Breaking News

Your Ad Spot

Apr 10, 2013

Dk. MWINYI ATAKA WATAALAM WA AFYA KUZUIA MAGONJWA


FRANK JOHN NA HASSAN SILAYO-MAELEZO
WAZIRI wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Hussein Mwinyi (kushoto), amewataka wajumbe wa Baraza la Usajili  wa  Wataalam wa Afya  ya   Mazingira nchini, kufanya kazi kwa kujituma na ushirikiano ili kupambana na changamoto zinazokabili sekta   hiyo  na kuzuia maambukizi ya magonjwa.

Dk. mwinyi aliyasema hayo leo (jana) wakati wa uzinduzi wa baraza hilo uliofanyika jana jijini Dar es salaam ambapo  alisema sekta ya afya na ustawi wa jamii inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ongezeko la milipuko ya magonjwa kutokana na uchafuzi wa mazingira.

Alibainisha kuwa afya ya mazingira ni suala mtabuka ambalo linahitaji ushirikishwaji wa wadau  wa sekta ya afya ya mazingira ili kutoa matokeo yenye tija na ubora wa hali ya  juu katika kupambana na magonjwa hayo.

Aliongeza kuwa  serikali inatarajia kwamba kwa kutumia baraza hilo huduma ya afya ya jamii itatolewa kwa wananchi kwa viwango vinavyotakiwa na hivyo,  kuboresha maisha ya wananchi kwa kusimamia na kudhibiti utoaji wa huduma ya afya ya mazingira kwa misingi ya haki.

“Pia  wataalam wa kada hii watajiendeleza na kufikia kiwango cha juu cha elimu tofauti na miaka iliyopita ampapo wengi waliridhika na kubaki katika eneo moja kwa muda mrefu na kusababisha kudumaa kwa taaluma,alisema  Dk.Mwinyi.

Alisema  kwa  kufanya , hivyo upo  uwezekano mkubwa wa kupunguza ongezeko la kasi ya magonjwa, vifo na madhara mengine katika jamii yatapungua  ikiwa  huduma ya afya ya jamii itaboreshwa.

Naye Mwenyekiti wa baraza hilo , lililomaliza muda wake Bwana Fabian Magoma alisema linakabiliwa na changamoto za upungufu wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za baraza na ukosefu wa mitaala hivyo linahitaji ushirikiano wa karibu na taasisi zinazoandaa mitaala ya elimu nchini.

Magoma alishauri baraza hilo, liangalie sheria zinazohusiana na afya ya mazingira, ili waweze kutambua taaluma hiyo. Huku akiongeza kuwa watu wanaoteuliwa  kufanya kazi hiyo wawe ni wa kada hiyo.

Kwa upande wake mjumbe wa baraza jipya Haji Mdemu alishauri serikali kuzingatia  mbinu za zamani za afya mazingira , kuzifufua ili kuimarisha afya mazingira na uwajibikaji wa maafisa afya.

Baraza hilo lilizinduliwa rasmi mwaka 2009 ikiwa ni matokeo ya sheria ya kusajili wataalam wa afya mazingira ya mwaka 2007 iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania likiwa na majukumu ya kusajili, kudhibiti nidhamu kiutendaji katika kada ya afya ya mazingira pamoja na kumshauri  waziri husika  juu ya masuala yote yahusuyo afya ya mazingira nchini.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages