Breaking News

Your Ad Spot

Apr 25, 2013

WAKENYA WAFUATA TANZANIA TEKNOLOJIA YA MATENGENEZO YA UMEME BILA KUKATA


MOROGORO,Tanzania
SHIRIKA la Umeme la Kenya (KPLC) limetuma wataalam wake kuja Tanzania kwenye kampuni binafsi ya McDonald Liveline Technology, iliyopo mkoani Morogoro, kujifunza teknolojia ya kutokata umeme wakati wa mategenezo.

KPCL imekuja na hatua hiyo ikiwa ni katika jitihada za kutafuta suluhisho la kudumu dhidi ya kero ya kuwakatia umeme mara kwa mara wananchi, wakati wa matengenezo mbalimbali kwenye miundombinu ya nishati hiyo, ikiwemo kubadilisha nguzo na kurekebisha hitilafu kwenye nyanya.

Wataalam hao ambao walitembelea jana kampuni hiyo ya McDonald Live line Teknology, ni Meneja Operesheni na Huduma kutoka makao makuu ya Shirika hilo jijini Nairobi, Noah Omond Ogano, Meneja Msaidizi wa huduma za matengenezo mkoa wa Nairobi, Injinia Charles Mwaura, na Mwalimu wa masuala ya matengenezo ya mtandao wa ugavi wa umeme Peter Waweru.

Wakitembezwa  na Mkurugenzi wa Kituo hicho ambaye pia ndiye mtaalam wa teknolijia ya matengenezo ya umeme bila kukata, McDonald Mwakamele ambaye amewahi kuwa mtumishi katika Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na sasa ameamua kujiajiri, Wakenya hao walishuhudia utaalam wa hali ya juu na vifaa vya kisasa vinavyotumiwa na kampuni ya McDonald Liveline katika matengenezo ikiwemo vya kinga ya madhara ya fundi kunaswa na umeme akiwa kazini.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Wakenya hao walisema, Kenye tayari inao utaalam na vifaa vingi vya matengenezo ya umeme, lakini wakakiri kwamba bado teknolojia hiyo ya matengenezo bila kukata mtiririko wa umeme bado hawana, na kwamba kutokana na kutokuwa nayo wamekuwa wakilazimika kukata umeme mara kwa mara wakati wa matengenezo jambo ambalo wamesema limekuwa likikera wateja.

"Unajua wananchi wengi siku hizi wanajua haki zao, kampuni inapoingia mkataba na mwananchi kwamba inampatia huduma fulani ambayo ni muhimu maana yake ni kwamba kutompatia huduma hiyo hata kwa nusu saa ni kuvunja haki ya mteja, na sisi Kenya tatizo hili tunalo, ndiyo sababu sasa tumekuja hapa kupata utaalam ili kukomesha shida hii", alisema, Injinia Mwaura.

Walisema mbali ya kubughudhi mkataba wao wa kimsingi na wateja, ukataji wa mara kwa mara wa umeme wakati wa matengezo umekuwa ukilisababishia shirika la KCPL upotevu wa fedha nyingi.

"Kugawa umeme ni kama biashara nyingine, sasa umeme unapokuwa unapatikana fedha inaingia, lakini ukikatika mita inasimama na hivyo fedha haiingii jambo ambalo ni hasara ambayo inapaswa kuepukwa kama shirika lina lengo la kutaka kusonga mbele na kuwa imara zaidi. Lakini pia ubora za huduma pia ni moja ya mambo ambayo huweka taswira nzuri ya Shirika mbele ya umma, linapokuwa linatoa huduma mbovu taswira yake inakuwa mbaya, hii ndiyo hatutaki itokee KCPL", alisema, Ogano.

Wakenya hao walisema, baada ya kusikia kwamba Tanzania upo utaalam wa kufanya matengenezo ya umeme bila kuukata, waliamua kuja na kwamba baada ya kutembelea  kituo hicho cha Mwakamele wanatarajia kwamba baada ya mwaka wa fedha wa Unaoanza Julai mwaka huu wataanza rasmi utekelezaji wa teknolojia hiyo nchini Kenya.

Akizungumzia teknolojia hiyo, Mwakamele alisema, alipata mafunzo yake nchini Marekani akiwa ni miongoni mwa wanafunzi watano tu kutoka Afrika, na kwamba walifaulu wachache kuendelea na kazi ya teknolojia hiyo kwa kuwa wataalam wengi wa masuala ya umeme huikimbia kwa kuwa ni ya hatari kwa asiyekuwa makini akiwa kazini.

Alisema, katika miaka ya 1988, alikuwa akifundisha katika kilichokuwa chuo cha Tanescho Morogoro, lakini baadaye chuo hicho kilifutwa na kugeuzwa Chuo Kikuu cha Kiislam, hatua iliyomfanya alazimike kuondoka Tanesco, lakini kutokana na uzalendo akaamua kuwekeza ujuzi wake kwa kuanzisha kituo cha kutoa mafunzo na huduma ya ufundi huo.

Mwakamele alisema, licha ya kwamba ushirikiano anaopata kutoka serikalini bado siyo wa kutosha kulingana na umuhimu wa teknolojia yenyewe, lakini ameshafanya kazi za kuboresha miundombini ya huduma za umeme ya Tanesco katika maeneo mbalimbali nchini na imeinyesha manufaa ufanisi na manufaa makubwa.

Alisema, endapo teknolojia hiyo ya matengenezo bila kukata umeme itatumika, Tanzania itaweza kuokoa fedha na muda ambavyo vimekuwa vikipota kila umeme unapolazimika kukatwa kwa ajili ya matengenezo kama ya kubadilisha nguzo au kukata miti iliyofusa nyanya za umeme.
MKURUGENZI wa Kampuni ya McDonald Liveline Techonology, McDonald Mwakamele (kulia) akionyesha baadhi ya vifaa vinavyotumika katika tenkolojia ya matengenezo ya umeme bila kukata, Wataalam kutoka Shirika la Umeme la Kenya (KCPL) walipotembelea kituo chake hicho, kilichopo Mvomelo mkoani Morogoro, jana kujifunza teknolojia hiyo. Kutoka kushoto ni Meneja wa Mafunzo ya Ufundi wa KCPL Peter Waweru, Meneja wa Huduma wa KCPL  Charles Waura na Meneja wa Operesheni na Matengenezo KCPL, Noah Ogano.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages