Balozi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Tuvako Manongi akichangia majadiliano ya ajenda namba 27 kuhusu Maendeleo ya Jamii, Kamati ya Tatu ambayo ni Moja ya Kamati sita zinazounda Baraza Kuu la 67 la Umoja wa Mataifa na kama ilivyo kwa kamati nyingine imeanza majadiliano ya kubadilishana mawazo kuhusu suala zima la maendeleo ya jamii, ambapo taarifa mbalimbali zimekuwa zikipokelewa na kujadiliwa. Kila nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa inapata fursa ya kuelezea mafanikio na changamoto inayokabiliana nazo katika utekelezaji wa jukumu la kuwaletea maendeleo wananchi wake. Aidha wajumbe wamekuwa pia wakitoa mapendekezo na ushauri wa nini kifanyike ili kusukuma mbele ajenga ya maendeleo endelevu na kuupiga vita umaskini kwa njia ya ubia kati ya nchi hizo, Umoja wa Mataifa na wadau wengine wa maendeleo. Katika Mkutano huo Tanzania kwa upande wake imesisitiza haja na umuhimu wa watu wenye ulemavu kupewa kipaumbele katika mipango ya maendeleo kwa kile inachosema kwamba kuna uhusiano wa karibu kati ya umaskini na ulemavu na kwamba kundi hilo la jamii ni muhimu sana katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia ( MDGs)
HABARI KAMILI
NA MWANDISHI MAALUM, NEW YORK
Wakati Umoja wa Mataifa((UM) ukieleza kwamba, kumekuwa na ongezeko kubwa la kati ya walionacho na wasionacho, Tanzania kwa upande wake inasema inaamini kwamba kuna uhusiano mkubwa kati ya umaskini na ulemavu.
Na kwa sababu hiyo, Tanzania , imependekeza kuwapo kwa juhudi za makusudi za kuwasidia watu wenye ulemavu na kutambua mchango wao ili waweze siyo tu kuondokana na umaskini na bali pia kujiletea maendeleo endelevu.
Kauli hiyo imetolewa na Balozi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Tuvako Manongi, wakati alipokuwa akichangia majadiliano ya Kamati ya Tatu ya Baraza Kuu la 67 la Umoja wa Mataifa. Kamati hiyo ambayo ni kati ya Kamati Sita zilizo chini ya Baraza Kuu, inahusika pamoja na mambo mengine na masuala ya Maendeleo, Haki za Binadamu na Utamaduni.
Kuanzia mwanzoni mwa wiki hii, wajumbe wa Kamati hiyo wamekuwa wakijadiliana na kubasilishana mawazo kuhusu Ajenda namba 27, ajenda hiyo inahusu suala zima la Maendeleo ya Jamii katika nyanja zote muhimu.
Katika mchango wake, Balozi Manongi anasema, kwa kutambua nafasi ya walemavu katika kusukuma mbele ajenda ya maendeleo na kuupiga vita umaskini, ndiyo maana ujumbe wa Tanzania kwa kushirikiana na ujumbe wa Ufilipino waliandaa Azimio kuhusu walemavu. Azimio ambalo hatimaye lilipelekea kuingizwa kwa suala la walemavu katika ajenda za Malengo ya Maendeleo ya Millenia ( MDGs).
Aidha kupitia juhudi hizo za Tanzania na Ufilipino, Umoja wa Mataifa umekubali kufanyika kwa mkutano wa kilele katika ngazi ya Viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali hapo mwakani.
Ajenda kuu ya mkutano huo itakuwa ni kujadili masuala ya watu wenye ulemavu na nafasi yao katika utekelezaji wa MDGs, na kuupiga vita umaskini, Malengo ambayo yanafikia kilele chake mwaka 2015.
Kupitia mkutano huo Tanzania inaamini kwamba viongozi wakuu wa nchi na serikali watatarajiwa kutoka na mkakati ambao utahakikisha kwamba watu wenye ulemavu na vipaumbele vyao vinazigatiwa katika maeneo yote ya maendeleo.
Kwa upande mwingine mwakilishi huyo wa Tanzania katika UM anasema , ingawa Tanzania imefanikiwa katika kuandaa mipango na sera za kumwondolea mwananchi umaskini kupitia MKUKUTA na MKUZA , kupunguza ukali wa maisha, na kuboresha huduma mbalimbali za kijamii zikiwamo za afya. Bado inakabiliwa na changamoto mbalimbli zikiwamo vifo vya wanawake wajawazito na watoto wachanga chini ya miaka mitano.
Aidha akasema changamoto nyingine ni ile ya idadi kubwa ya wanawake kuendelea kukabiliwa na unyanyasaji na ubaguzi kama ilivyo duniani kote. Hata hivyo amesema kwa upande wa Tanzania, serikali za pande zote mbili zimejitahidi katika kuhakikisha kwamba wanawake wanakuwa na fursa sawa ikiwa ni pamoja na kuwa na haki ya kumiliki ardhi.
Awali akifungua mkutano huo, Katibu Mkuu Msaidizi anayesimamia Idara ya Uchumi na Masuala ya Jamii ( ECOSOC) Bw. Wu-Hongbo, yeye aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo kwamba, ingawa kumekuwa na mafaniko kadha wa kadha katika utekelezaji wa MDGs kuelekea mwaka 2015 lakini bado kuna changamoto nyingi.
Akazitaja baadhi ya changamoto hizo kuna ni kuongezeka kwa pengo ya kati ya walionacho na wasionacho na tatizo kubwa la ukosefu wa ajira hususani kwa vijana.
Akabainisha kwamba kuanzia mwaka 1990 nchi 62 kati ya 116 na ambazo taarifa zao zimeweza kupatikana , zimeonyesha kwamba kumekuwapo na ongezo kubwa la kati ya wasionacho na walionacho hali ambayo imechangia katika kuzorotesha kasi ya kupunguza umaskini na matumaini ya kuwa na maendeleo endelevu.
Kama hiyo haitoshi, Bw. Wu- Hongbo anasema tatizo la ukosefu wa ajira nalo ni kubwa sana hususani wa vijana ambao ndio wamekuwa waathirika wakubwa.
“ Vijana, wanawake na wanaume wanawakilisha karibu asilimia 40 ya watu milioni 200 ambao hawana ajira duniani kote” anabainisha Bw. Wu- Hongbo
Nini basi kifanyike katika kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira na changomoto nyinginezo zinazohusu maendeleo ya mwanadamu.
Katibu Mkuu Msaidizi anapendekeza kwa Jumuia ya Kimataifa kuhakikisha kwamba sera na mipango yao ya kiuchumi inazingatia haki za wanawake pamoja na mambo mengine, kwa kile alichosema hakuna jamii inayoweza kustawi pasipo kuwawezesha wanawake.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269