.

RAIS ATUNUKU HATI IDHINI KWA VYUO VINANE NCHINI

Aug 20, 2013

RAIS KIKWETE
NA IMMACULATE MAKILIKA, MAELEZO
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete ametunuku hati Idhini kwa vyuo vikuu na vyuo vishiriki viane baada ya vyuo hivyo kutimiza taratibu zote za uanzishwaji wake hapa nchini.

Vyuo vilivyotunukiwa hati  baada ya kutimiza taratibu zote ni Chuo Kikuu cha Tumaini(TUMA),Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT),Chuo  Kikuu Kishiriki  cha Ruaha(RUCo),Chuo Kikuu  cha Mount Meru(MMU),pamoja na Chuo Kikuu cha Arusha (UoA).

Vyuo vingine vilivyotunukiwa hati hiyo ni Chuo Kikuu Kishiriki cha Tumaini Dar es salaam(TUDARCo) ,Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi  na Teknolojia Arusha (NM-AIST) na Chuo Kikuu cha Sayansi  na Teknolojia Mbeya(MUST).

Rais  Kikwete  alivitunuku  vyuo hivyo kwenye hafla fupi iliyofanyika  leo Ikulu jijini  Dar es Salaam , ambapo  alisema  vimepiga hatua kubwa ya  kuongeza idadi ya wanafunzi wanaojiandikisha hadi kufikia  laki moja sitini na sita elfu mwaka 2013 ,ukilinganisha na idadi ya wanafunzi elfu arobaini ya mwaka 2005.

 “Idadi kubwa ya wanafunzi pekee haitoshi,ubora wa elimu uzingatiwe . Ikiwemo kupata wakufunzi wengi na wenye sifa  ni lazima sisi wenyewe tuwekeze ndani ili kupata wakufunzi wakutosha katika vyuo vyetu ,” alisema Rais Kikwete.

Aidha Rais  Kikwete  alivitaka vyuo hivyo kutekeleza  mkakati wa elimu wa  Matokeo  Makubwa Sasa (Big results now)  ipasavyo  ili kuboresha elimu nchini kwa kuimarisha miundombinu  ya  vyuo vikuu nchini.

Aliongeza kuwa  lazima viwe na mahitaji yote muhimu kwa kutoa elimu bora ikiwemo vifaa vya kutosha,maabara,vyuo vya zamani viwekwe kwenye viwango  ili kukidhi utoaji wa elimu bora, na kusisitiza vyuo vikuu vyetu vishirikiane na vyuo vikuu vya nje na kuvishauri   vitafute vyanzo vingine vya mapato ili  kukidhi uendeshaji badala ya kutegemea ada.

 Utoaji wa hati Idhini kwa vyuo vikuu  ni zoezi endelevu linalolenga  kuboresha  kiwango cha utoaji elimu  ya juu nchini  ili kuwezesha wahitimu  kukabiliana na changamoto  za maendeleo  ya taifa letu kwa ujumla. Kwa mara ya mwisho zoezi hili lilifanyika  tarehe 18 Agosti,2010 ambapo jumla ya vyuo vikuu na vyuo vishiriki  13 vilitunukiwa hati Idhini.

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช