Mwenyekiti
Mtendaji wa kampuni ya Forward Formidable Enterprises (FFE) inayoandaa
tamthilia mpya na ya kisasa ya “A boys mission” Johnson Lujwangana
katikati akifafanua jambo kuhusiana na tamthilia hiyo itakayoanza
kurushwa kwenye vituo vya televisheni kuanzia mwezi septemba. Wengine
katika picha kutoka kushoto ni Brian daniel, Neema Mung’anya, Samuel
katabazi, Jesca haule, Aisha bakari na Victor Casmir.
Waigizaji wa tamthilia ya “A boys mission” inayoandaliwa na kampuni ya Forward Formidable Enterprises katika picha ya pamoja.
………………………………………………………………………………………..
Na Mwandishi wetu
Kampuni mpya katika utengenezaji
wa filamu nchini, Forward Formidable Enterprises (FFE) inayoandaa
tamthilia mpya na ya kisasa ya “A boys mission” inahitaji kiasi cha Sh
milioni 800 ili ikamilike.
Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni ya
FFE, Johnson Lujwangana alisema kuwa kwa sasa wameweza kutengeneza toleo
la utangulizi “pilot episode’ kwa ajili ya kuonyesha nini wanakifanya
huku kila kitu kikiwa tayari kwa ajili ya kurekodiwa.
Johnson alisema kuwa tamthilia yao
inazungumzia changamoto na suluhisho mbalimbali kwa maisha ya vijana
nchini na fedha hizo zinahitajika kwa ajili ya kughalimia gharama
mbalimbali za kuzalisha rasmi tamthilia hiyo.
Baadhi ya gharama hizo kwa mujibu
wa Johnson ni kulipa mtayarishaji bora, kuwalipa wasanii fedha kutokana
na ubora wa kazi zao, kulipia vifaa vya kisasa, kulipa sehemu bora ya
kurekodi tamthilia, usafiri, chakula na gharama nyinginezo.
“Kama msanii wa muziki wa kizazi
kipya, Diamond anatengeneza video ya dakika tatu kwa Sh Milioni 60, kwa
nini tamthilia ambayo kila sehemu (episode) inatumia si chini ya dakika
45 hisifikia kiwango hicho cha fedha? Alihoji Johnson.
Alisema kuwa wao wanataka
kuwafaidisha wasanii wao kwa kuwalipa vizuri na kuendelea kudumu katika
fani na kuwataka wadhamini kujitokeza kwa wingi kusaidia mradi huo.
“Hakuna hata msanii mmoja maarufu
katika tamthilia hii, lengo si kama kuwatupa wasanii hao, bali ni
kupanua wigo na kuwapa nafasi wasanii wengine, nataka kizazi kipya zaidi
katika tasnia ili kuendeleza kuzalisha mastaa,” alisema.
Alisema kuwa katika tamthilia
imeonyesha na kutoa majibu ya nini vijana wanatakiwa kufanya hapa nchini
na kuachana na fikra za kukimbilia nje ya nchi kwa kudhani kuwa ndiko
kutakuwa suluhisho la matatizo yao.
Alifafanua kuwa mara baada ya
kufika huko, hali inakuwa tofauti na kukutana na changamoto nyingi zaidi
za maisha na kuwaza kurejea nchini.
“Tamthilia ni ya kisasa zaidi
kwani lengo letu pia ni kuonyeshwa nje ya nchi na kuonyesha madhari ya
kuvutia ya jiji letu la Dar es Salaam na kupromoti mji wetu tofauti na
hali iliyozoeleka kwani tamthilia nyingi uonyesha maisha ya vijijini,”
alisema Johnson.
Alifafanua kuwa kwa kuonyesha
usafi wa mji, maeneo mbalimbali ya starehe ya hapa nchini, kutawavutia
hata wasanii watayarishaji wa tamthilia nje ya nchi kuja kutayarishia
kazi zao hapa nchini.
Alisema kuwa tamthilia hiyo ina
jumla ya sehemu 12 ambapo katika kila sehemu, muigizaji mkuu ma maudhui
ya tamthilia pia yanabadilika.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269