*KINANA AWASIKILIZA KWA MOYO MKUNJUFU
*AWATAKA KUWA WATULIVU WAKATI SERIKALI IKIFANYA JITIHADA KUTATUA KERO ZAO
SHINYANGA, Tanzania.
*AWATAKA KUWA WATULIVU WAKATI SERIKALI IKIFANYA JITIHADA KUTATUA KERO ZAO
NDUGU KINANA |
MSAFARA wa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana leo umelazimika kusimama kwa muda baada ya wakazi wa
kijiji cha Mwabenda kata ya Solwa wilayani Shinyanga kuuzuia wakiwa na mabango
wakiomba kupatiwa huduma ya maji na umeme.
Hali hiyo ilijitokeza wakazi msafara huo ukielekea katika
kijiji cha Salawe ambako kulipangwa kufanyika kwa mkutano wa hadhara ambapo
mara baada ya magari kufika katika kijiji hicho umati mkubwa wa wananchi
ulisimama barabarani ukiwa na mabango yenye ujumbe wa “Tunataka Maji” na
“Tunataka umeme.”
Kutokana na hali hiyo msafara huo ulilazimika kusimama
huku mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Annarose Nyamamubi, mbunge wa Jimbo la Solwa,
Ahmed Salum na baadhi ya askari polisi wakihaha kuwazuia wananchi hao na kuwasihi
waondoke barabarani ili msafara uweze kuendelea na safari yake.
Hata hivyo juhudi hizo hazikufua dafu mbele ya wananchi
hao ambao mbali ya kubeba mabango baadhi ya akina mama walikuja na ndoo za maji
wakionyesha maji wanayotumia ambayo yalikuwa yamechanganyikana na tope huku
wakihoji kuwa hayo maji ndiyo na hao viongozi wanatumia kwao?
Hali hiyo ilisababisha katibu mkuu na viongozi wengine wa
kitaifa aliokuwa ameongozana nao pamoja na mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Ally
Rufunga kufika katika eneo ambalo wananchi hao walikuwa wamesimama na
kuwasikiliza malalamiko yao
ambapo waliomba kushusha mabango chini ili wajibiwe hoja zao.
Walipopewa nafasi ya kueleza tatizo lao walisema pamoja
na bomba kubwa la maji kutoka Ziwa Victoria
kwenda katika miji ya Shinyanga na Kahama kupita katika kijiji chao lakini wao
hawana huduma hiyo huku wakilazimika kutumia maji yaliyochanganyikana na tope
ambayo siyo salama kwa matumizi ya binadamu.
Kutokana na hali hiyo mbunge wa Jimbo la Solwa
alilazimika kutoa maelezo ya kina kwa wananchi hao ambapo alisema tayari
mipango ilikuwa mbioni kuhakikisha kijiji hicho cha Mwabenda na vijiji vingine
44 vinapatiwa huduma ya maji kutoka Ziwa Victoria
pamoja na umeme.
“Ndugu zangu naomba mtusamehe kwa kutowapatia taarifa juu
ya miradi hii ya maji na umeme inavyoendelea kutekelezwa katika maeneo yetu,
hivi ninavyozungumza tayari mipango ya kukipatia kijiji chenu maji kwa kuunganisha
mtandao kutoka katika bomba kuu na vijiji vingine 44 imekamilika na kazi hiyo
itaanza hivi karibuni,”
“Kiasi cha shilingi bilioni 3.6 zimeishapatikana na kazi
hii itaanza hivi karibuni niwaeleze wazi kuwa kufikia mwanzoni mwa mwezi
Novemba mwaka huu kazi itakuwa imekamilika na tatizo la maji litamalizika,
kuweni na subira,” alisema Salumu.
Hata hivyo katibu mkuu pia alimuomba mkuu wa mkoa naye
azungumze na wananchi ili awathibitishie juu ya maombi yao, ambapo mkuu huyo
aliposimama aliwatoa hofu wananchi hao kutokana na uamuzi waliouchukua wa
kuzuia msafara wa kiongozi mkuu ndani ya chama na kwamba kilichochangia hali
hiyo ni kutokuwepo kwa mawasiliano ya karibu.
“Ndugu zangu tunakuombeni radhi sana kwa kucheleweshewa kupatiwa taarifa juu
ya suala hili, ukweli ni kwamba tayari kazi ya kuwapatia maji katika kijiji
chenu iko mbioni kuanza, lakini pia suala la umeme mkandarasi kwa ajili ya
kusambaza umeme katika vijiji 10 amepatikana, hivyo kuweni na subira,” alisema
Rufunga.
Kinana aliwataka
wananchi kuwa na subira wakati serikali ya CCM ikishughulikia kero zao
mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili na kwamba Chama cha Mapinduzi kitahakikisha
ahadi ilizozitoa kwa wananchi mwaka 2010 zinatekelezwa na pale
itakaposhindikana kitaeleza sababu za kukwama. IMEANDIKWA NA CHIBURA MAKORONGO, SHINYAGA
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269