Mwanafunzi
wa darasa la tano katika shule ya msingi Ilola iliyopo katika wilaya ya
Shinyanga mkoani Shinyanga Veronica Venance(12) amefariki dunia kwa
kupigwa na mwanafunzi mwenzake wakati wakigombania daftari darasani kwa
ajili ya kuandika dondoo (notes).
Tukio
hilo limetokea Februari 24 ,mwaka huu saa 7 na nusu mchana katika
darasa la tano shule ya msingi Ilola iliyopo katika kata ya Ilola tarafa
ya Itwangi wilaya ya Shinyanga.
Walioshuhudia
tukio hilo walisema mwanafunzi huyo aliyekuwa anasoma darasa la tano
alifariki dunia baada ya kupigwa makofi na ngumi sehemu za kichwani na
mwanafunzi mwenzake aitwaye Sophia Mathew(12) ambaye pia ni mwanafunzi
wa darasa la tano katika shule hiyo kutokana na ugomvi uliotokana na kugombania daftari.
Akizungumza
na Malunde1 blog, afisa mtendaji wa kata ya Ilola Mahona Joseph alisema
tukio hilo lilitokea wakati wanafunzi hao wakigombania daftari ambapo
marehemu alikuwa ameng’ang’ania daftari aliloazima kwa mwanafunzi
mwenzake Sophia Mathew kwa ajili ya kuandika dondoo za daftari hilo.
Alisema
kitendo cha kung’ang’ania daftari hilo wakati siyo mali yake kilimkera
mwanafunzi mwenzake na kuzua ugomvi kati ya wanafunzi hao na kubababisha
kifo cha mwanafunzi huyo.
Naye
mwalimu mkuu wa shule ya msingi Ilola Magere Jonas aliiambia malunde1
blog kuwa tukio hilo lilitokea wakati wanafunzi hao wakigombana darasani
na kwamba huenda mwanafunzi huyo aliumia kisogoni baada ya kuanguka
wakati wa ugomvi huo.
“Ilikuwa
muda wa saa saba mchana wakati wanafunzi wengi wameenda kula wengine
wakiwa bado wako shuleni,walimu walikuwa majumbani lakini mimi na
mwalimu mkuu msaidizi tulikuwa chini ya mti tunapunga upepo,mara akaja
mwanafunzi mmoja akasema kuna wanafunzi wanagombana darasani, ndipo
tukaenda na kumkuta amelala chali darasani” alisimulia mwalimu mkuu.
“Kufuatia
hali hiyo tukachukua jukumu la kumpeleka kwenye zahanati ya Ilola
ambapo nesi akatushauri kwenda kituo cha afya cha Bugisi kutokana na
hali mbaya aliyokuwa nayo mwanafunzi huyo lakini tulipofika Bugisi
tukaambiwa tayari ameshafariki dunia,tunahisi pengine aliumia
kisogoni”,alieleza mwalimu Jonas.
Kaimu
kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Longinus Tibishubwamu alisema
wanamshikilia mtuhumiwa Sophia Mathew anayedaiwa kumpiga Veronica
Venance sehemu za kichwani kwa kutumia mikono yake.
Na Kadama Malunde-Shinyanga
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269