NA TIGANYA VINCENT-MAELEZO, DAR ES SALAAM
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imeongeza mbele tarehe za kumaliza kazi ya sensa ya watu na makazi hadi Jumamosi ya tarehe 8 septemba mwaka huu ili kuhakikisha kuwa kila mwananchi aliyebaki anahesabiwa.
Kauli hiyo imetolewa leo(jana) na Kamishna wa Sensa kutoka NBS Hajjat Amina Mrisho Said wakati akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es salaam kuhusu masuala mbalimbali yaliyohusu kazi nzima ya kuhesabu watu na makazi inaendelea katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Alisema kuwa ni vema wananchi ambao hawajafikiwa na makarani wa sensa watoe taarifa katika Ofisi za Serikali za Mitaa au Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa ajili ya kuhesabiwa.
Hajjat Amina alisema taarifa zinazotakiwa ni pamoja na taarifa za wanakaya waliolala katika kaya yao usiku wa kuamkia tarehe 26 Agosti mwaka huu.
Alitoa mwito kwa wale ambao hawajaandikishwa hadi hivi sasa watume taarifa kwa namba 2122724, 0754583415, 2129622 ,0713335429,0713574622 na 0713312699 .
Hajjat aliongeza kuwa katika taarifa watakazopeleka ni vema wakaeleza mitaa au kijiji au kitongoji gani walipo ili iwe rahisi kwa NBS kutambua karani mhusika na kumwelekeza afanye kazi hiyo.
Aidha , Kamishna hiyo alisema kuwa malipo ya makarani yalishafanyika kwa awamu ya kwanza kulingana na mkataba na wanataraji kuwalipa awamu ya pili mara baada ya kazi zao kuhakikiwa na wasimamizi wao.
Aliongeza kuwa kwa wasimamizi watalipwa baada ya kazi zao kukamilika na kuhakikiwa na waratibu katika ngazi za wilaya.
Kuhusu malipo ya wenyeviti wa vijiji , vitongoji na mitaa ,alisema fedha zao wasishapelekwa siku nyingi na maelekezo ya namna ya kuzigawa yalipelekwa kwa waratibu wa Sensa wa mikoa na wilaya ambao walipaswa kuwa wameshalipa ili kuepuka manung’uniko.
Katika hatua hnyingine Kamishna wa Sensa huyo amewaonya kuwa Karani yoyote atakayechakachua taarifa na ikathibitika hilo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria na kuongeza kuwa NBS inafuatilia taarifa kutoka Dodoma eneo la Kisasa kuwa kuna Karani amekwenda kwenye kaya lakini alikuwa haulizi maswali.
Wakati huo huo Kamishna wa Sensa Hajjat Amina alisema kuwa wale viongozi wengi waliokuwa wakiwa hamasisha wenzao wasihesabiwe , wamehesababiwa kwa hiari baada ya kutoa ushirikiano wa kutosha ikiwemo kuacha taarifa muhimu zilizohitajiwa ikiwemo zile zilihitajika katika madodoso. Kwa wale ambao hawakuwakuta waliweka alama maalum ili wawarudie mara ya pili.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269