Breaking News

Your Ad Spot

Feb 22, 2015

BALOZI SEIF IDDI : JUKUMU KUBWA LA VYUO VYA ELIMU YA JUU NCHINI NI KUTOA TAALUMA INAYOLENGA KURAHISISHA UTEKELESAJI WA MIPANGO YA MAENDELEO YA TAIFA

Balozi Seif Iddi: Jukumu kubwa la Vyuo vya Elimu ya Juu nchini ni kutoa taaluma inayolenga kurahisisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Taifa

Wahitimu wa Chuo cha Elimu ya Baishara Pemba wakiandamana kuingia katika uwanja wa Michezo wa Chuo cha Amali Vitongoji kwa ajili ya Hamafali yao baada ya kumaliza mafdunzo yao ngazi ya Cheti.
Wahitimu wa Chuo cha Elimu ya Biashara Pemba wakiwa tayari kuthibitishwa kukamilisha mafunzo yao na kupewa vyeti vyao kwenye mahafali yao ambapo mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi. 
Baadhi ya wahitimu wa Chuo cha Elimu ya Biashara Pemba wakifuatilia matukio mbali mbali kwenye mahafali yao iliyofanyika katika viwanja vya Chuo cha Amali Vitongoji Chake chake Pemba. 
Mohammed Suleiman Khalfan akipokea tuzo na fedha taslim kutoka kwa Balozi Seif baada ya kuwa Mwanafunzi Bora wa Fani ya Hesabu katika chuo cha Elimu ya Biashara Pemba. 
Balozi Seif akimzawadia Tuzo na Fedha Taslim Mwanafunzi Bora wa Fani ya Mawasiliano ya Umma wa Chuo cha Elimu ya Biashara Pemba Nassor Mussa Khamis kwenye mahafali ya chuo hicho hapo Vitongoji Chake Chake Pemba.
Balozi Seif akiwa katika picha ya pamoja na Uongozi wa Bodi ya chuo cha elimu ya Baishara pamoja na Serikali Mkoa wa Kusini pemba mara baada ya kukamilika kwa mahafali ya kwanza ya chuo hicho. Kulia ya Balozi Seif ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo akiwa pia Mkuu wa Wilaya ya Mkoani Nd. Hemed Suleiman Abdullah, Mkuu wa Chuo hicho Abdulwahab Said Abubakari na Mhadhiri wa chuo hicho Moh’d Said. Kushoto ya Balozi Seif ni Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mh. Mwanajuja Majid na Mkuu wa Wilaya ya Chake chake Bibi Hanuna Ibrahim Masoud. 
Balozi Seif akiwa katika Picha ya pamoja na Uongozi na wahadhiri wa chuo cha elimu ya Biashara Pemba mara baada ya kukamilika kwa mahafali ya kwanza ya chuo hicho tokea kilipoanzishwa Januari 2014. (Picha zote na Hassan Issa– OMPR – ZNZ)

Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
22/2/2015.
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba jukumu kubwa  la Vyuo vya Elimu ya juu hapa nchini ni kutoa Taaluma inayolenga kurahisisha utekelezaji wa mipango ya Maendeleo ya Taifa pamoja na Jamii kwa ujumla.

Alisema fikra za kupanua wigo katika kuongeza fani ya teknolojia ni muhimu zaidi kwa vile itasaidia vijana kuweza kuendana na wakati wa sasa wa mabadiliko ya Sayansi na teknolojia.
Balozi Seif alieleza hayo kwenye  mahafali ya kwanza ya chuo cha elimu ya Biashara Pemba yaliyofanyika katika viwanja vya chuo cha Amali kiliopo Vitongoji  Wilaya ya Chake chake Mkoa wa Kusini Pemba.

Alikishauri chuo hicho kuangalia namna ya kujiunga na Taasisi mbali mbali za Kimataifa za Elimu ili kujiimarisha zaidi pamoja na kupata fursa za kubadilishana uzoefu na utaalamu miongoni mwa walimu na wanafunzi.

Balozi Seif alisema zipo Taasisi nyingi za kielimu Duniani ambazo chuo cha Elimu ya Biashara Zanzibar kinaweza kushirikiana nazo ili kupiga hatua za haraka kitaaluma sambamba na kuliongezea Taifa Wataalamu watakaosaidia taasisi za umma na hata zile Binafsi.

“ Mnaweza kushirikiana na taasisi kama vile Association of Business Excutives        { ABE }, Chartered Institute ofManagement { CIMA } za Uingereza, Institute of Hospitality { IH }  na Association of Information Technology Professionals { AITP } za Marekabi “. AlisemaBalozi Seif.

Alihimiza kwamba ufundishaji wa chuo hicho uelekezwe katika kutoa mchango na rai tofauti zitazochangia na kurahisisha utekelezaji wa mipango ya Serikali ikiwemo Dira ya Maendeleo ya 2020,MKUZA 11, pamoja na malengo ya Milenia.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi wa chuo cha Elimu ya Baishara kwa uamuzi wake  wa busara wa kuanzisha kwa mara ya  kwanza chuo Binafsi ambacho Makao Makuu yake yapo Pemba wakati jamii imezoea kuona Matawi ya vyuo vya elimu ya juu ndio yanayofunguliwa Kisiwani humo.
Alisema uamuzi wao umepelekea vijana wengi Kisiwani Pemba kupata fursa za kujiunga na mafunzo ya elimu kwa gharama nafuu tofauti na ile wanayotoa wakati wanapoamua kufuatia masomo hayo Unguja au Tanzania Bara.

“ Kuna Gharana ya usafiri, chakula na malazi ambazo zinakuwa kubwa na wengine wanashindwa kuzimudu, lakin i uwepo wa fursa hizo nyumbani baadhi ya gharama zinapunguwa na nyengine kuondoka kabisa na hivyo kuwafanya wanafunzi kusoma kwa utulivu “. Alisisitiza Balozi Seif.
Akizungumzia suala la ajira Balozi Seif alifahamisha kwamba chuo cha elimu ya Biashara kitakuwa na mchango mkubwa katika Taifa la Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kuzalisha vijana bora kielimu ili kuweza kukabiliana na ushindani wa ajira ndani ya Jumuiya hiyo.

Alisema wapo vijana wengi wanaomaliza masomo yao ya sekondari ya vyuo lakini jamii inapaswa kuamini kwamba Taifa linakabiliwa na tatizo kubwa la soko la ajira pamoja na soko la biashara linalokabiliwa na changamoto kadhaa Duniani.
Balozi Seif alisema ushindani katika soko la ajira utaongezeka kutokana na  Mataifa ya jumuiya ya Afrika Mashariki na soko la pamoja kuelekea kwenye Umoja wa Kisiasa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  aliwaomba wahitimu wa Chuo cha Elimu ya Biashara Pemba waendelee kutafuta Taaluma zaidi kwa vile Taifa linawategemea. Hivyo wanapaswa kujituma zaidi kwa lengo la kuchangia Maendeleo ya Taifa.
Aliwaasa wahitimu hao kuelewa kwamba maendeleo ya Taifa yatachangiwa na jitihada zao kwa vile hakuna Mjomba wa kuja kuwafanyia kazi kuwaletea maendeleo. Kazi hiyo watalazimika kuitekelza wao wenyewe.

Akisoma Risala ya Chuo cha elimu ya Biashara Pemba Mkuu wa Cuo hicho Bwana Abdulwahab  Said Aboubakar alisema lengo la kuanzishwa kwa chuo hicho Januari mwaka 2014 ni kutoa elimu ya Biashara kwa Vijana `ili waweze kujinasua  katika tatizo la ajira.
Alisema Uongozi wa chuo hicho pia umezingatia katika mambo ya msingi yaliyotiliwa mkazo zaidi ni pamoja na kutoa ushauri katika fani ya biashara kwa taasisi na hata jumuiya za kiraia ndani na nje ya nchi.

Mkuu huyo wa Chuo cha Elimu ya Biashara Pemba aliwashukuru washirika wa chuo hicho waliochangia kufanikisha uanzishwaji wa chuo hicho ambacho kitakuwa mkombozi kwa wananchi wa Kisiwa cha Pemba katika masuala ya Biashara.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Elimu ya Biashara Pemba ambae pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mkoani Nd. Hemed Suleiman Abdulla alisema kulikuwa na changamoto kubwa sana wakati wa uanzishwaji wa chuo hicho likiwemo tatizo la ukosefu wa Majengo.

Nd. Hemed alisema ni faraja iliyoje kwa wananchi wa Kisiwa cha Pemba hasa Vijana kupata fursa `baada ya kuanzishwa kwa chuo hicho ambayo itawapunguzia gharama za masomo pamoja na makaazi wakiwa nje ya Pemba.

Makamu Mwenyekiti huyo wa Bodi ya chuo cha elimu ya Biashara aliwashauri Viongozi wa Serikali na hata Taasisi za kiraia kuwaruhusu wafanyakazi wao kupata Taaluma katika chuo hicho ili kuongeza uwezo wa kazi kitaaluma.

Akimkaribisha mgeni rasmi katika mahafali hayo ya kwanza ya chuo cha elimu ya Biashara Pemba Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mh. Mwanajuma Majid alieleza kwamba fani ya taaluma ndani ya Kisiwa cha Pemba ilikuwa na ukwasi Mkubwa.
Mh. Mwanajuma alisema wananchi wa Pemba hasa Vijana na Wanafunzi sio kwamba walikuwa hawahitaji kupata elimu ya juu lakini kilichokuwa kikiwakabili ni  changamoto ya gharama za masomo na malazi wakati wakiwa nje ya Kisiwa hicho.
Mahafali  hayo ya kwanza ya chuo cha elimu ya Biashara Pemba yamejumuisha Wahitimu 133 wa ngazi ya Cheti katika fani Tano ambazo ni Uhasibu, Usimamizi wa Biashara, Uongozi wa Rasilmali Watu, Manunuzi na Ugavi pamoja na Mawasiliano ya Umma.

Balozi Seif Katika mahafali hayo alipata futrsa ya kutoa  tuzo na fedha taslim kwa wahitimu waliofanya vizuri zaidi kwenye mitihani yao ambao ni Mohammed Suleiman Khalfan Hesabu, Rashid Ali Rashid Usimamizi wa Biashara na Rehema Ali Haji Manunuzi na Ugavi, Kassim Juma Rasilmali Watu pamoja na Nassor Mussa Khamis Mawasiliano ya Umma.

Chuo cha Elimu ya Biashara Pemba kinachotumia Majengo ya kukodi na kikiwa katika harakati za kujenga majengo yake ya kudumu hivi sasa kina Wanafunzi wapatao 175 kati yao asilimia 64.8% ni Wanawake ikiwa juu zaidi ya Wanafunzi Wanaume ipatayo  asilimia 58.2%.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages