Breaking News

Your Ad Spot

Jun 11, 2013

KAMATI KUU YA CCM YAIPOKEA RASMI RASIMU YA KATIBA MPYA

*Yawaachia Wanachama wake kutoa msimamo
*Yawahimiza kujitokeza kwa wingi kwenye mijadala rasmi
*Yaiomba Tume kuuelimisha umma hatua kwa hatua
DAR ES SALAAM, Tanzania
Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, iliyokutana jana mjini Dodoma, 10/06/2013 chini ya Mwenyekiti wa Taifa wa CCM Dk. Jakaya Kikwete kimepokea rasimu ya katiba mpya na kuamua kuwaachia wanachama wake kuitolea msimamo wa pamoja.

Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, NBape Nnauye amesema, Kamati Kuu imeipongeza Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini kwa kazi nzuri na kukamilisha kazi kwa wakati.

"Kwa kuwa rasimu hii ni ya kwanza ambayo inapelekwa kujadiliwa tena kwa wananchi kupitia mabaraza mbalimbali ya katiba baada ya kwisha kwa hatua ya kutoa maoni, Kamati Kuu imekiagiza Chama kijipange kuijadili rasimu hiyo ndani ya Chama kama baraza la kitaasisi la katiba na kuwataka wanachama na wapenzi wa CCM wajitokeze kwa wingi na kushiriki kwenye mabaraza haya", amesema Nepe.

Amesema ushiriki huu wa CCM baada ya kupokea rasimu umekusudia kushirikisha wanachama wote kwenye ngazi ya matawi, wilaya, mkoa na Taifa.

Amesema pia Jumuiya za CCM zitashiriki kama mabaraza ya Katiba na hivyo kuongeza ushiriki wa wanachama na wapenzi wa CCM katika mchakato huu.

"CCM kama baraza la Katiba la kitaasisi litaipitia rasimu iliyowasilishwa kifungu kwa kifungu na kwa kuzingatia maoni ya CCM yaliyotolewa mwanzoni kabisa mwa mchakato wa mabadiliko ya Katiba, wanachama wetu watashiriki kutoa maoni yao, Nape alifafanua.

Nape alisema, pamoja na kazi nzuri ya Tume ya Mabadiliko ya katiba, Kamati Kuu inaiomba Tume hiyo kueleza vizuri mchakato mzima kutoka rasimu ya kwanza ya sasa mpaka rasimu ya mwisho ili kuondoa mkanganyiko kwa wananchi juu ya mchakato mzima hasa baada ya rasimu ya kwanza kutoka.

"Kamati Kuu inawasihi Watanzania kushiriki tena kwenye kutoa maoni kupitia mabaraza ya katiba kwa rasimu ya kwanza, bunge maalum la katiba kwa rasimu ya pili na kupitia kura ya maoni kwa rasimu ya tatu, kwa amani,utulivu na kuvumiliana ili mwisho wa siku tupate Katiba nzuri ya nchi yetu kwa masilahi ya Watanzania walio wengi", alisema.
Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye akizungumza na wandishi wa habari mjini Dodoma leo, kuhusu maamuzi ya kikao cha Kamati Kuu ya CCM, kuhusu rasimu ya Katiba mpya.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages