Breaking News

Your Ad Spot

Nov 3, 2012

MIPANGO AFRIKA MASHARIKI KUWA NA VIZA MOJA YAIVA


BERLIN, UJERUMANI
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inakamilisha mipango ya kuwa na viza moja itakayowawezesha watalii kutembelea sehemu mbalimbali ndani ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo. 

Hii ni miongoni mwa hatua iliyokubaliwa kwa pamoja na nchi za Afrika Mashariki kuvutia watalii na wawekezaji katika kanda hiyo yenye kujumuiahsa nchi za Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi, linaripoti Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki(EANA) . 

Katibu Mkuu wa EAC, Dk. Richard Sezibera, alisema katika mkutano wa uwekezaji nchini Ujerumani kuwa hatua hizo ni pamoja na kuhamasisha maboresho na uwezeshaji katika kuibua ujasiliamali kama vile mikakati ya uanzishwaji vituo vya kibiashara, kuanzisha fursa za kimaendeleo na kuharakisha ubadilishaji wa sheria za kitaifa zinazokinzana na nia ya kuwepo kwa Soko la Pamoja. 

Mkutano huo wa siku mbili ulifunguliwa jana mjini Berlin na kuwaleta pamoja wawakilishi kutoka EAC na jumuiya ya biashara ya Ujerumani. 

Jumuiya pia inaandaa itifaki ya utawala bora yenye nia ya kuweka viwango na ukomo katika kuinua utawala bora ndani ya kanda. Mapendekezo ya itifaki hiyo kwa mujibu wa Dk. Sezibera unajumuisha maswala ya kulinda haki za binadamu, kuzingatia utawala wa sheria na upatikanaji wa haki, kuzingatia demokrasia na masuala ya chaguzi, uhamasishaji wa washikadau muhimu na kupambana na rushwa. 

“Upanuzi wa mtangamano wa EAC unahitaji mazingira ambayo ni tulivu na imara katika kuinua uwekezaji wa biashara katika kanda. Migogoro ya ndani ya aina yoyote, iwe ya ugawaji wa rasilimali au chaguzi, inahitaji mfumo wa kikanda ambao unajua muktadha wa kanda na mgogoro wenyewe,” alisema Dk Sezibera katika hotuba yake ambayo EANA ilipata nakala yake.  

Dk. Sezibera alisema msisitizo pia umeelekezwa kwenye upandishwaji na uboreshaji wa mtandao uliopo wa kilomita 8,100 za reli, kwa kuongezea upanuzi wake katika maeneo mengine ya Afrika Mashariki.  

Alibainisha kuwa kilomita 5,000 za njia ya reli inategemewa kuongezwa hivi karibuni wakati mradi wa Lamu-Juba/Addis na ule wa Isaka-Kigali/Keza utakapokamilika. Miradi hii inakadiriwa kugharimu dola za Kimarekani billioni 29 inayojumuisha maboresho ya njia zilizopo, kupandisha hadhi na taratibu nyingine muhimu za kuwezesha utumiaji wa njia hizo. 

Hatua zingine ni kutekeleza Mradi wa mtandao wa Barabara wa Afrika Mashariki katika Kanda na kukamilisha miradi mingine mbayo inaendelea kwa sasa kwa nia ya kujenga uwezo wa uhakika wa kusambaza umeme. 

“Upatikanaji mpya wa nishati katika kanda umeongezea fursa katika sekta ya nishati. Matarajio ya hifadhi ya mapipa bilioni 2.5 Uganda, Tanzania yenye futi za ujazo 3-7 trilioni za gesi na hivi karibuni kutangazwa kupatikana kwa mafuta nchini Kenya, vyote vinaashiria Afrika Mashariki kuwa na mwelekeo wa uwekezaji katika miundombinu,” alisema Dk Sezibera.  

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages