HII NI TAARIFA YA IKULU KAMA TULIVYOIPATA IKIKANUSHA HABARI ILIYOCHAPISHWA LEO KATIKA GAZETI LA TANZANIA DAIMA,
Gazeti la Tanzania Daima la leo, Jumamosi, Februari 16, mwaka huu wa 2013 lilichapisha habari nzito kwenye ukurasa wa kwanza wa gazeti hilo zenye kichwa cha habari, “Wassira, Mwema watimuliwa Geita”.
Katika habari hiyo, Gazeti hilo limedai kama ifuatavyo: “Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira na Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Saidi Mwema wametimuliwa mkoani Geita…Vigogo hao wa Serikali walikumbwa na patashika hiyo juzi (Alhamisi, Februari 14, 2013) mkoani humo walikoenda kusaka suluhu ya vurugu za kidini…”
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais (DPC), Ikulu, inapenda kuwaarifu wananchi kuwa habari hii siyo ya kweli. Ni habari ya kutunga. Ni habari ya uzushi. Na kwa sababu habari hiyo ni ya uongo, ni ya uzushi na ni ya kutunga, ni dhahiri kuwa ina lengo la kuwapotosha wananchi na kudhalilisha maofisa waandamizi wa Serikali.
DPC inapenda kufafanua kama ifuatavyo:
Kwanza Mheshimiwa Stephen Wassira siyo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu. Mhe. Wassira ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu.
Pili, Mhe. Rais hakwenda Geita juzi, Alhamisi, Februari 14, 2013 kama inavyodaiwa na Gazeti la Tanzania Daima. Kwa siku tatu zilizopita, Mhe. Wassira amekuwa anaandamana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete katika ziara ya mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.
Juzi, Alhamisi, siku ambayo inadaiwa kuwa “alitimuliwa Geita” Mheshimiwa Wassira aliandamana na Mhe. Rais katika mazishi ya Askofu Mstahivu( Bishop Emeritus) wa Jimbo Katoliki la Moshi, Mhashamu Baba Askofu Amedeus Peter Msarikie yaliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la Kristo Mfalme mjini Moshi.
Jana, Ijumaa, Februari 15, 2013, Mhe. Wassira aliandamana na Rais Kikwete kumzika aliyekuwa Askofu wa Dayosisis ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) ya Kaskazini Kati, Baba Askofu Dkt. Thomas Olmorijoi Milia Lazier yaliyofanyika Kanisa Kuu ya KKKT Dayosisi ya Arusha, mjini Arusha.
Leo, Jumamosi, Februari 16, 2013, Mhe. Wassira akiambatana na Mhe.Rais Kikwete amerejea Dar es Salaam na kwenda moja kwa moja nyumbani kwake Masaki kushiriki shughuli za msiba wa kaka yake. Na hata leo hakwenda Geita.
DPC inapenda kuvikumbusha vyombo vya habari nchini kuhusu msimamo thabiti na usionyumba wa Serikali ya Mheshimiwa Kikwete wa kuhimiza, kulea na kulinda Uhuru wa Vyombo vya Habari na uhuru mwingine wowote nchini. Hakuna wakati wowote katika historia ya nchi yetu, Uhuru huo umejengeka, ukaimarika na ukashamiri kama ilivyo kipindi cha sasa cha Uongozi wa Awamu ya Nne ya Rais Kikwete.
Lakini ili uhuru huo uzidi kushamiri zaidi ni wajibu wa vyombo vyetu vya habari nchini kutenda kazi zao kwa kuongozwa na misingi mikuu ya uandishi wa habari ambayo ni kuandika habari za kweli na kwa misingi ya haki.
Habari hii ya Tanzania Daima leo ni mfano mwingine wa uvunjaji wa misingi hiyo kwa sababu siyo tu kwamba habari yenyewe ni ya uongo bali Mhariri wa Gazeti hilo hata hakujali kumtafuta na kuzungumza na Mhe. Wassira mwenyewe ambaye angesaidia kumpa ukweli wa hakika wa “habari zake za uhakika kutoka Geita”.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269