.

KATIBU MKUU JUMUIA YA WAZAZI AANZA KAZI KWA KUTEMA CHECHE

Aug 27, 2013

Seif Shabaan Mohamed
KATIBU Mkuu mpya wa Jumuia ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi Seif Shabaan Mohamed  ameonya kuwa hatakuwa na huruma na kiongozi yeyote atakayefuja fedha za jumuia hiyo.

Alisema katika kipindi cha miaka mitano cha uongozi wake atahakikisha anafanyakazi kwa uadilifu na uamini mkubwa  na kwamba atakuwa mkali na makini kuhusu matumizi ya fedha za jumuia yake.
Mohamed alisema kila kiongozi anastahili kufanya kazi kwa kuzingatia taratibu, maadili na miiko kwa kutokana na dhamana aliyonayo na si vinginevyo.
Kauli Katibu Mkuu huyo mpya imekuja huku jumuia hiyo ikiwa imegumbikwa na wingu jeusi la matumizi mabaya ya fedha na hivyo kuifanya isue sue kwa kipindi kirefu badala ya kusonga mbele.
Aliyasema hayo jana katika ukumbi wa Dodoma Hoteli wakati akiwashukuru Wajumbe wa Baraza Kuu la Jumuia ya Wazazi kwa kumthibitisha kushika wadhifa huo.
Mohamed anashika nafasi hiyo kwa mara ya kwanza baada ya aliyekuwa akiishikilia Khamis Suleiman Dadi kutoteuliwa tena na vikao vya juu vya CCM.
“Kwanza nashukuru kupata nafasi hii ya juu maana sikutegemea kama ingekuwa hivi, lakini niwaambie kwamba nitakuwa mkali sana na masuala fedha,” alisema Mohamed.
Hata hivyo, aliwataka viongozi wenzake wampe ushirikiano wa kutosha ili kifikisha malengo ya jumuia hiyo kuwa katika hali nzuri zaidi.
“Binafsi nitafanya kazi kwa karibu sana nikishirikiana na na nyinyi wenzangu hivyo, nanyi mnipe ushirikiano,” alisema.
Mbali na Katibu Mkuu huyo mpya, jumuia hiyo imefanya mabadiliko makubwa ya kiongozi baada ya kupata Manaibu Makatibu Wakuu wapya.
Manaibu hao ni Glorious Luoga (Bara) na Najma Murtaza Giga (Zanzibar).
Akizungumza na viongozi hao, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdallahman Kinana aliwapongeza viongozi hao kwa kushika wadhifa huo na kuwataka wafanye kazi kwa uadilifu na kwa kasi kubwa.
“Kwanza nimpongeze mwenyekiti wenu Bulembo na viongozi wenzake kwa kuifanya jumuia hii sasa isikike kila kona.
“Jumuia hii ilikuwa inakufa, lakini sasa kila unakopita unasikia Bulembo kapita na anafanya mambo makubwa sana ya kuipigania jumuia na Chama chake,” alisema Kinana.
Hata hivyo Kinana alimtaka Bulembo na viongozi wenzake kuongeza kasi ya kuiimarisha jumuia hiyo ili iwe na nguvu zaidi.
Kwa upande wake Bulembo alisema amejipanga kikamilifu kwa kuishirikiana na viongozi wenzake ili kuidishia hadhi yake jumuia hiyo.
“Sisi tumejipanga kikamilifu…tutakimbia huku na kule kwa ajili ya kukisemea chama chetu kwa mazuri iliyoyafanya huku tukifufua uhai wa jumuia yetu,” alisema.
Bulembo aliutaka uongozi mpya wa sasa wa jumuia hiyo kukaa kama timu moja na kuchapakazi kwa ushirikiano wa karibu.

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ª