Breaking News

Your Ad Spot

Jul 17, 2014

CCM KUZIPITIA MWEZI UJAO ADHABU ILIZOWAPA WAWANIA URAIS, YARIDHISHWA NA MAZUNGUMZO YA VYAMA CHINI YA MSAJILI WA VYAMA

NA BASHIR NKOROMO
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema, mwezi ujao, kitafanya mapitio  ya utekelezaji wa adhabu walizopewa baadhi ya wanachama kwa kukia  taratibu za kuwania Urais, ikiwemo kujitangaza mapema.

Kimesema, Kamati ya Usalama na Maadili ya Chama itafanya mapitio ya  mwenendo wa utekelezaji wa adhabu walizopewa na Kamati Kuu  mapema mwaka huu, na kama itabainika kuwa hawatekelezi ipasavyo  masharti ya adhabu zao, itapendekeza kwa Kamati Kuu kuongezwa kwa  adhabu kulingana na ukubwa wa uvunjaji wa masharti ya adhabu  husika.


     Hayo yamesemwa leo, na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape  Nnauye, akieleza maamuzi yaliyofikiwa katika Kikao cha Kamati Kuu ya  CCM, kilichofanyika jana, mjini Dar es Salaam, chini ya Mwenyekiti wa  CCM, Rais Jakaya Kikwete.


    "Kamati Kuu ilipokea taarifa za harakati za baadhi ya wanachama wa  CCM walioonesha nia ya kuomba ridhaa ya CCM kugombea Urais.  Baada ya kutafakari kwa kina, Kamati Kuu inapenda kuwakumbusha  wote kuwa ili wasipoteze sifa za kugombea, ni muhimu wakazingatia  Katiba, Kanuni na taratibu za Chama zinazosimamia masuala hayo",  amesema Nape na kuongeza.


    Nape alisema, ni muhimu wanachama wote wakakumbuka kuwa Chama  ni pamoja na Katiba, Kanuni na taratibu zake, hivyo kutoziheshimu na  kuzifuata ni kukivuruga, jambo ambalo halivumiliki.


    Alisema, nia ya CCM kusimamia hayo ni kuhakikisha Chama kinakuwa  na umoja na mshikamano ambao ni muhimu sana, hasa Chama  kinapoelekea kukamilisha kazi ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya  CCM ya 2010/2015 na Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.


     Nape alisema, pia kikao hicho cha Kamati Kuu, kilipokea taarifa ya  mazungumzo yanayoendelea kati ya CCM kwa upande mmoja na  CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi kwa upande wa pili.


    Alisema, mazungumzo hayo yanayosimamiwa na Msajili wa Vyama vya  Siasa nchini Jaji Francis Mutungi yana lengo la kuangalia kwa kina ni  kwa nini baadhi ya wajumbe wachache wa Bunge Maalum la Katiba  walisusia na kutoka nje katika awamu ya kwanza ya Bunge hilo, na  kuangalia namna watakavyorudi ili kukamilisha mchakato wa mabadiliko  ya Katiba nchini.


     Nape alisema, kwa ujumla Kamati Kuu ya CCM imeridhishwa na  mwenendo wa mazungumzo hayo na kupongeza juhudi hizo  zilizofanywa na Msajili wa Vyama vya Siasa na Vyama husika.


    "Kamati Kuu inapenda kueleza imani yake kuwa mazungumzo hayo  yatazaa matunda kwa wajumbe wachache waliosusia Bunge Maalum la  Katiba, kurejea Bungeni na kumalizia sehemu ya mchakato uliobakia.  Kamati Kuu inayatakia kila la kheri mazungumzo hayo", alisema Nape.


     Aidha, Kamati Kuu imewatakia kheri na fanaka Watanzania wote wakati  huu wanapomalizia mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages