Fundi Mkuu katika Kiwanda cha
Sabuni cha Gereza Kuu Ruanda, Mbeya Sajin wa Magereza, George akitoa
maelezo ya aina za Sabuni zinazotengenezwa katika mradi wa Sabuni Gereza
Kuu Ruanda, Mbeya kama zinavyoonekana katika picha.
Sabuni za kufulia zenye miche
minene mirefu(Big Bars) zinazotengenezwa katika Kiwanda cha Sabuni cha
Gereza Kuu Ruanda, Mbeya zikiwa tayari kupelekwa kwa watumiaji.
Muonekano wa Sabuni ya kufulia
ikiwa bado haijawekwa kwenye mashine maalum ya kukatia vipande vyenye
ukubwa tofauti tofauti. Kwa wastani Kiwanda hicho kinauwezo wa kuzalisha
katoni 150 hadi 200 kwa siku.
…………………………………………………………………………………………………………………………
Na Lucas Mboje, Mbeya
Kamishna Jenerali wa Magereza
Nchini, John Casmir Minja amepongezwa kwa kukifufua Kiwanda cha
utengenezaji Sabuni za aina mbalimbali Gereza Kuu Ruanda, Mbeya.
Pongezi hizo zimetolewa na Maofisa na Askari wa Magereza
Mkoani Mbeya kutokana na kukiwezesha Kiwanda hicho vifaa na malighafi za
utengenezaji sabuni hivyo kukifanya Kiwanda hicho kizalishe sabuni za
kutosha kwa Wafungwa waliopo Magerezani Tanzania Bara.
“Tunampongeza sana Kamishna Jenerali Minja hususani kwa
kukiwezesha Kiwanda chetu vifaa vya utengenezaji sabuni. Tunaamini
kutokana na kasi ya utendaji wake wa kazi ataendeleza juhudi za kukiunga
mkono Kiwanda hiki ili kiweze kukidhi mahitaji halisi ya soko la ndani
na nje.” Walisikika wakisema.
Kiwanda cha Uzalishaji sabuni cha Gereza Kuu Ruanda, Mbeya ni
miongoni mwa miradi 23 iliyopo chini ya Shirika la Magereza(Prison
Corporation Sole) ambapo mradi huu ulianza shughuli zake za Uzalishaji
sabuni mnamo Mwaka 1978.
Madhumuni ya kuanzishwa kwa mradi huu yalilenga zaidi kutimiza
majukumu ya msingi ya Jeshi la Magereza hususani utekelezaji wa Programu
ya Urekebishaji wa Wafungwa kwa kuwafundisha
utengenezaji wa sabuni pia kiwanda hicho kinajiendesha kibishara hivyo kuchangia pato la Taifa.
Kiwanda hicho kinatengeneza Sabuni za aina mbalimbali zikiwemo
Sabuni za kufulia zenye miche minene na mifupi, sabuni za kuongea,
sabuni za maji kwa ajili ya usafi majumbani pamoja na sabuni za chenga
chenga(flex soap).
Malighafi zinazotumika katika Kiwanda hicho ni caustic soda,
mafuta ya mawese na mafuta ya mise ambayo hupatikana kwa wingi Wilayani
Kyela, Mkoani Mbeya. Kwa wastani Kiwanda hicho kinauwezo wa kuzalisha
katoni za sabuni 150 hadi 200 kwa siku.
Tangu kuanzishwa kwa mradi huu kwa kiasi kikubwa kimechangia
utoaji elimu ya Ufundi Stadi kwa vitendo kwa Wafungwa katika fani ya za
utengenezaji wa sabuni ambapo kuna Wafungwa wengi wamenufaika kupitia
mradi huu na wameweza kuanzisha shughuli zao baada ya vifungo vyao
kukoma.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269