.

WAVUVI WAPATA MKONG'OTO KUTOKA KWA WANANCHI, BAADA YA KUDAIWA KUKUTWA WAKIFANYA UVUVI HARAMU

Oct 19, 2013

BUNDA, Mara
WAVUVI watatu wamenusurika kifo kwa kipigo kutoka kwa wananchi wenye hasira, baada ya kukutwa wakivua uvuvi haramu wa kutumia sumu katika ziwa Victoria wilayani Bunda, mkoani Mara,
 
Wavuvi hao waliokutwa na chupa moja ya sumu, walikamatwa na wananchi pamoja na wanajeshi wa JKT, jana usiku, wakidaiwa kuvua kwa sumu, katika eneo la kijiji cha Buzimbwe, kata ya Butimba wilayani hapa.
 
Watu hao walitambuliwa kwa majina ya Bomu Alfred Mayuya (32), John Gamba (32) na Dotto Kulwa, ambao wote ni wakazi wa mji mdogo wa Kibara wilayani hapa.
 
Diwani wa kata ya Butimba, Ngunya Msalaba, alisema jana kuwa baada ya wavuvi hao kuona wananchi pamoja na wanajeshi hao wanawafuata, waliwarushia mishale na kuwaponda kwa mawe, hali iliyopelekea kujibu mapigo kwa kufyatua risasi mbili hewani na kufanikiwa kuwakamata.
 
Msalaba alisema kuwa baada ya kuwashushia kipigo, ndipo wavuvi hao walisema kuwa wenzao wawili wamejitosa majini, na kwamba hao watatu walinusurika kifo baada ya kupelekwa kituo cha polisi Bulamba.
 
Polisi walithibitisha kukamatwa kwa wavuvi hao, ambapo wawili wamelazwa katika hospitali ya DDH-Bunda, lakini kuhusu wavuvi wawili kujitosa majini walisema kuwa hawana taarifa hiyo.
 
“Wavuvi hao kukamatwa taarifa hiyo tunayo na wawili wamelazwa lakini mmoja tunaye hapa kituoni….lakini kuhusu taarfa ya wengine wawili kujitosa majini hiyo sina” alisema afisa mmoja wa jeshi hilo ambaye hakuwa tayari kutajwa jina lake.
 
Inadaiwa kuwa wavuvi hao wamekuwa wakiendesha uvuvi haramu kwa kipindi kirefu, ambapo hivi karibuni walikamatwa na wananchi na kesi yao ikafunguliwa mahakamani.

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช