Mamia
ya wananchi wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, jana walijitokeza
kuuaga mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mbinga-Magharibi, Kapteni
John Komba ambao uliwasili majira ya saa 10.25 katika Uwanja wa Ndege wa
Ruhuwiko, mjini hapa.
Baada
ya mwili huo kuwasili kwa ndege ya kukodi mkoani hapa, ulipokelewa na
viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa na serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa
wa Ruvuma, Said Mwambungu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mark Mwandosya
pamoja na baadhi ya wabunge wa Mkoa wa Ruvuma huku baadhi yao wakiangua
vilio kiwanjani hapo.
Baadaye
mwili huo lipelekwa katika uwanja wa michezo wa Majimaji ambapo
wananchi walipata fursa ya kuuaga na kisha kuelekea kijijini kwake
Lituhi kwa ajili ya mazishi ambayo yamefanyika leo.
Msafara
huo kutokea uwanja wa ndege uliongozwa na pikipiki magari ya watu
binafsi sambamba na vikosi vya ulinzi na usalama huku wananchi wakiwa
wamejipanga barabarani kushuhudia mwili huo.
Awali,
kabla ya mwili wa Komba haujaingia uwanjani, waliupitisha katika mitaa
mbalimbali ya Manispaa ya Songea kwa lengo la kutoa nafasi kwa wananchi
ambao hawataweza kufika uwanjani, wapate fursa ya kuaga.
Mkuu
wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu alisema hadi mwili unawasili, bado
wananchi hawakuwa wakiamini kilichotokea kwa kumpoteza mtu muhimu,
makini na mbunifu na mwenye vionjo vya muziki.
Alisema, Komba alikuwa mtu wa watu wote mwenye upendo na mpenda maendeleo na kwamba kifo chake kilikuwa ni cha kushtukiza.
Aliwataka
wananchi mkoani Ruvuma kuwa watulivu na watakaobahatika kwenda kuzika
kijijini, walitakiwa kuwahi kabla ya Rais Jakaya Kikwete hajawasili
Lituhi.
Rais
Kikwete, leo ameongoza mamia ya wananchi kwenye mazishi ya Kepteni
Komba ambapo ilitangulia ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu
wa Jimbo la Mbinga, John Ndimbo.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269