandao
mikubwa ya upashanaji habari kwa kutumia njia za kisasa na thabiti za
upashanaji habari kwa kupitia mtandao (social media tools). Mtandao wa Internet umepanua majadiliano na
ubadilishanaji mawazo baina ya watu wa mataifa yote duniani. Kwa kiwango kikubwa
mtandao huu wa mawasiliano ulichangia kuangushwa kwa tawala kandamizi Kaskazini
mwa Afrika mwaka jana na ndio unawezesha raia katika nchi za Magharibi- ikiwemo
Marekani - kufuatilia utendaji wa serikali zao.
Uhuru
wa vyombo vya habari umejumuishwa katika Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu
la Mwaka 1948 linaloeleza kuwa "Kila mtu ana haki ya uhuru wa kujieleza na
kutoa maoni yake; haki hii inajumuisha uhuru wa kuwa na maoni bila kuingiliwa
na kutafuta, kupokea na kusambaza taarifa na maoni kwa kupitia njia yoyote ya
upashaji habari bila kujali mipaka ya nchi."
Uongozi
katika vyombo vya habari, iwe ni vile vya uchapishaji, utangazaji, mtandao wa
internet na mitandao ya kijamii ni muhimu katika maendeleo ya uhuru wa habari.
Hasa katika kuvifanya vyombo hivi kutokuwa vyombo vya kuisemea serikali bali
vyombo huru vya ufuatiliaji. Uongozi ndiyo unaotoa dira na misingi ya kimaadili
kwa uandishi wa habari na hivyo kujenga imani ya umma kwa vyombo hivyo.
Viongozi katika tasnia ya habari Tanzania ni wale wote wanaowafundisha,
kuwaongoza na kuwatia moyo waandishi wa habari wa kizazi kijacho kwa kupitia
njia mbalimbali za kuwaendeleza (professional development). Viongozi hawa wanaongoza
kwa mifano wakiwezesha vyombo vya habari kutekeleza wajibu wake wa kuimarisha
utawala wa kidemokrasia.
Kwa
upande mwingine, watu katika taifa lolote wanaponyimwa haki na uhuru wao wa
kupata habari husababisha kuenea kwa taarifa za upotoshaji, uvumi na dhana
potovu.
Marekani ina fahari kubwa kushirikiana na
vyombo vya habari vya Tanzania katika jitihada za kuwapatia Watanzania taarifa
sahihi na zinazotolewa kwa wakati na kuhimiza na kuimarisha demokrasia. Vyombo vya habari vinashiriki kikamilifu na
kuchangia katika kuweka kumbukumbu ya jitihada za kujenga demokrasia kwa kupitia
chaguzi za kidemokrasia, mjadala wa katiba mpya na hata harakati za kuongeza
ushiriki wa wanawake na vijana katika kufanya maamuzi. Kuendelea kuimarika kwa
uongozi na viwango vya utendaji katika vyombo vya habari kutawezesha kulinda
mafanikio yaliyofikiwa na kupatikana kwa mafanikio zaidi katika nyanja hizi na
nyinginezo.
Wakati siku ya Kimataifa ya Uhuru wa
Vyombo vya Habari ikikaribia, Marekani inapenda kusisitizia dhamira yake ya
dhati ya kuona kuwa waandishi huru wa habari wanafanya kazi yao bila hofu
yoyote. Aidha, tunawakumbuka na kuwaenzi waandishi wa habari, waandishi katika
mitandao (bloggers) na raia jasiri ambao wamejitolea maisha, afya na uhuru wao
ili watu wengine waweze kufahamu ukweli. Hali kadhalika, tunathamini na kuenzi
mchango wa vyombo huru vya habari katika kujenga demokrasia, uwazi na uthabiti
wa jamii.
Tunatambua kuwa, kama wakala wa
mabadiliko, viongozi wa vyombo vya habari wanachangia pia katika kuimarisha
utawala bora na maendeleo ya kiuchumi kwa kujenga jukwaa litakalowawezesha
wanajamii kutoa sauti yao na hivyo kuwezesha kujengwa na kukua kwa jamii iliyo
wazi zaidi. Mjadala wa kitaifa nchini kote Tanzania utaimarishwa pale ambapo
kila raia atasaidia kuiimarisha kada ya uandishi wa habari katika misingi ya
maadili na uhuru na hivyo kuiwezesha kuchangia zaidi katika maendeleo ya taifa.
Tunawapongeza waandishi wa habari wa Tanzania kwa kujitoa kwa dhati katika
kuitumikia kada hii, ambayo ni mojawapo kati ya kada muhimu na zinazoheshimika
duniani na tunaahidia kuendelea kuwapa ushirikiano wetu katika kufanikisha
jitihada na maono yao.
Mwisho, kama alivyosema Waziri wa Mambo
ya Nje wa Marekani Bibi. Hillary Clinton, ni lazima tukumbuke kuwa katika
maeneo mbalimbali duniani bado waandishi wa habari wanakabiliwa na vitendo vya unyanyasaji,
ukatili na wakati mwingine kuuawa. Leo
hii tunakumbuka kuwa uandishi wa habari ni wito wa mashujaa wa kila siku. Ni
lazima tuendelee kusimama kidete na kuwatetea wale wanaosimama na kupaza sauti
zao katika mazingira hatari wanapotekeleza wajibu wao wa kutafuta, kurekodi na
kufichua ukweli.
__________________________________________________________
Dana L. Banks ni Afisa wa Masuala ya Umma wa Ubalozi
wa Marekani katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269