KATIBU Mkuu wa CCM Ndugu. Abdulrahaman Kinana , amekipongeza Chama Cha ZANU PF Cha Zimbabwe kwa kusimama imara licha ya Changamoto mbalimbali zinazoikabili Zimbambwe ikiwemo vikwazo vya kiuchumi ambavyo vimewekwa dhidi ya nchi hiyo.
Taarifa iliyotumwa na Ofisa wa Makao Makuu ya CCM, Edward Mpogolo, imesema, Ndugu Kinana (pichani) amewataka wana ZANU PF kuendelea kuunga mkono chama chao na kuongeza mapambano dhidi ya maadui wote wanaotaka kurudisha nyuma jitihada za kupigania maslahi ya nchi yao.
Taarifa imesema, akisoma salamu za mshikamano za Chama Cha Mapinduzi kwenye mkutano Mkuu wa ZANU PF unaofanyika mjini Harare Ndugu Kinana aliwakikishia wana ZANU PF na wana Zimbabwe wote kuwa katika mapambano hayo CCM iko nyuma yao na kwamba haitaacha kupaza sauti dhidi ya vikwazo vya uchumi ilivyowekewa Zimbabwe.
Alisema vikwazo hivyo si halali uhalali na kwa ujumla wake vinatoa adhabu isiyo ya haki kwa Wananchi wa Zimbabwe wasio na hatia.
Ndugu Kinana, alimpongeza Rais Mugabe ujasiri na kwa msimamo wake usioyumba wa kupigania maslahi ya wana Zimbabwe licha ya vitimbi vya wapiga maendeleo.
Alisema ujasiri na msimamo wa Mugabe pamoja na Chama anachokiongoza Cha ZANU PF ndiyo uliowezesha Zimbabwe kusimama ilivyo hivi sasa kama Taifa huru na lisilikubali kuyumbishwa.
Alisema Mugabe na Chama chake wameonyesha kwa mfano kwamba kumbe watu wakisimama imara chini ya uongozi wa chama imara hakuna anayeweza kukwamisha nyendo zao za kimapinduzi zinazoendana na matakwa ya umma.
Akizungumzia ushindi wa kishindo wa ZANU PF kwenye uchaguzi Mkuu June mwaka jana Kinana alisema hicho ndicho kiashiria cha kukubalika kwa Chama na sera zake.
Alisema CCM inaipongeza ZANU PF kwa ushindi huo na kwamba wana CCM wanajisikia fahari sana wanapoona ZANU PF ikiendelea kukua na kuimarika.
Aidha Ndugu. Kinana alimpongeza Rais Mugabe na kueleza kuwa CCM na Watanzania kwa ujumla wanafurahishwa na msimamo wa dhati alionyesha Rais Mugabe katika majukwaa mbalimbali ikiwemo mkutano wa wakuu wa nchi za SADC uliofanyika Victoria Falls wa kueleza umuhimu wa kutambua na kuheshimu mchango wa Mwalimu Nyerere katika ukombozi wa Afrika na hasa kusini mwa Afrika.
Hotuba ya Ndugu Kinana ilipokelewa kwa shangwe na furaha kubwa sana na wajumbe wa mkutano huo ambao mara kwa mara walishangalia kuashiria kuridhika na kauli za kimapinduzi na kidugu kutoka kwa wana CCM.
Ndugu Kinana na ujumbe wake wataondoka kesho kureke nyumbani. Ujumbe wa Katibu Mkuu kwenye mkutano ulimhusisha pia Mjumbe wa halmashauri Kuu ya Taifa CCM Ndg. Phares Magesa na afisa wa makao makuu ya CCM Ndg. Thobias Mwilapwa.
Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu Abdulrahman Kinana akihutubia katika Mkutano Mkuu wa Chama Cha Ukombozi cha ZANU-PF cha Zimbabwe mjini Harare. |
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269