Breaking News

Your Ad Spot

Feb 21, 2013

KUMBUKUMBU YA MAREHEMU GEOFFRET NKURLU

MAREHEMU NKURLU

Kazi ya Mungu haina makosa, lakini kwetu ni majonzi makubwa.
Kama binadamu tungekuwa na uwezo wa kukata rufaa ya kifo, hakika nasi tungekata rufaa mbele ya Mungu ili turudishiwe  baba yetu kipenzi, Geoffrey Nkurlu, na kuendelea kuishi pamoja nae hapa duniani.

Hakika, tunajikuta tukiandika barua hii kwa uchungu mkubwa, maana familia yako inaadhimisha miaka 12 ya kukukosa kwako, tangu  hapo tarehe kama ya leo 17/2/2001 ulipotutoka na kuwa mbali na sisi.

Baba mpendwa, watoto wako wote bado tumeshikamana  kwa pamoja kama jinsi wewe ulivyotulea na kutusisitiza  tuwe wamoja. Tuko pamoja katika dhiki na faraja,hakika tunaendelea kukuwaza, kukukumbuka, kukuenzi na kuishi katika maadili bora  ambayo ulitufunza.Kwa kweli tunakulilia miaka yote, maana mchango wako ni mkubwa katika kuilea familia yako, ambayo leo hii imeweza kusimama imara kutokana na malezi mema na  mapenzi yako.

Baba mpendwa, sisi watoto  wako, wakati mwingine kila tunapokufikiria, hakika mioyo yetu inashindwa kuamini kama ni kweli haupo pamoja nasi. Tangu kuzaliwa kwetu, umeweza kutulea, kutusumbukia na kutusomesha kwa kidogo chako ulichokuwa unakipata.

Kitendo kama hicho ni cha kipekee. Nani kama wewe? Maisha yetu bila wewe, yangekuwaje katika kipindi cha maisha yetu, tangu kuzaliwa kwetu, kukua na kufikia katika kila kipindi kigumu ambacho daima ni picha kamili ya maisha yetu.

Ingawa tupo mbali na wewe, lakini  umetutoka kimwili tu, kiroho tuko na wewe. Bado tunakumbuka kauli zako, ushauri wako katika familia yako uliyoiacha katika wasiwasi mkubwa. Tumelia sana. Tumeumia sana.Na tuonapo baba wa wenzetu wakifurahia na kupata hata mawaidha, nasi huwa tunaukumbuka uwepo wako.

Picha na mtiririko wa maisha yako ni ushahidi kuwa wewe ulikuwa baba bora kwetu, huku tukiamini Mungu muweza na muumba wa yote ataitumia fursa hiyo kama sehemu ya kukulaza mahali pema kwa unyenyekevu wako.

Suala zima la kifo, linaashiria kuwa ni sehemu ya mpito katika maisha ya duniani. Vitabu vyote vya dini vimekitaja kifo kuwa hakuna kiumbe ambaye anaweza kuvuka bila kupitia katika hatua hiyo, hivyo tunatumia nafasi hii kukuombea mwanga wa milele ukuangazie.

Baba mpendwa, wakati tunaendelea kuyakumbuka mazuri yako katika familia hii uliyoiacha hali ya kuwa bado inakuhitaji, macho yetu yanashindwa kuhimili mtiririko wa machozi katika mboni zetu, yakiwa ni mapenzi makubwa baina yako na yetu.
Kazi ya Mungu haina makosa, lakini kwa upande wako ni ngumu mno kukubali matokeo na kujua kweli hatutakuwa wote katika kipindi cha maisha ya duniani. Umetangulia baba. Jina la bwana libarikiwe,sisi tunaendelea kukulilia miaka yote.

Tusingeweza na hatukuwa na sababu ya kuzuia hitaji la Mungu. Ingawa sisi tulikupenda na kukuhitaji sana, lakini Mungu alikupenda zaidi na aliona muda wako wa kuishi duniani umekoma na hakika ulistahili kwenda kwake kwa mapenzi yake, kwa vile kifo ni njia yetu sote na  kila nafsi itaonja mauti. Dunia tunapita.

Sisi watoto wako, Masala, Matina, Nzigia, Amani, Angaza na Atuza.
Tunakulilia na kukuombea daima.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages