Ngorongoro Heroes |
Katika hali inayoonyesha Sudan kuwa na kiu ya kuibuka na ushindi, imeamua watazamaji kuingia bure katika mechi ya timu ya soka ya Tanzania ya Vijana chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes na timu yao ya vijana, itakayopigwa Jumamosi hii, kuanzia saa 2 usiku kwenye Uwanja wa Khartoum.
Ngongoro Heroes waliwasili mjini Khatoum, jana saa 4.00 usiku, tofauti na muda waliotarajiwa wa saa 2.10 usiku, lakini haikuwezekana kutokana na ndege kuchelewa kuondoka kwa saa moja na nusu kutokana na hali ya hewa kuwa mbaya katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kutokana na mvua kubwa.
Baada ya kuwasili Taka Hotel ambapo imefikia, Ngorongoro Heroes ilifanya mazoezi ya saa moja kuanzia saa 4.30 usiku kwenye Uwanja wa Khartoum ambao ndiyo utakaotumika katika mechi dhidi ya Sudan.
Katika mechi ya awali Ngorongoro Heroes ilishinda mchezo wa kwanza mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Hoteli ya Taka ndipo pia timu ya El Merreikh ya hapa Sudan imeweka kambi yake kujiandaa kwa mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC). El Merreikh ililala mabao 2-0 katika mechi ya kwanza iliyochezwa jijini Lubumbashi.
Kwa mujibu wa kocha Kim Poulsen, wachezaji wote wako katika hali nzuri na kikosi kitakachoanza kwenye mechi hiyo kitajulikana kesho (Ijumaa) baada ya mazoezi ya mwisho yatakayofanyika saa 2 usiku kwenye Uwanja wa Khartoum.
Wachezaji walioko kwenye kikosi cha Ngorongoro Heroes ni Aishi Manula, Ramadhan Singano, Hassan Dilunga, Frank Damayo, Frank Sekule, Issa Rashid, Hassan Ramadhan, Saleh Malande, Said Zege, Emily Mugeta, Jerome Lambele, Samir Ruhava, Simon Msuva, Thomas Ulimwengu, Atupele Green, Dizana Yarouk, Jamal Mroki na nahodha Omega Seme.
Mwamuzi Aden Abdi Djamal wa Djibouti ndiye atakayechezesha mechi hiyo. Djamal atasaidiwa na Wadjibouti wenzake Egueh Yacin Hassan, Bogoreh Salime Fahan na Aden Ali Farah. Waamuzi hao watawasili kesho (Ijumaa) saa 8 mchana kwa ndege ya Ethiopian Airlines wakati Kamishna wa mechi hiyo Patrick Naggi kutoka Kenya atawasili leo (Alhamisi) saa 2.10 usiku kwa ndege ya Kenya Airways.
Iwapo Ngorongoro Heroes itafanikiwa kuitoa Sudan itacheza mechi ya raundi ya pili dhidi ya Nigeria.
Mechi ya kwanza itchezwa Julai 28 mwaka huu jijini Dar es Salaam wakati ya marudiano itakuwa kati ya Agosti 10 na 12 mwaka huu.
Ikifanikiwa kuitoa Nigeria, Ngorongoro Heroes itacheza mechi ya raundi ya tatu na mshindi kati ya Afrika Kusini na Congo Brazzaville.
Mechi ya kwanza itakuwa ugenini kati ya Septemba 21 na 23 mwaka huu wakati ya marudiano itakuwa nyumbani Oktoba 6 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269