Breaking News

Your Ad Spot

Aug 14, 2013

HATMA YA MADIWANI WANANE WALIOTIMULIWA BUKOBA, SASA MIKONONI MWA KAMATI KUU YA CCM

Nape akizungumza na Waandishi leo, Dar es Salaam
DAR ES SALAAM, Tanzania
HATIMA ya madiwani wanane wa CCM katika Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, waliovuliwa uongozi na Halmashauri Kuu ya CCM mkoa Kagera, sasa ipo mikononi mwa Kamati Kuu ya CCM.

Hatima hiyo, imetangazwa leo jijini Dar es Salaam, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Nape Nnauye alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu sakata hilo.

Akizungumza na waandishi, Nape amesema kwamba licha ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kagera kutangaza uamuzi wake wa kuwafutia madiwani hao dhamana ya CCM, jana tarehe 13/08/2013 katika kikao chake cha siku moja kilichofanyika mjini Bukoba, CCM Makao Mkuu imewataka madiwani hao kuendelea na kazi kama kawaida wakati wakisubiri maamuzi ya Kamati Kuu ya CCM ambayo itakutana mjini Dodoma Agosti 23, mwaka huu.

"Kwa mujibu wa utaratibu wa kutoa adhabu kwa viongozi wa CCM walio kwenye vyombo vya dola hasa Wabunge na Madiwani uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Mkoa sio wa mwisho.  Uamuzi huo unapaswa kupata Baraka za Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ndipo utekelezwe", alisema Nape na kuongeza;

"Hivyo basi, mpaka sasa Madiwani hao wanane waliosimamishwa wanapaswa kuendelea na kazi zao kama kawaida wakisubiri kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa kitakachoketi tarehe 23 Agosti, 2013 mjini Dodoma ambacho pamoja na mambo mengine kitapitia uamuzi huo wa Halmashauri Kuu ya Mkoa wa Kagera".

Nape alisema, pia CCM makao makuu wamepokea barua ya madiwani hao kukata rufa kupinga uamuzi huo wa Halmashauri Kuu ya Mkoa kwa msingi wa madai ya kukiukwa kwa utaratibu katika kufikia uamuzi huo.

Alisema, wakati sakata hilo likiwa bado lipo katika hali hiyo, CCM inawasihi wananchi wa Bukoba na Kata husika, wanachama na viongozi wote kuwa watulivu katika kipindi hiki ambapo suala hili linashughulikiwa na vikao vya Kitaifa.

Akifafanua zaidi Nape amekanusha kwamba, Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Kikwete alipokuwa katika ziara ya kiserikali mkoani Kagera, alitumia fursa hiyo pia kuwapatanisha madiwani na Meya katika mgogoro unaodaiwa kuota mizizi baina yao.

Nape amesema, Rais Kikwete aliagiza hatua za kumaliza mgogoro huo zimalizwe kwa kufuata sheria na kanuni kwa lengo la kuhakikisha kuwa hakuna upande utakaoonewa au akupendelewa.

Akitangaza jana  Katibu wa CCM wa mkoa wa Kagera, Avelin Mushi,aliwataja madiwani waliotimuliwa kuwa ni,  Yusuph Ngaiza (Kata Kashai) ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wilaya Bukoba, Samwel Ruangisa (Kitendagulo) ambaye ni Meya mstaafu na Mkuu wa mkoa wa mkoa wa kwanza wa mkoa wa Kagera, Murungi Kichwabuta (Viti maalumu) Deusdedith Mutakyawa (Nyanga) Richard Gaspal (Miembeni)Alexander Ngalinda (Buhembe) ambaye pia alikuwa Naibu MeyaDauda Kalumuna (Ijuganyondo) na Robert Katunzi wa kata Hamugembe. VIDEO:NAPE AKIZUNGUMZA NA WAANDISHI LEO>>BOFYA HAPA

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages