Breaking News

Your Ad Spot

Dec 21, 2013

NAPE ARIDHIHSWA KUWAJIBISHWA MAWAZIRI

*Asema ni fundisho kwa watakaolala
*Ataka hatua zaidi zichukuliwe
*ziara za Kinana zimesaidia sana kutatua kero
*Bado moto wa ziara hizo haujapamba
*2015 CCM kurejesha viti  vya ubunge, Udiwani vilivyoko upinzani
NAPE NNAUYE
NA BASHIR NKOROMO
KATIBU wa NEC, Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye amesema amepokea kwa faraja kubwa, hatua ya mawaziri wanne kuenguliwa nyadhifa zao kwa ridhaa ya Rais Jakaya Kikwete.

"Najisikia vizuri, maana kwa kitendo cha mawaziri hao wanne kuchuliwa hatua, ninaamini kitasaidia wale wengine waliolala nao waamke. Bila shaka sasa hakuna atakayelala na akilala anajua itakula kwake.", alisema Nape akijibu swali la mtangazaji wa Kituo cha Televisheni cha ITV, Emmanuel Buhohela, kwenye kipindi cha 'mahijiano' cha televisheni hiyo, mjini Dar es Salaam, leo asubuhi.

Mtangazaji huyo alitaka kujua, Nape kama kiongozi wa ngazi ya juu CCM,  amejisikia au kupokeaje hatua ya Bunge

kumuomba Rais kuwawajibisha mawaziri hao wanne na kisha Rais kuridhia ombi hilo kwa kutengua uteuzi wake wa nafasi za mawaziri hao jana.

Mawaziri waliofutiwa uteuzi wao na Rais na nafasi walizotoka zikiwa kwenye mabano ni, Dk. Emmanuel Nchimbi (Waziri wa Mambo ya Ndani), Shamsi Vuai (Waziri wa Ulinzi), Mathayo David Mathayo ( Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi) na Khams Kagasheki (Maliasili na Utalii) ambaye ndiye pekee pamoja na uteuzi wake kutenguliwa na Rais lakini alitangaza kujiuzulu akiwa Bungeni, jana.


Kutenguliwa kwa uteuzi wa mawaziri hao kulitangazwa rasmi Bungeni jana jioni, na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, hatua inayoaminika kuwa imetokana na shinikizo la bunge, baada ya Kamati yake ya Kudumu ya  Ardhi, Maliasili na Mazingira kubaini 'uozo' katika operesheni iliyofanyika hivi karibuni ya tokomeza ujangili.

Chini ya Mwenyekiti wake, James Lembeli, Kamati hiyo ilieleza kwamba pamoja na mambo kadhaa iliyoyaeleza kuwa ya hovyo yaliyojitokeza kwenye operesheni hiyo, vitendo vingi ikiwemo ubakaji na udhalilishaji vilifanyika ambapo ni kinyume na utu na haki za binadamu.

Kufuatia kadhia hiyo, Kamati hiyo kupitia kwa Lembeli, iliwataka mawaziri wanaohusika kutazama kama wanafaa kuendelea na nyadhifa zao au wajiuzulu, na pia Kamati hiyo ikaenda mbali zaidi kwa kumuomba Rais Jakaya Kikwete kuchukua hatua ya kuwawajibisha.

Akizungumzia zaidi hatua hiyo, Nape alisema, pamoja na mawaziri hao kuwajibika, lakini ipo haja ya kwenda mbali zaidi kwa kutazama mifumo na sheria zilizopo sasa kwa kuwa inaonekana navyo ni miongoni mwa vyanzo vya vikwazo katika utekelezaji wa utawala bora.

"Kwa mfano leo hii, mawaziri wameng'oka, sawa ni jambo jema, sitetei, lakini inawezekana kabisa kuna mifumo na sheria ambazo zilimkwaza Waziri huyu kutimiza wajibu wake. Mfano, alihitaji kumfukuza mtu kazi kwa kuzembea jambo fulani, lakini malmaka ya kufukuza kazi mtumishi yapo kwa Katibu Mkuu wa Wizara, hapa atafanyaje!", alisema Nape na kuongeza;

"La msingi hapa ni lazima sasa hatua hizi ziende mpaka chini huku kwa watendaji, ili isiwe mawaziri wanawajibishwa tu kwa sababu ya dhamana zao za kusimamia kisiasa, huku watendaji wanazidi kuvuta shuka bila hofu wakati baadhi yao ni sehemu ya matatizo".

Akijibu swali kuhusu ziara za Katibu Mkuu na sekretarieti ya CCM mikoani, Nape alisema, ziara hizo ndiyo kwanza zimeanza, na mado moto wake mkubwa zaidi unakuja hasa itakapokaribia uchaguzi mkuu wa 2015.

Nape alisema, ziara hizo, zimeonyesha matunda makubwa sana, klwa kuwa zimesaidia kupunguza kero nhyingi katika maeneo zilikofanyika.

Alitoa mfano wa ziara hiyo ilivyoweza kuondoa msongamano wa malori wilayani Tunduma mkoani Mbeya, akisema kwamba wakati Kinana na msafara wake wanaingia tunduma walikuta msongamano ni mkubwa sana kutokana na wafanyakazi wanaohudumia malori hayo kufanya kazi kwa mda mfupi.

"Baada ya kuiagiza serikali isimamie wafanyakazi wa eneo hilo wafanya kazi kwa saa 24, kwa zamu, siku ya pili yake ya agizo hilo, msongamano ulionekana kupungua sana na kuleta nafuu kwa madereva na wafanya biashara kwa jumla pale Tunduma", alisema Nape.

Nape alisema, pia kutokana na ziara hizo, mgogoro uliokuwa mkubwa baina ya wananchi na wenye mgodi wa machimbo Nyamongo, umepungua kwa asilimia 90 sasa, na hali imekuwa ya kuridgisha sana.

Akizungumzia wabunge wanaodaiwa kulipwa posho bila kuzifanyia kazi, Nape alisema, kurudisha fedha pekee hakutatosha, kwa upande wa CCM ambayo ndiyo yeneye wabunge wengi itabidi ichukue hatua zaidi dhizi ya waliohusika na kadhia hiyo bila kuoneka mtu.

Kuhusu ajira kwa vijana, Nape alaisema ili kutimiza hilo, ni lazima viwanda vifufuliwe kwa dhati kabisha, ikiwa ni kuchukua hatua za kuwanyang'anya wawekezaji waliochukua viwanda mbalimbali kwa lengo la kuviendeleza lakini baadhi yao majengo ya viwanda hivyo wakayafanyia shughuli zingine tofauti ikiwemo kuyageuza maghala.

Nape aliitaka pia serikali kupunguza au kuondoa kabisa urasimu katika kupokea wawekezaji katika sekta mbalimbali za uchumi hapa nchini akisema, kwamba, kwa sasa vikwazo na urasimu bado ni vingi sana kiasi kwamba wawekezaji waanakwazika na hivyo kupunguza kasi ya uwekezaji ambao wakiongezeka haraka ajira kwa vijana nazo zitakua haraka.

Alisema, hatua ya sasa inayofanywa na CCM kusimamia serikali ni ya kawaida kabisa kwa kuwa kazi hiyo haipaswi kufanya na wapinzani kwa kuwa sera inayotekelezwa siyo yao, na wahaijui.

Nape aliahidi kwamba katika uchaguzi zijazo CCM itakomba viti vyote vya ubunge na udiwani vililivyopo sasa chini ya wapinzani, akisema, kwamba, baada ya wapinzani kujaribiwa wameshindwa kuonyesha matunda yoyote ya kusaidia wananchi na hivyo kutokuwa mbadala wa CCM.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages