Serikali ya Kenya imeutambua rasmi mwili
wa jamaa mmoja uliopatikana katika mbuga ya wanyama, kuwa ni wa shahidi
wa mahakama ya ICC, Meshack Yebei, katika kesi inayomkabili makamu wa
rais wa Kenya, William Ruto.
Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari, uchunguzi wa chembechembe za DNA umehakikisha fika kuwa ni yeye.
Tangazo hilo linatarajiwa kuipa afueni
familia ya Yebei, ambayo nusura izike mwili tofauti mnamo mwezi Januari,
kabla ya kuambia kwamba mwili huo haukuwa wa mtoto wao.
Mwanachemia wa serikali ya Kenya
hatimaye ametangaza kuwa mwili Fulani ambao umelala kwenye chumba cha
kuhifadhia maiti tangu mwezi Desemba ni wa Meshack Yebei.
Bwana Yebei alitarajiwa kuwa shahidi wa
mshtakiwa kwenye kesi dhidi ya Makamu wa Rais wa Kenya, William Ruto,
anayekabiliwa na mashtaka ya mauaji katika mahakama hiyo ya kimataifa
huko Hague.
Gazeti moja la Kenya limemnukuu afisa wa
uchunguzi akisema kwamba chembechembe za DNA zimedhibitisha kwamba
mwili huo uliopatikana ni wa Yebei.
Matokeo haya ni sambamba na yale yaliyochapishwa na daktari mmoja wa Afrika Kusini aliyepewa kazi hiyo na familia.
Inatarajiwa kuwa serikali sasa itafanya uchunguzi wa pili kugundua kilichosababisha kifo chake.
Inasemekana kwamba Meshack Yebei
alitekwa nyara mwishoni mwa mwezi Desemba nyumbani kwake Eldoret
alipokwenda kumwona mkewe ambaye alikuwa anaugua.
ICC imefichua kuwa marehemu alipewa nafasi ya kupata ulinzi na makazi salama lakini akakataa.
Mwezi Januari mwili ulioharibika vibaya
ulipatikana katika mto ulio takriban kilomita arobaini kutoka nyumbani
kwake, na familia ikadhani kuwa ni yeye.
Lakini uchunguzi wa DNA ukaonyesha kuwa ni mwili wa mtu mwengine ambaye pia alitoweka wakati huo huo.
Kufikia wakati huo familia yake tayari
ilikuwa inalalamika kuwa kutoweka kwake Yebei kunatokana na kuhusishwa
na kesi hiyo nyeti.
Ufumbuzi huu sasa unaibua maswali mapya.
Mbuga ya Wanyama ya Tsavo, ambako mwili
huo ulipatikana, iko takriban kilomota mia sita kusini mashariki mwa
Eldoret alikotoweka.
Aidha familia yake imelalamika kuhusu
muda ambao serikali imechukua kutangaza matokeo ya DNA, na imetishia
kuuchukua mwili huo ili iuzike wiki hii, iwapo serikali itatoa
thibitisho hilo au la.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269