Breaking News

Your Ad Spot

Feb 20, 2015

WAZIRI MKUU ATAKA WATANZANIA WAWE NA HOFU YA MUNGU

images 
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewataka Watanzania wasikilize na kufuata mafundisho yanayotolewa na viongozi wa dini ili Tanzania iwe nchi yenye watu waadilifu na wenye hofu ya Mungu.
Ametoa wito huo leo mchana (Ijumaa, Februari 20, 2015) wakati akizungumza na maelfu ya waumini na wananchi waliohudhuria ibada ya mazishi ya Askofu Mstaafu Magnus Mwalunyungu kwenye kanisa la Moyo Mtakatifu wa Yesu la Tosamaganga, Jimbo Katoliki la Iringa.
“Leo ni siku ya pekee ya kuwasikiliza viongozi wa dini wakituasa tujiandae kwa maisha baada ya kifo. Tukio hili la leo litupe nguvu ya kukubali kwamba kifo kipo licha ya kuwa hakizoeleki na kinapotokea kinaleta simanzi kubwa,” alisema.
“Ninawasihi Watanzania wote tufuate mafundisho yanayotolewa na viongozi wa dini zetu ili Tanzania iwe na kundi la watu wenye hofu ya Mungu, waadilifu na wanyofu kama ambavyo mahubiri ya leo yamesisisitiza,” alisema.
Waziri Mkuu ambaye yuko kwenye ziara ya siku tano ya kikazi mkoani Iringa, aliamua kusitisha ziara yake siku ya leo ili aweze kushiriki msiba huo. Pia alitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete ambaye yuko Kenya kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Akitoa mahubiri kwenye ibada hiyo, Askofu Damian Dallu wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea alisema wanadamu wanahangaika na kuogopa kifo kwa sababu hawajui baada ya kifo maisha yao yatakuwaje.
“Askofu Mwalunyungu ameishi kwa miaka 85 na kati ya hiyo, miaka 55 alikuwa akitumikia kama padre na kwa miaka 22 alimtumikia Mungu aakiwa Askofu. Na hata baada ya kustaafu aliomba awe Parokopale Kidamalai ambako alitumikia kwa miaka minne. Maisha yake yanaendana na neno kutoka kitabu cha hekima kwamba kifo cha mwadilifu ni kupumzika kwa starehe,” alisema.
Ibada hiyo ya mazishi ilihudhuriwa na Maaskofu wa kanisa katoliki zaidi ya 20.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages