Breaking News

Your Ad Spot

May 6, 2015

MGOMBEA URAISI KUPITIA CHADEMA KUPATIKANA AGOSTI 4



Viongozi wa Chadema wakiomba dua kabla ya kuanza kwa kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho kilichofanyika Dar es Salaam jana. Kuanzia kulia ni Makamu Mwenyekiti, Profesa Abdallah Safari, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu Dk Willibrod Slaa na Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu. Picha na Venance Nestory
Dar es Salaam. Kamati Kuu ya Chadema imepanga Agosti 4 kuwa siku ya kumpata mgombea wake wa urais ambaye ataingia kwenye kinyang'anyiro cha kumtafuta mgombea wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Vyama vinne vilivyounda Ukawa, Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, vimekubaliana kusimamisha mgombea mmoja wa kuanzia ngazi ya urais, lakini kila chama kitateua mgombea wake kabla ya kukubaliana mtu atakayeungwa mkono na vyama vyote.
Ratiba iliyotolewa jana na Chadema inaonyesha kuwa chama hicho kitatumia siku 76, kuanzia Mei 18, kumaliza mchakato wa kuwapata wagombea wake wa nafasi za udiwani, ubunge na urais kwa kuhitimisha na Mkutano Mkuu. Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Chadema itampata mgombea wake wa urais takriban siku 14 zaidi kulinganisha na mwaka 2010 wakati Dk Willibrod Slaa alipoteuliwa.
Kwa mujibu wa Ibara ya 7.710 (C) ya katiba ya Chadema, Mkutano Mkuu ndiyo chombo chenye mamlaka ya kumpitisha mgombea wa urais kwa tiketi ya chama hicho.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliwaambia wanahabari jana kuwa kamati hiyo imeridhia mchakato wa uchukuaji na urejeshaji fomu uanze ili watia nia katika maeneo mbalimbali waanze kuchukua fomu za udiwani, uwakilishi na ubunge.
Katika ratiba hiyo , chama hicho kimeyapa kipaumbele maeneo yanayoonekana kutokuwa na madiwani na wabunge, kuanza kuchukua fomu siku ya kwanza ya kazi hiyo na kuzirudisha Juni 25.
Aidha ratiba hiyo inaonyesha kuwa makada waliopo kwenye maeneo yenye madiwani watachukua na kurejesha fomu ndani ya siku 10 kuanzia Julai Mosi.
Wakati huo, maeneo yenye wabunge kwa sasa yakipatiwa siku tano za kukamilisha uchukuaji na urejeshaji wa fomu hizo kuanzia Julai 6 hadi 10 huku vigogo wanaounyemelea urais wakipigiwa kipenga Julai 20 hadi 25.
Mara baada ya wagombea urais kukamilisha taratibu za kinyang'anyiro, Chadema imepanga kufanya uteuzi wa mwisho wa wagombea ubunge Agosti 1 na 2 huku Baraza Kuu likipangwa kukutana siku inayofuata kabla ya Mkutano Mkuu kukutana Agosti, 4.
Chadema imeungana na CUF kutangaza ratiba ya kuwapata wanachama watakaowania uongozi katika Uchaguzi Mkuu ambao kikatiba unatakiwa ufanyike wiki ya mwisho ya Oktoba na kubakiza mchakato wa kumpata mgombea mmoja kila nafasi ya uongozi.
Akielezea zaidi yaliyojiri katika vikao vya kawaida vilivyofanyika Mei 3 na 4 mwaka huu, Mbowe alisema Kamati Kuu ilipokea na kujadili makubaliano yaliyofikiwa ndani ya Ukawa.
Mbowe, ambaye pia ni mbunge wa Hai, alisema kuwa kamati hiyo iliwapongeza viongozi hao kwa hatua walizofikia na kuwataka wamalize masuala machache yaliyosalia ili wawajulishe Watanzania wanaounga mkono umoja huo wajue kinachoendelea.CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages