Breaking News

Your Ad Spot

Jun 15, 2012

MWENYEKITI WA CHADEMA MBEYA MJINI NUSURA ASHUSHWE JUKWAANI

MWENYEKITI wa CHADEMA, wilaya ya Mbeya mjini, John Mwambigija, leo amenusurika kushushwa jukwaani na kupigwa na baadhi ya wanachama waliokuwa na mabango ya kutomtaka.
    Mwambigija aliokolewa na polisi waliofika kwenye mkutano huo, uliokuwa unafanyika eneo la soko la SIDO lililopo mjini hapa, baada ya kupata taarifa za kuwepo dalili za kutokea fujo kwenye mkutano huo.
    Mengi ya mabango yaliyokuwa yameandaliwa, yalikuwa yamekunjwa kwa kuhofia kukamatwa na polisi, lakini yalionyeshwa mara baada ya Mwambigija kupanda jukwaani na kuanza kuhutubia.
     Wakizungumza baadhi ya viongozi wa CHADEMA, ambao hawakutaka kutaja majina yao, walisema wamechoshwa na tabia ya Mwenyekiti wao huyo kukiharibu chama hicho, kwa kujenga makundi ndani yake.
     Waliongeza kutokana na adhima yao kushindwa kutimia kwa kuogopa polisi, watahakikisha wanaitisha mkutano wa ndani wa kumkataa Mwambigija, na baadaye watafanya mkutano mwingine wa hadhara ili kuanika udhaifu wa kiongozi huyo.
    Kwa mujibu wa wana-CHADEMA hao, Mwambigija amekuwa anakiendesha chama hicho jinsi atakavyo yeye, na hilo linachangiwa kwa kiasi kikubwa madai ya kuwa analindwa na Katibu Mkuu Taifa Dk.Willbroad Slaa.
    Naye Mwambigija alipotafutwa kuthibitisha tukio hilo, alisema yeye halifahamu na wala hakuona mabango yoyote katika mkutano huo.
    “Unajua tuna mamluki ndani ya CHADEMA, ambao wanaongozwa na aliyekuwa Katibu wetu wa mkoa, Eddo Mwamalala…baada ya kutoka kwenye uongozi amekuwa anaandaa mtandao wa kuhakikisha naondolewa kwenye uongozi” alisema Mwambigija.
    Aliongeza kuwa wanachama hao hawana ubavu wa kumshusha jukwaani wala kumpiga, na alikana tuhuma za kuendesha siasa za chuki kuwa huo ni uzushi ambao baadhi ya wana-CHADEMA wamekuwa wanamzulia.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages