Breaking News

Your Ad Spot

Dec 23, 2013

DIWANI WA CCM AFARIKI DUNIA KWA AJALI YA PIKIPIKI YAKE

SHINYANGA, Tanzania 
DIWANI wa CCM katika kata ya Nyida wilaya ya Shinyanga mjini, Shindiko Masele (40) amekufa papo hapo baada ya kupindua na pikipiki yake aliyokuwa akiendesha.

Akizungumza na waandishi wa habari Mjini hapa, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Sosteness Ngassa alisema diwani huyo alipata ajali hiyo jana saa 2.30 usiku wakati alipojaribu kumkwepa mwendesha baiskeli na kusababisha pikipiki yake kupoteza mwelekeo na ikagonga mti uliokuwa kando ya barabara.

Ngassa alisema baada ya pikipiki hiyo kugonga mti diwani huyo alianguka chini na kufa papo hapo huku abiria aliyekuwa amebebwa aliyetambuliwa kwa jina la Silasi Ngoni alijeruhiwa kidogo kwa kupata michubuko ambapo hata hivyo alikimbizwa katika hospitali ya serikali mkoani Shinyanga alikotibiwa na kuruhusiwa.

Makamu mwenyekiti huyo alisema kifo hcho  kilichotokea ghafla  kimewasikitisha na kwamba halmashauri yake imepoteza mmoja wa viongozi muhimu na ameacha pengo ambalo halitokuwa kuwa rahisi kuzibika kwa siku za hivi karibuni.

Alisema hivi sasa wanaendelea na maandalizi ya shughuli za mazishi ambapo mwili wa marehemu ulikuwa umehifadhiwa katika hospitali ya serikali mkoani Shinyanga na kwamba iwapo mipango itakwenda kama ilivyopangwa mazishi yake yalitarajiwa kufanyika leo mchana kijijini kwake Nyida.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Annarose Nyamubi alisema amepokea kwa majonzi makubwa taarifa za kifo cha diwani huyo na kwamba alikuwa ni mmoja wa watu waliokuwa mstari wa mbele katika suala zima la uhimizaji wa maendeleo katika kata yake na usimamiaji wa utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010.

“Nimeshitushwa na taarifa za kifo cha diwani wetu wa kata ya Nyida, kwa kweli inasikitisha sana, maana ametutoka ghafla, ameacha pengo ndani ya halmashauri yetu na katika kata yake, alikuwa mstari wa mbele katika suala zima la uhimizaji wa maendeleo katika eneo lake ni wazi tutamkumbuka daima,” alisema Nyamubi.

Marehemu Masele alizaliwa mwaka 1973 wilayani Shinyanga na ameacha mjane mmoja na watoto watatu a ambapo wakati akipata ajali hiyo alikuwa akitokea Kata ya Isaka wilayani Kahama akirejea kijijini kwake Nyida.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages