Rais Dk. Jakaya Kikwete |
Rais wa Shirikisho la Vyama vya
Wafanyakazi Tanzania,
Ndugu Ayoub Omari Juma;
Waziri wa Kazi na Ajira -Mheshimiwa
Gaudensia Kabaka (MB);
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mheshimiwa Chiku
Galawa;
Waheshimiwa Mawaziri na Wabunge;
Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Dunia
(ILO) Kanda ya
Afrika Mashariki, Ndugu Alexio Musindo;
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya
Wafanyakazi,
Ndugu Nicholaus Mgaya;
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha
Waajiri Tanzania (ATE),
Dr. Aggrey Mlimuka;
Waheshimiwa Mabalozi;
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu,
Divisheni ya Kazi;
Wenyeviti na Makatibu wa Vyama vya
Wafanyakazi;
Viongozi wa Serikali;
Wawakilishi wa Vyama vya Siasa;
Ndugu Wafanyakazi na Wananchi;
Mabibi na Mabwana.
Shukrani
Nakushukuru Ndugu Ayoub Omari Juma na viongozi wenzako wa TUCTA
kwa fursa ya kuungana na wafanyakazi wenzangu kusherehekea sikukuu ya wafanyakazi
duniani mwaka huu. Naungana nanyi
kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, aliyetujaalia uhai na afya, na kutuwezesha
kukutana leo katika sherehe hizi, hapa Tanga.
Nawapongeza viongozi wa Mkoa wa Tanga wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa,
Mheshimiwa Chiku Galawa na wakazi wote wa Mkoa huu, kwa kukubali kuwa wenyeji
wa sherehe hizi na tunawashukuru kwa kutupokea vizuri. Aidha, nawapongeza sana kwa maandalizi mazuri
mliyoyafanya kwa kushirikiana na Chama cha Wafanyakazi wa Mashambani (TPAWU), TUCTA na Wizara ya Kazi na
Ajira. Aidha, kwa namna ya pekee nawapongeza
wafanyakazi na wananchi wote mliokusanyika hapa leo kuadhimisha siku hii muhimu
kwetu sote.
Pongezi kwa Wafanyakazi Bora
Ndugu Wananchi;
Kama ilivyo utamaduni wa sherehe hizi, leo tena nimetunuku tuzo kwa
wafanyakazi bora wa mwaka huu. Wenzetu
hawa wanastahili pongezi zetu sote kwa kufanya kazi kwa bidii, maarifa na
nidhamu. Nawomba waendelee
na moyo huo ili hata mwakani watunukiwe tena.
Nchi yetu itajengwa na watu kama hawa wanaojituma na kufanya kazi kwa
bidii, ufanisi na nidhamu. Kwa wale
ambao hawakupata safari hii, nawaomba wasikate tamaa bali wachukulie kupata kwa
wenzao leo kama chachu na motisha kwao kuongeza bidii zaidi kazini ili mwakani
nao watambuliwe na kuzawadiwa.
Kauli Mbiu ya Mwaka Huu
Ndugu Rais wa
TUCTA;
Ndugu
wafanyakazi;
Nimesikiliza risala yenu iliyowasilishwa
kwa ufasaha na Katibu Mkuu Ndugu Nicholaus Mgaya. Mambo mliyoyataja ni ya msingi kwa maslahi na
ustawi wa wafanyakazi na taifa letu. Risala
yenu nimeipenda kwa vile kwa kila suala mlilolizungumza mmetoa mapendekezo ya
jinsi ya kulitatua. Napenda kuwaahidi
kuwa tumesikia na tutayafanyia kazi.
Inawezekana tusifikie pale mnapopataka mara moja lakini tutafika muda si
mrefu.
Kauli Mbiu yenu inayosema, “Mshahara mdogo, kodi kubwa na mfumuko wa
bei, pigo kwa mfanyakazi’’ ni kauli muafaka kabisa. Inaeleza ukweli wa mambo ulivyo na kilio cha
wafanyakazi nchini. Narudia kuwahakikishieni kuwa mimi na wenzangu Serikalini tunazitambua
changamoto zinazowakabili wafanyakazi na kuzitafutia jawabu ndiyo shughuli
tuifanyayo kila siku. Ninyi na mimi ni mashahidi kwa namna gani Serikali yetu inavyojitahidi kushughulikia masuala yahusuyo
haki na maslahi ya wafanyakazi nchini.
Mambo mengi yamefanyika yanayoelezea uthabiti wa dhamira ya Serikali.
Ndugu Rais wa
TUCTA na Ndugu Wafanyakazi;
Miongoni mwa mambo ambayo yamefanyika ni
pamoja na: Kutungwa kwa Sera mpya ya malipo ya mishahara na motisha katika
utumishi wa umma; kuundwa kwa Bodi ya Mishahara katika utumishi wa umma; kutunga
Sheria na kuanzishwa kwa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi
ya Jamii; kupunguza kodi ya mapato kwenye mishahara; kuongeza kiwango cha chini
cha kutoza kodi ya mapato na kuweka utaratibu wa kupanga kima cha chini cha
mishahara katika sekta binafsi kwa kuzingatia tija ya kila sekta.
Ndugu
Wafanyakazi;
Naamini nanyi
mnajua kwamba wapo waajiri wengi wanaotulaumu kuwapa wafanyakazi haki na ulinzi
mkubwa dhidi ya waajiri, lakini hatutishiki wala kubabaika na hivyo hatutaacha
kupigania haki za wafanyakazi kama tufanyavyo kwa haki za waajiri. Nchi yetu ni miongoni mwa nchi za mwanzo
kutia saini Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Wafanyakazi wa Majumbani. Kwa miaka nenda rudi, ndugu zetu hawa wamekuwa
wakikandamizwa kupita kiasi. Kilio chao tumekisikia na tumeamua kuchukua hatua
za kuwakomboa.
Mshahara Mdogo
Ndugu Wafanyakazi;
Chama kinachounda Serikali hii kina historia ya kipekee na wafanyakazi
tangu enzi za kupigania uhuru na baada ya uhuru. Hatuwezi na wala hatuthubutu, hata
siku moja, kuwatelekeza wafanyakazi. Mtakumbuka kuwa katika hotuba yangu
ya Mei Mosi Mwaka jana (2011) pale Morogoro nilisema kuwa Serikali inatambua
kilio cha wafanyakazi wake kuhusu maslahi.
Niliwaelezea hatua mbalimbali ambazo Serikali imekuwa inazichukua
kuboresha maslahi ya wafanyakazi.
Niliwahakikishia wafanyakazi wa nchi yetu kwamba, hakuna upungufu wa
dhamira wala utashi wa kisiasa wa kuboresha maslahi yao kwa upande wangu
binafsi au wa wenzangu Serikalini. Uwezo
wa taifa letu kiuchumi ambao ndiyo huamua uwezo wa Serikali kifedha kukidhi
mahitaji ya wafanyakazi ndiyo mambo yanayoturudisha nyuma. Kwa sababu hiyo, hatuwezi kuboresha maslahi
ya wafanyakazi kwa kiwango tunachokitaka sote.
Pamoja na hayo katika miaka sita iliyopita, karibu kila mwaka tumechukua
hatua za kuboresha maslahi ya wafanyakazi.
Leo narudia kuahidi kuwa tutaendelea kufanya hivyo hata mwaka huu.
Ndugu
Wafanyakazi;
Katika miaka sita hii, tumeendeleza juhudi za
kukusanya mapato ya Serikali na tumefanikiwa sana. Mapato ya Serikali yameongezeka kutoka
wastani wa shilingi bilioni 125 kwa mwezi hadi shilingi bilioni 433 kwa
mwezi au kutoka jumla ya shilingi trilioni
1.9 mwaka 2005/6 hadi shilingi
trilioni 5.2 mwaka 2010/11. Mwaka
huu tunaelekea kufanikiwa zaidi. Katika kipindi cha Julai hadi Machi 2012 tumefikia
shilingi trilioni 4.8 ambayo ni sawa na asilimia
102 ya lengo la makusanyo kwa kipindi hicho.
Kwa sababu ya mafanikio hayo tumeweza kuongeza
kima cha chini cha mshahara Serikalini kutoka shilingi 65,000 kwa mwezi mwaka 2005 hadi shilingi 150,000 mwaka 2011. Kwa nyongeza hizo za mishahara, katika mwaka
huu wa fedha Serikali inatarajia kutumia jumla ya shilingi trilioni 3.2 kati
ya shilingi trilioni 6.7 za mapato ya ndani kwa ajili ya
mishahara. Hii ni asilimia 48 ya mapato hayo. Mishahara huchukua sehemu kubwa ya kiasi
hicho cha mapato ya Serikali, hilo ndilo jambo linalokuwa kikwazo katika
kuongeza mishahara na maslahi mengine ya wafanyakazi kama ambavyo sote
tungependa iwe. Vinginevyo, pesa kwa
ajili ya kutoa huduma muhimu kwa wananchi na kwa utekelezaji wa majukumu ya
kiutawala, kiuchumi, na ya ulinzi na usalama ya Serikali yatakwama. Kwa sababu ya
kutaka tuwe na uwiano mzuri, ndiyo maana tumekuwa tunaongeza mishahara kidogo
kidogo kila mwaka.
Wakati huo huo tumekuwa tunaongeza juhudi za
kuongeza mapato ambapo, kama nilivyokwishaeleza kwamba tunazidi kupata
mafanikio. Kwa ajili hiyo, tunaendelea
kutekeleza mikakati ya kupanua wigo wa walipa kodi na kuzidi kubana mianya
inayovujisha mapato ya Serikali. Aidha,
tunaangalia upya misamaha ya kodi. Mwaka
wa jana kwa mfano, misamaha ya kodi ya kisheria ilifikia shilingi trilioni 1.05.
Tumeamua kuzitazama upya sheria husika ili tuone wapi tunaweza kupata
nafuu na kuiongezea Serikali uwezo wa kutekeleza majukumu yake kwa wananchi pamoja
na wajibu wa msingi wa kuboresha maslahi ya wafanyakazi wake.
Mfumuko wa Bei
Ndugu Rais wa TUCTA na Ndugu Wafanyakazi;
Nakubaliana nanyi kwamba katika
hali hii ya ujira na maslahi yasiyotosheleza mahitaji, mfumuko wa bei unafanya
maisha ya wafanyakazi kuwa magumu.
Napenda kuwahakikishia kuwa tatizo la mfumuko wa bei tunalitambua na
kwamba Serikali imekuwa inachukua hatua mbalimbali kudhibiti mfumuko wa bei na
kupunguza makali yake. Bila ya juhudi
hiyo pengine hali ingekuwa mbaya zaidi.
Lazima niwe mkweli kwamba siyo
kazi rahisi hata kidogo. Kwa nini nasema
hivyo? Kinadharia mfumuko wa bei
unatokana na ujazi wa fedha kuwa mkubwa mno kuliko bidhaa. Mara nyingi Serikali kukopa sana kutoka
katika mabenki huwa ndicho kichocheo katika mazingira hayo. Hapa nchini hilo
silo tatizo na hata kama lingekuwa, ingekuwa rahisi kuudhibiti kwa kutumia sera
za fedha na bajeti. Kiini cha mfumuko wa
bei hapa kwetu ni kupanda kwa bei za nishati ya mafuta na umeme na kupanda kwa
bei za vyakula.
Bei ya mafuta imepanda huko tunakoyanunua na hivyo kusababisha gharama
ya kila shughuli inayotumia mafuta hapa kwetu kupanda. Kwa sababu hiyo, gharama za usafiri na uchukuzi, uzalishaji umeme,
uzalishaji viwandani na mashambani pamoja na mafuta ya matumizi ya majumbani na
kwingineko zimepanda. Hivyo basi, kuongeza
gharama ya maisha kwa watu wanaotumia bidhaa na huduma hizo.
Kwa upande wa umeme, juhudi zetu za kuongeza uzalishaji wa umeme
kutokana na gesi asilia utatupunguzia mzigo huo katika muda wa kati na mrefu
ujao. Kwa upande wa bei ya mafuta
hatuwezi kutabiri hali hii itakuwaje huko mbele ya safari hasa baada ya mwezi
Julai wakati vikwazo dhidi ya mafuta ya Iran vitakapoanza kutekelezwa kwa dhati
na nchi za Ulaya na Marekani.
Kwa upande wa bei ya chakula kuna sababu kadhaa. Ipo ile inayochangiwa na kupanda kwa bei ya
mafuta, hivyo kupandisha gharama za uzalishaji na uchukuzi wa mazao kuyafikisha
kwenye masoko. Lakini katika miaka ya
hivi karibuni mvua kutokunyesha kwa kiwango cha kuridhisha na kwa mtawanyiko
usiokuwa mzuri, kumesababisha kupungua kwa uzalishaji wa mazao na kusababisha upungufu
wa chakula.
Ndugu
Wafanyakazi;
Kana kwamba hilo halitoshi, nchi jirani nazo kutegemea nchi yetu kupata
chakula chao kumelifanya tatizo kuwa kubwa zaidi na kusababisha bei za mahindi,
mchele, sukari na maharage kupanda sana.
Mwaka wa jana niliagiza Wakala wa Chakula wa Serikali (NFRA) waanze utaratibu wa
kuuza chakula mijini hasa nyakati za upungufu wa chakula kinacholetwa katika
masoko kutoka vijijini. Lengo langu katika
kufanya uamuzi ule ni kutaka kusaidia kupunguza makali ya bei ya vyakula mijini
na hivyo kuwapa nafuu wakazi wa mijini na hasa wafanyakazi. NFRA
wameanza kuuza chakula mijini lakini bado mpango huu haujafanikiwa vya
kutosha. Nimeagiza wabaini upungufu uliopo
na kuurekebisha ili uwe ukombozi kwa wakazi wa mijini.
Kwa upande wa
sukari na mchele tuliwaruhusu wafanyabiashara binafsi kuagiza bidhaa hiyo toka
nje bila kulipa ushuru wa forodha (Surchage).
Waliopewa vibali wamekuwa wanaleta sukari lakini sijaridhishwa na kasi
ya uagizaji. Naambiwa wapo watu
walioomba vibali ambao uwezo wao ulikuwa mdogo na hivyo kuwanyima Watanzania
fursa ya kunufaika na vibali hivyo na nafuu ya kodi. Nimeagiza Wizara husika zifanye ukaguzi wa
utekelezaji wa waliopewa zabuni ili wale walioshindwa wanyang’anywe na
kupewa watu wengine wenye uwezo.
Pamoja na hatua hizo tumefanya uamuzi wa
makusudi wa kuongeza uzalishaji wa mpunga na sukari nchini. Kwa upande wa sukari tayari hekta 80,000 zimeshatambuliwa kwa ajili
ya kulima mashamba na kujenga viwanda vya kuzalisha sukari. Kazi ya kutambua maeneo zaidi katika Bonde la
Rufiji na mabonde mengine nchini inaendelea.
Aidha, juhudi zinaendelea za kutafuta wawekezaji wa kutoka ndani na nje
kuwekeza katika uzalishaji wa sukari. Kwa
upande wa mchele, mikakati inaendelea ya kupanua na kuboresha uzalishaji wa
mpunga katika mabonde kadhaa hapa nchini.
Kwa kuanzia nguvu zetu tumezielekeza Wilaya ya Ulanga na Kilombero.
Kodi Kubwa
Ndugu wafanyakazi;
Kilio chenu cha
kupunguziwa kiwango cha kodi ya mapato tumekipokea kwa uzito unaostahili. Jambo
hili si geni. Mlishalileta siku za nyuma na tumechukua hatua na tunaendelea
kuchukua hatua. Mwaka 2007 tulipunguza PAYE kutoka asilimia
18.5 hadi asilimia 15 kwa lengo la kuwapunguzia mzigo wafanyakazi wa kipato cha
chini. Aidha mwaka 2010/11 tulipunguza
kodi hiyo kutoka asilimia 15 hadi 14,
sambamba na kuongeza kima cha chini cha mshahara kisichokatwa kodi kutoka shilingi 100,000 hadi kufikia shilingi 135,000. Serikali
itaendelea kupunguza kiwango cha kodi hatua kwa hatua ili kuwapunguzia
wafanyakazi mzigo wa kodi.
Vilevile tutaendelea
kubuni njia mbalimbali za kuwafikia watu wengi zaidi waliopo nje ya mfumo wa kulipa
kodi ili walipe na kuwapunguzia mzigo wa kodi kwa wafanyakazi. Naamini mpango wa kutoa vitambulisho vya taifa
utakapotekelezwa kwa ukamilifu, utasaidia kutambua walipa kodi wengi ambao hivi
sasa hawajajulikana.
Ukosefu wa Ajira
Ndugu wafanyakazi;
Nchi yetu, kama zilivyo nchi nyingi duniani inakabiliwa
na tatizo kubwa la ajira hasa kwa vijana.
Ukosefu wa ajira hapa nchini umefikia karibu asilimia 12 kwa mujibu wa sensa ya kazi ya mwaka 2006. Taarifa ya Utafiti ya Shirika la Kazi la Kimataifa (ILO) inaonyesha kuwa mnamo mwaka 2011 watu
wapatao milioni 200 hawakuwa na
ajira duniani, na inategemewa kwamba
idadi hiyo itaongezeka na kufikia watu milioni 204 mwaka huu (2012)
na ifikapo mwaka 2013, idadi hiyo itafikia watu milioni
209.
Kwa kutambua umuhimu wa kuchukua hatua thabiti za kukuza
ajira ili kupunguza tatizo hilo, Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2005 ya CCM iliipa
Serikali yake lengo la kuzalisha ajira milioni
moja. Bahati nzuri lengo hilo
liliweza kufikiwa na kuvukwa. Ajira milioni 1.2 zilizalishwa. Katika kipindi hiki Serikali imejipanga
kuzalisha ajira maradufu ya zile za kipindi cha kwanza.
Kwa ajili hiyo hatua mbalimbali
zimeendelea kuchukuliwa ili kuzalisha ajira mpya nyingi zaidi. Niruhusuni nitaje baadhi tu ya hatua
zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa:
1. Tumefanya maboresho katika kuendeleza rasilimali
watu hasa katika nyanja za elimu, mafunzo na ujuzi ili kuwawezesha wahitimu
wake wawe na sifa za kuajiriwa ndani na nje ya nchi na uwezo wa kujiajiri wenyewe. Tumeelekeza kuwa mitaala ya shule na vyuo
izingatie kutoa elimu na mafunzo yanayotakiwa na soko la ajira. Kadhalika vijana wapate elimu na mafunzo
yatakayowawezesha kujiajiri. Kwa ajili
hiyo tumesisitiza somo la ujasiriamali kufundishwa shuleni na vyuoni. Hii itawawezesha vijana kujua namna ya
kuanzisha na kuendesha shughuli za uzalishaji na huduma zitakazowapatia mapato.
2. Tumeanza kuchukua
hatua za kutekeleza mkakati maalum wa kuwatafutia Watanzania ajira nchi za
nje. Hatua hizo zimewezesha vijana wa
Kitanzania 1,327 kupata ajira katika
nchi za Oman, Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu kupitia Wizara ya Kazi na
Ajira katika mwaka 2011/12. Lengo letu
ni kuona vijana wengi zaidi wanapata ajira katika nchi hizo na nyinginezo nyingi
duniani kama walivyo majirani zetu.
3. Kwa nia ya kuwasaidia vijana kupata ajira hapa
nchini, tumeamua kuunda Kamati Maalum za
kukuza ajira katika kila Wizara na Mikoa.
Kwa kuanzia Wizara sita na Halmashauri
12 katika mikoa ya Lindi na Mtwara zimeunda
Kamati Maalum na madawati ya kukuza ajira. Wizara hizo ni pamoja na Wizara ya
Mambo ya Ndani, Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, Wizara ya Kilimo, Wizara
ya Fedha, Wizara ya Ujenzi pamoja na TAMISEMI.
4. Tumeendelea
kuwawezesha wajasiriamali wadogo wa Tanzania kushiriki katika maonyesho ya kila
mwaka ya nguvu kazi/jua kali ya nchi za
Afrika Mashariki. Lengo letu kuu ni kuwapatia wajasiriamali wetu wadogo (ambao ndio wengi) fursa ya kujifunza, kupata soko na kutumia fursa hizo kukuza
shughuli zao wazifanyazo. Kwa kufanya
hivyo, Watanzania watanufika na fursa za itifaki ya soko la pamoja la Afrika
Mashariki. Wastani wa wajasiriamali 106
wamekuwa wakiwezeshwa kushiriki maonesho husika (Nguvu Kazi/Jua kali) kila
mwaka kwa kipindi cha miaka 13 sasa.
5. Kupitia mradi wa
kujenga usawa wa jinsia na ajira bora kwa wanawake, hadi kufikia mwezi April
2012 kiasi cha shilingi bilioni 1.23 kimekopeshwa kwa wanawake. Wanawake wapatao 4,097 wamenufaika kupitia
SACCOS za wanawake katika wilaya za Kinondoni, Ilala, Temeke na Tukuyu. Baada
ya mafanikio yaliyopatikana katika Wilaya hizo, tunajipanga kueneza mpango huu
nchi nzima.
6. Mtakumbuka kuwa mwaka
2006 tulianzisha Mfuko wa Mikopo kwa Wajasiriamali Wadogo. Tulitenga shilingi bilioni moja kwa kila
mikoa ya Tanzania Bara na shilingi
milioni 200 kwa Mjini Magharibi na shilingi
milioni 100 kwa mikoa mingine minne
ya Unguja na Pemba. Kwa upande wa
Tanzania Bara, hadi kufikia mwezi Desemba, 2010, ilitolewa mikopo yenye thamani
ya shilingi bilioni 47.3 kwa wajasiriamali 73,496, SACCOS
192 na vikundi vya kiuchumi 86. Wote hao wamejiajiri na kuwawezesha watu
kadhaa kupata ajira. Tumekamilisha
tathmini ya mpango huu na makakati unaandaliwa wa kuuendeleza. Shabaha yetu ni kuongeza fedha na kuboresha
mfumo wa ukopeshaji, utafutaji na usimamizi wa wakopaji.
7. Serikali
imeendelea kuwekeza katika shughuli za ujenzi wa majengo na miundombinu, shughuli
ambazo zimekuwa zikitoa ajira nyingi kwa wananchi. Katika miaka ya 2009, 2010
na 2011 peke yake shughuli hizi zimepanuka
sana. Jumla ya miradi mikubwa 8,870 yenye thamani ya shilingi trilioni 7.6 ilisajiliwa na
Bodi ya Wakandarasi. Miradi hii imezalisha
ajira 59,743 kati ya mwaka 2010 na
2012 kwa wahandisi na wataalamu wa fani mbali mbali, mafundi, vibarua, wenye
magari ya uchukuzi, madereva na waendesha mitambo, mama lishe, wauzaji wa vifaa
vya ujenzi, na watoa huduma za ujenzi.
Uwekezaji uliofanywa
katika sekta ya ujenzi sio tu umeongeza ajira bali pia umeongeza mzunguko wa
fedha nchini. Umesaidia kupunguza
umaskini. Tutaendelea kuwekeza zaidi
katika sekta hii ya ujenzi na sekta nyinginezo zenye kuzalisha ajira kwa wingi.
8. Tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo Serikali
ilikuwa mwajiri mkubwa siku hizi ni sekta binafsi. Ni kwa sababu hiyo basi, Serikali inahimiza kukuza
uwekezaji kutoka ndani na nje, na kuendeleza sekta binafsi ya wazawa nchini. Tumeendelea kuvutia uwekezaji katika Sekta ya
Viwanda hususan kwenye Maeneo Maalum ya Kiuchumi (SEZ) na Maeneo Maalum ya
Mauzo Nje (EPZ). Mwaka wa jana peke
yake, jumla ya miradi mipya 17 yenye
thamani ya dola za Kimarekani 112
ilipatikana na kutoa ajira 8,059 kwa
wananchi. Matarajio yetu kwa mwaka huu
ni kupata miradi mipya 23
itakayozalisha ajira 14,500.
Maboresho katika
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii
Ndugu wafanyakazi;
Serikali inatoa umuhimu wa juu katika kuboresha maslahi
ya wafanyakazi wakati wakiwa kazini na baada ya kustaafu. Sera na Sheria za Mifuko mbalimbali ya
Hifadhi ya Jamii zina shabaha ya kuhakikisha kuwa mfanyakazi anapostaafu
anaweza kuishi maisha mazuri. Tumetunga Sheria
na kuanzisha Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii
(SSRA). Madhumuni ya mamlaka hiyo ni kuhakikisha
kuwa, afya ya mifuko ni nzuri na inaendelea kustawi. Mamlaka hiyo imeanza kazi na kwa kushirikiana
na Benki Kuu ya Tanzania ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha tathmini ya
mifuko yote ya hifadhi ya jamii (Actuarial Valuation). Lengo la zoezi hilo ni kubaini maeneo ya kuimarisha na kuondoa
tofauti za ukokotoaji wa malipo baina ya
mifuko. Zoezi hili litakapokamilika litawasaidia sana wafanyakazi kujiandaa
kustaafu na pia kupunguza makali ya maisha kwa wafanyakazi wanaostaafu, ili
wastaafu kwa heshima.
Tija Kazini
Ndugu Wafanyakazi;
Pamoja na jitihada zote za kuongeza
ajira, naomba tuendelee kukumbushana umuhimu wa wafanyakazi nchini kufanya kazi
kwa bidii na maarifa ili kukuza tija kazini.
Vyama vya wafanyakazi vinao wajibu mkubwa kwa hili kama walionao wa
kutetea haki za wafanyakazi. Hakuna haki
isiyokuwa na wajibu. Nawaomba
wafanyakazi kutambua wajibu wa kufanya kazi kwa bidii, maarifa, uaminifu na
uadilifu. Bado minong’ono ya Watanzania kutokufanya
kazi kwa bidii na kutokuwa waaminifu ipo.
Hali hii inawafanya baadhi ya wawekezaji wa kutoka nje na ndani
kufikiria kuajiri wageni.
Nalirudia kulisemea jambo hili kwani si jema
na kwamba tabia hii ikiendelea itafanya mazingira ya ajira kwa Watanzania
kutokuwa mazuri. Nawasihi ndugu zangu
tubadilike, ili watu duniani wapende kuajiri Watanzania. Inawezekana.
Tunaweza kabisa kufanya kazi kwa bidii, maarifa, nidhamu, uaminifu na
uadilifu. Haya shime tufanye hivyo na
tuonekane tunafanya hivyo.
Ndugu Wananchi;
Kabla ya kumaliza hotuba yangu napenda
kuzungumzia masuala matatu muhimu kwa taifa.
Mawili nimekwishayazungumzia siku za nyuma na moja nalizungumza kwa mara
ya kwanza. Jambo la kwanza ni Sensa ya
Watu na Makazi itakayofanyika tarehe 26 Agosti, 2012. Duniani kote, nchi hufanya sensa kila baada
ya muda wa miaka fulani; wengi hufanya kila baada ya miaka 10. Sababu na umuhimu wa sensa ni kuisaidia
Serikali kupanga mikakati na mipango ya maendeleo ya nchi na maeneo kwa
uhakika. Kwa kujua idadi ya watu na
mtawanyiko wao ni rahisi kwa Serikali kupanga nini cha kufanya, wapi na namna
gani. Nawasihi wafanyakazi na Watanzania
wote kwa jumla mjitokeze kuhesabiwa siku hiyo.
Si busara kukosa. Isaidie
Serikali yako kupanga mipango ya uhakika kwa kuhesabiwa.
Katiba
Ndugu
Wafanyakazi, Ndugu Wananchi;
Jambo la pili ambalo ningependa kuliongelea siku ya
leo ni Mchakato wa kupata Katiba Mpya ya nchi yetu. Wafanyakazi ni sehemu
muhimu sana katika mchakato wa kupata Katiba mpya. Kama mjuavyo Tume ya Kukusanya Maoni ya
Wananchi imeshaundwa na inaanza kazi zake rasmi siku ya leo. Baada ya muda si mrefu Tume itaelekeza
utaratibu wa wananchi kutoa maoni.
Narudia kuwaomba wafanyakazi na wananchi wote kwa jumla mjitokeze kutoa
maoni yenu kuhusu Katiba ya nchi yetu.
Ni fursa nzuri ya kutumia haki yenu ya kikatiba kutoa maoni yenu. Katiba ni kitu muhimu katika maisha na ustawi
wa taifa na watu wake. Tafadhali
jitokezeni msiache fursa hii ikapita halafu ukaja kulalamikia mambo yaliyomo
katika Katiba mpya. Mwaka jana pale
Morogoro mliomba kupata mwakilishi kwenye Tume ya Kukusanya Maoni ya Wananchi
kuhusu Katiba. Hongereni kwa kupata uwakilishi katika Tume hiyo kupitia
kwa Ndugu Yahaya Msulwa, Katibu Mkuu wa Chama Walimu.
Sakata la
Bungeni
Ndugu
Wafanyakazi;
Ndugu Wananchi;
Jambo la tatu
ni mambo yaliyojitokeza katika Bunge lililopita. Katika Mkutano uliopita wa Bunge, taarifa ya
mwaka wa fedha wa 2009/10 ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali pamoja
na taarifa za Kamati za Kudumu za Bunge ziliwasilishwa na kujadiliwa. Mjadala wa taarifa hizo ndani ya Bunge na
katika Kamati ya Wabunge wa Chama cha Mapinduzi, ulikuwa mkali na mapendekezo
kadhaa yalitolewa juu nini kifanyike kurekebisha upungufu uliobainika. Aidha, kumetolewa rai kwa baadhi ya Mawaziri
kuwajibika au wawajibishwe. Katika jamii nako kumekuwepo na mjadala
kuhusu taarifa hizo na yaliyotokea Bungeni.
Kama ilivyo kawaida, kumekuwepo na maneno mengi na mengine ya uongo na
opotoshaji kuhusu msimamo wangu na maoni yangu juu ya sakata la Bungeni. Napenda kuwahakikishia kuwa sikukasirishwa wala
kufadhaishwa na mjadala wa Bungeni kuhusu taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali. Kinyume chake
nimefurahi kwamba taarifa hiyo sasa inapewa uzito unaostahili na kwamba inajadiliwa
kwa uwazi. Hayo ndiyo matakwa yangu. Narudia kuwapongeza Wabunge kwa jinsi walivyoijadili
taarifa hiyo na mapendekezo yao. Tumejipanga
vizuri kutekeleza mapendekezo yao.
Ndugu
Wafanyakazi na Ndugu Wananchi;
Wanadamu husahau upesi. Mimi ndiye niliyefanya
uamuzi kwamba taarifa za kila mwaka za ukaguzi wa hesabu za Serikali Kuu,
Serikali za Mitaa na Mashirika ya Umma ziwekwe wazi kwa wananchi kuzisoma na
Bungeni zitengewe muda wa kutosha wa kujadiliwa. Kabla ya hapo taarifa hizi zilikuwa hazisikiki,
hazionekani na wala hazizungumzwi. Hata Bungeni
taarifa hizi zilikuwa ama hazizungumzwi au hazizungumzwi vya kutosha. Aghalabu huwekwa mezani tu na kama kuna mjadala basi huwa ni wa muda mfupi
sana kwani kwa kawaida taarifa hizo hutolewa siku ya mwisho kabla ya hotuba ya
kufunga Bunge. Kutokana na ushawishi
wangu taarifa hiyo inapewa nafasi ya kutosha ya kujadiliwa.
Ndugu Wananchi;
Kabla ya kuwa Rais mwaka 2005, (wakati wa kampeni) na
baada ya kuwa Rais, (katika hotuba yangu ya kuzindua Bunge la Tisa, 30 Desemba,
2005) nilielezea dhamira yangu ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kusisitiza
nidhamu ya matumizi. Nafurahi kwamba kwa
yote mawili mafanikio yanaonekana.
Tumepata mafanikio makubwa kwa upande wa mapato ya Serikali kama
nilivyokwishaeleza huko nyuma.
Kwa upande wa nidhamu ya matumizi nako tunaanza kuona
mwanga wa matumaini ingawaje bado tunayo kazi kubwa ya kufanya. Katika mikakati yangu ya kufikia lengo hilo
niliamua kwanza tuelekeze nguvu zetu katika kuimarisha Ofisi ya Taifa ya
Ukaguzi. Hiki ndicho chombo kikuu cha
kusimamia na kushauri kuhusu nidhamu ya matumizi ya fedha na mali za umma. Niliona bila ya kufanya hivyo kazi hii
itakuwa ngumu sana au haitawezekana
kabisa. Bila ya wao hutajua hali ikoje
na hivyo huwezi kujua wapi pa kuanzia na nini kifanyike.
Baada ya kumteua Ndugu Ludovick Utuoh kuwa Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Septemba,
2006 nilimtaka jambo moja kubwa, nalo ni kuimarisha Ofisi ya Taifa ya
Ukaguzi ili tuweze kupambana na utovu wa nidhamu, wizi na ubadhilifu wa fedha
na mali za umma. Lengo langu ni kutaka
fedha na mali hizo zitumike kwa manufaa ya umma badala ya kunenepesha matumbo
ya viongozi na watumishi wa Serikali wasiokuwa waaminifu na watovu wa
uadilifu. Nilimuahidi ushirikiano na
msaada wangu kwa yale atakayotaka Serikali ifanye kwa ajili hiyo.
Ndugu Utuoh alituletea Serikalini mahitaji yake na
tumechukua hatua za dhati ambazo zimesaidia kuimarisha Ofisi ya Taifa ya
Ukaguzi. Tumeiboresha Sheria ya Ukaguzi
na kuiongezea mamlaka na kuihakikishia uhuru katika utekelezaji wa majukumu
yake. Tumeiwezesha ofisi ya Taifa ya
Ukaguzi. Tumeiongeza bajeti yake na hivyo
wameajiri watumishi wengi wenye ujuzi wa kazi za ofisi hiyo. Wameongeza vitendea kazi kama vile, majengo ya
ofisi Makao Makuu na mikoani, magari, computer n.k. Kazi ya kujenga na kuimarisha ofisi ya Taifa
ya Ukaguzi tunaendelea nayo na inatupa moyo wa kufanya hivyo kwani matokeo yake
kwa hapa tulipofikia ni mazuri.
Ndugu
Wananchi ;
Baada ya kupokea taarifa yake ya kwanza ya ukaguzi,
Machi, 2007, kusikiliza ufafanuzi wake na baada ya kuisoma na kuielewa
nilitambua umuhimu na uharaka wa kuanza kuchukua hatua za kurekebisha
mambo. Niliona tuanze na wahusika
wanaozungumzwa katika taarifa hiyo.
Nilitaka wasikie yale yanayosemwa juu yao kuhusu walivyotumia fedha na
mali za umma. Kwa sababu hiyo, nilimtaka
Ndugu Utuoh azungumze na Baraza la Mawaziri na Watendaji Wakuu wa
Serikali. Tulifanya hivyo Dodoma. Baadaye niliwataka wazungumze na Wenyeviti,
Wakurugenzi na Waweka Hazina wa Halmashauri za Wilaya na Miji. Niliitisha mkutano huo tarehe 28 Aprili, 2007
pale Ubungo Plaza.
Baada ya mikutano ya Ndugu Utuoh na Mawaziri na
Watendaji wa Serikali Kuu na viongozi wa Halmashauri za Wilaya na Miji nchini,
nilitoa maelekezo na maagizo kadhaa juu ya mambo ya kufanya kuimarisha nidhamu
ya matumizi ya fedha na mali za umma.
Mosi, niliwataka viongozi na watendaji wakuu wa Wizara, Idara
zinazojitegemea, Halmashauri za Wilaya na Miji na Mashirika ya Umma wazipe
uzito unaostahili taarifa za ukaguzi kuhusu taasisi zao wanazoziongoza. Nilitaka wazisome na kuzijadili kisha
wachukua hatua ya kurekebisha kasoro zilizoonekana.
Pili, niliagiza ziundwe Kamati Maalum za kuongoza na
kufuatilia mwenendo wa mapato na matumizi ya fedha katika kila taasisi. Niliagiza kuwa Mawaziri waongoze Kamati za
Wizara zao na wajumbe wake wawajumuishe Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu
Mkuu, Mhasibu Mkuu na Wakurugenzi au Makamishna waliopo Wizarani. Katika Halmashauri za Wilaya na Miji, Wenyeviti wa Halmashauri wataongoza kamati hizo
na wajumbe wake ni Mkurugenzi Mtendaji, Mweka Hazina na Wakuu wa Idara. Kamati
hizi pia zitajadili taarifa ya miezi mitatu ya Mhasibu Mkuu kabla haijapelekwa
ngazi za juu.
Ndugu
Wananchi ;
Jambo la tatu nililoagiza lifanywe ni kuwa, wahasibu
wenye elimu na ujuzi stahiki wa mahesabu waajiriwe mapema iwezekanavyo na kupangiwa
kufanya kazi katika Halmashauri zote nchini.
Moja ya mambo ambayo Mkaguzi Mkuu alibainisha kwetu ni kuwa Halmashauri
zina uhaba mkubwa wa wahasibu wenye ujuzi, jambo ambalo linachangia mambo kuwa
mabaya. Kutokana na maagizo yangu hayo,
wahasibu 795 waliajiriwa na kila
Halmashauri ilipatiwa wahasibu wasiopungua watatu.
Ndugu
Wafanyakazi na Ndugu Wananchi ;
Baada ya kuimarisha ukaguzi wa hesabu
za Serikali na Mashirika ya Umma, kuundwa na kufanya kazi Kamati Maalum na kuajiri
na kusambaza Wahasibu wenye sifa, hali imeanza kubadilika na kuboreka. Hivi sasa Wizara na Halmashauri zinazopata
hati zinazoridhisha (safi) zimeongezeka na zinazopata hati zisizoridhisha (chafu)
zimepungua. Kwa mfano, mwaka 2009/10
taarifa ilikuwa kama ifuatavyo: Halmashauri zenye hati safi zilikuwa 66 hati zenye mashaka (qualified) 64 na hati chafu 4. Mwaka 2010/11 hali
ilikuwa kama ifuatavyo: Hati zinazoridhisha 72, zenye mashaka 56 na zisizoridhisha
5. Hali kadhalika kwa upande wa Wizara nako
kuna maendeleo ya kutia moyo. Taarifa ya
mwaka 2009/10 inaonesha kuwa Wizara zilizopata hati zinazoridhisha 42, zenye mashaka 13 na zisizoridhisha 1. Taarifa ya Ukaguzi ya mwaka 2010/11 inaonesha
kuna hati zinazoridhisha 50, zenye
mashaka 10 na zisizoridhisha 0.
Ndugu
Wafanyakazi na Ndugu Wananchi;
Kuna
mambo manne mapya kuhusu ukaguzi wa hesabu za Serikali ambayo niliagiza
yafanyike na sasa yanafanyika. Kwanza,
kwamba, pamoja na ukaguzi wa vitabu vya hesabu vya taasisi, ufanyike ukaguzi wa
thamani ya fedha (value for money) kwa
yale yaliyoandikwa kuwa yamefanywa. Kazi
hiyo sasa imeanza kufanyika, ndiyo maana hata Wahandisi ni wakaguzi katika
Ofisi ya Taifa ya Mkaguzi. Katika baadhi
ya maeneo au miradi, ukaguzi ulipofanyika mambo ya udanganyifu yamegundulika na
wahusika kuchukuliwa hatua.
Jambo la pili ni kwamba, nilitaka CAG kutoa taarifa
kwa vyombo vya kisheria pale atakapoona dalili ya wizi kufanyika. Kabla ya hapo, wajibu wa CAG ni kutoa taarifa
kwa Rais ambaye nae huagiza Mawaziri husika kuziwasilisha taarifa hizo
Bungeni. Hata kama amebaini wizi au
ubadhilifu ni juu ya mamlaka husika.
Niliona huu ni upungufu, tukarekebisha Sheria na sasa inafanyika.
Jambo la tatu ni ukaguzi wa uchunguzi (forensic audit)
ambao shabaha yake ni kushauri taasisi kuhusu kasoro zilizopo au maeneo ya
udhaifu ambayo yanahitaji kuimarishwa.
Ukaguzi huo umeshafanywa Customs, NHIF na Halmashauri ya Misungwi kwa
mfano.
Jambo la nne ni kuwa na Wakaguzi wa Ndani katika kila
Wizara na Idara zinazojitegemea ambao wanawajibika moja kwa moja kwa Mkaguzi
Mkuu wa Ndani wa Serikali. Huko nyuma
Wakaguzi wa Ndani walikuwa wanawajibika kwa Makatibu Wakuu wa Wizara na Wakuu
wa Taasisi, jambo ambalo nililiona lingewafanya Maafisa hao kukosa uhuru wa
kutosha kutekelekeza majukumu yao.
Ndugu
Wafanyakazi na Ndugu Wananchi;
Nimeyaeleza haya yote kwa kirefu mjue tulikotoka,
tulipo sasa na huko mbele tuendako. Nataka
muelewe na kutambua jitihada tulizozifanya kuimarisha nidhamu ya matumizi ya
fedha na mali za umma. Lakini tumechukua
hatua, tunaendelea na tutaendelea kuchukua hatua. Mafanikio yanaanza kupatikana lakini si ya
kiwango cha kutufanya tufurahi sana. Bado
tuna safari ndefu na kazi kubwa ya kufanya mbele yetu kwa sababu tumeanza katika
hali ya chini sana. Mimi napata faraja kwamba
muelekeo wetu ni mzuri na naamini tutafika pale tunapopataka, yaani “Mapato ya Serikali yataongezeka na fedha zinatumika kuwanufaisha
walengwa“.
Hitimisho
Ndugu Wafanyakazi;
Nimeongea mengi.
Ujumbe wangu mkubwa kwenu wafanyakazi wenzangu ni kuwa Serikali inatambua mazingira ya wafanyakazi na
tuko tayari kuchukua hatua ya kuboresha hali hiyo kwa kadri ya uwezo wetu
uliopo. Hatuwezi kusubiri uwezo uwe mkubwa.
Tutaendelea kugawa kilichopo kupunguza makali. Tutaendeleza juhudi za kudhibiti
mfumuko wa bei pamoja na changamoto zilizopo.
Hatutasita kufanya yale yaliyopo kwenye uwezo wetu.
Naomba nimalizie kwa kuwashukuru tena kwa kunialika kuja
kujumuika nanyi katika siku hii adhimu.
Ni heshima kubwa kwangu.
Ahsanteni sana. Nawatakia sikukuu
njema.
Asanteni kwa Kunisikiliza.
Mungu Ibariki
Afrika!
Mungu Ibariki
Tanzania!
Hotuba Safi,Kama Kawaida hii nayo imetoa Darasa kwa hoja nyingi na Hasa ya SAKATA BUNGENI kumbe ni hoja yake Mhe. Rais na Chama Chake? nimeipenda hiyo. Katika ZAMA hizi kumezuka wimbi kubwa la UPOKAJI wa agenda
ReplyDeleteJK endeleza mapambano TUNAKUAMINI
kwa kizazi kile na enzi zile CHAMA kiliwadhibiti wakengeufu wa IMANI ya chama ambao leo mnawaita MAFISADI kwa mbinu mbalimbali zilizofaa kwa zama zile Mfano AZIMIO LA ARUSHA, WAHUJUMU UCHUMI, FAGIO LA CHUMA nk.
ReplyDeleteKizazi hiki cha DOT COM cha KUKOPI NA KUPESTI cha ujanjaujanja na DIGIRII kibao WAKENGEUFU HAO WA IMANI YA CHAMA ni lazima washughulikiwe kwa MPANGO MKAKATI MAALUM kama ambavyo Mhe. Rais anaenda nao. PONGEZI KWAKO MHE.RAIS